Search This Blog

Saturday, October 5, 2013

AZAM YATOKA SARE NA WAGOSI COASTAL UNION - MECHI YATAWALIWA NA VURUGU


 Leo golikipa wa Azam Mwadini Ally alikuwa na wakati mgumu sana, ingawa bahati haikuwa ya Wagosi.


                             Yayo Kato akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Azam FC.
 Nahodha Jerry Santo akikunjuka nje kidogo ya lango la Azam, ingawa shuti lake halikuleta madhara.
 Kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco akiwabwatukia wachezaji wake wacheze kama alivyowafunza.



 Hili ndilo bao la kipindi cha pili walilokosa Coastal Union, ambapo shuti la Selembe lilipita mikononi mwa Mwadini Ally na kugonga mwamba.


SULUHU ya bila kufungana kati ya Coastal Union na Azam FC katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga imezidi kuwaongezea idadi ya suluhu Wagosi wa kaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo huo uliokuwa na presha kubwa kwa mashabiki na wachezaji ulimuweka katika wakati mgumu mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani, kutokana na kushutumiwa kuwapendelea Azam FC.

Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa nguvu zikihakikisha zinapata mabao ya mapema na kujihakikishia ushindi lakini hakuna hata timu moja iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kushambulia kwa kasi huku wakimiliki mpira hali iliyowachanganya wachezaji wa Coastal Union wakaanza kupoteana na kucheza bila kufuata mfumo. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya Wagosi wa Kaya hasa baada ya mwamuzi kuanza kutoa maamuzi ya utata, kwani katika dakika ya sabini alitoa kona kwa Azam wakati ilikuwa ni goal kick.

Mashabiki wakaanza kuhamaki na kutaka kuvuruga mchezo baada ya mwamuzi kuzidisha kutoa maamuzi ya utata kama faulo zisizoeleweka na kona za utata. Hali hiyo ilimtisha mwamuzi na kusimamisha mchezo mara kwa mara ili kuwataka wasimamizi wa mchezo huo kuwatuliza mashabiki.

Tukio lililotokea kipindi cha kwanza ambapo mwamuzi wa pembeni alipigwa na kitu kisichojulikana kutoka jukwaa la 'Rasha' lilitaka kujirudia kipindi cha pili baada ya chupa na mawe kutupwa uwanjani baada ya mwamuzi kutoa faulo nje kidogo ya 18 upande wa Coastal Union.

Dakika ya 65 mwalimu Hemed Moroco alifanya mabadiliko na kumtoa Pius Kisambale akaingia Suleiman Kassim 'Selembe'. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Wagosi hasa kutokana na aina ya uchezaji wa Selembe kutumia mipira ya kasi.

Azam FC walianza kuelemewa kutokana na Mganda, Yayo Kato kutumia vema mwili wake mfupi na wenye nguvu kuwashambulia mabeki wa Azam, hali hiyo iliwafanya Azam kubadilika na kucheza mpira wa hovyo uliowapa nafasi Coastal Union kupiga mipira mirefu ambapo ilipofika dakika ya 75 kipindi cha pili katika jukwaa la African Sports, Wagosi walikosa bao la wazi baada ya Selembe kupiga krosi iliyopenya ngome ya Azam akiwemo mlinda mlango Mwadini Ally na kugonga mwamba.

Kutokana na piga nikupige ya lala salama kufika dakika ya 74 mwamuzi alimnyooshea mlinzi wa kulia wa Coastal Union, kinda Hamadi Juma 'Basmat', kadi nyekundu baada ya kubadilishiana maneno na mchezaji wa Azam, Kipre Tchetche.

Tukio hilo lilianzia kwa Kipre kumpiga Hamadi kiwiko cha shingo hali iliyomfanya kinda huyo kumfuata kwa jazaba huku akimuuliza kwanini amemfanyia hivyo. Mwamuzi baada ya kuona Hamadi amemuelekezea kichwa Kipre akadhani kinda huyo anapigana ndipo akatoa kadi ya moja kwa moja.

Baada ya kadi hiyo hali ya uwanja ilichafuka ambapo mashabiki walikuwa wakipiga kelele huku wachezaji wakitaka kupigana, ndipo mchezaji mwingine wa Coastal Union beki wa kushoto Othman Tamim akapewa kadi ya njano papo hapo.

Baadaye mchezo ulirudi katika hali yake lakini ngome ya Coastal Union ilikuwa imepwaya hali iliyomfanya Juma Said 'Nyoso' kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha ngome yao inakuwa imara.

Ilipofika dakika ya 84 mwlimu Moroco alifanya mabadiliko kwa kumtoa Uhuru Suleiman na kumuingiza Yusuf Chuma. Ambapo kinda huyo alionyesha uwezo mkubwa na kurudisha uhai wa safu ya ulinzi.

Mpaka mwamuzi wa leo anapuliza kipyenga cha mwisho matokeo yaliendelea kusomeka hivyo hivyohivyo 0-0, na kuendelea kuibakisha Coastal Union katika nafasi ya nne ikiwa na point 11 nyuma ya Azam iliyo nafasi ya tatu yenye point 11 lakini ikiwa na mabao mengi ya kufunga.

Baada ya mechi ya leo Coastal Union itashuka dimbani wiki ijayo katika uwanja wa Chamazi dhidi ya Ashanti United wanaoshika mkia katika ligi
.

HABARI NA PICHA KWA HISANI YA COASTAL UNION BLOG

SIMBA YAVUTWA SHATI LIGI KUU - YATOKA SARE 1-1 NA RUVU SHOTING


 Mshambuliaji wa Simba, Haruna Chanongo akichuana na beki wa Ruvu shooting, stephano Mwasyika. (Picha na Habari Mseto Blog)
 Amri Kiemba akichuana beki wa Ruvu Shooting, Abuu Hashim.
 Hekaheka katika lango la Ruvu Shooting.
 Mshambuliaji wa Simba, Betram Mombeki akimiliki mpira huku akizongwa na beki wa Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Golikipa wa Ruvu Shooting, Abdul Seif akiokoa moja ya hatari langoni mwake.
 Berntram Mombeki akiruka daruga la beki wa Ruvu Shooting, Abuu Hashim. 
Henry Joseph, Abel Dhaira na Joseph Owino wakiteta jambo wakati wakitoka mapumziko. PICHA NA FRNACIS NDADE

Friday, October 4, 2013

HATIMAYE MECHI ZA LIGI KUU KUONYESHWA TBC 1

Azam Media Limited imefanikiwa kukamilisha utaratibu wa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utakaowawezesha mashabiki wa kandanda kote nchini kunufaika kwa kuona michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom kila mwishoni mwa juma hadi kukamilika kwa nusu ya msimu wa 2013/14 kupitia TBC1 kwa hisani ya AzamTV.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (Kamati ya Ligi) wameeleza kuunga mkono utaratibu huu makini.

“Baada ya kupata haki za matangazo ya luninga ya Ligi Kuu ya Vodacom, moja ya shabaha zetu kuu imekuwa ni kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kurusha matangazo yanayokidhi viwango vya kimataifa kwa ubora. Ili kufanikisha shabaha hiyo tumewekeza vilivyo katika teknolojia ya kisasa ya vifaa vya matangazo ya nje (Outside Broadcasting) na katika mafunzo kwa watumiaji wa vifaa hivyo. Ninayo furaha kusema kuwa matayarisho yamekwenda vema kiasi kwamba tumejikuta tuko tayari kurusha matangazo ya kiwango cha juu kabla hata ya kuzinduliwa kwa huduma kamili za AzamTV”, alisema Rhys Torrington, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited.



“Kwa kuwa mashabiki wengi kote nchini wanangojea kwa hamu kubwa kuziona timu wazipendazo, imeonekana ni vema kuanza kuonesha michezo hii ya Ligi sasa. Kwa kuzingatia hali hiyo, nilifanya mazungumzo na rafiki zetu pale TBC na kuwaomba iwapo wana uwezo na kuridhia kurusha matangazo yetu ya moja kwa moja bila ya malipo yoyote kuanzia mwisho wa juma hili hadi kukamilika kwa nusu msimu. Tulifanikiwa kufikia makubaliano kwa haraka na sasa tunafanyia kazi masuala ya kiufundi yatakayowezesha kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi utakaofanyika Uwanja wa Taifa”, Aliongeza Bw. Torrington.

Mara tu huduma kamili za AzamTV zitakapozinduliwa majuma machache yajayo, matangazo ya michezo ya Ligi Kuu kwa wigo mpana yatakuwepo pia kwenye chaneli yake hadi mapumziko ya nusu msimu. Baada ya hapo matangazo ya Ligi Kuu ya Vodacom yatapatikana kwa wale tu watakaokuwa na visimbuzi (decorders) vya AzamTV.

KAMPENI YA NANI MTANI JEMBE SIMBA NA YANGA YAZINDULIWA JIJINI ARUSHA.

 Mfanyakazi wa TBL Arusha, Christopher Kimonge ambaye ni shabiki wa Simba akishiriki kupiga vuvuzela katika hafla ndogo ya kutambulisha kampeni ya Nani Mtani Jembe kwa wafanyakazi hao kabla ya uzinduzi mkubwa utakaofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki. Kampeni hiyo itawashindanisha mashabiki wa Simba na Yanga nchi nzima kwa muda wa miezi miwili kupitia matukio mbalimbali (Picha: Mpiga Picha Wetu, Arusha)

 Mfanyakazi wa Kampuni ya  Bia Tanzania (TBL) kiwanda cha Arusha, Idrisa Athumani akishiriki katika shindano la kupiga danadana katika hafla ndogo ya kutambulisha kampeni ya Nani Mtani Jembe kwa wafanyakazi hao kabla ya uzinduzi mkubwa utakaofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki. Kampeni hiyo itawashindanisha mashabiki wa Simba na Yanga nchi nzima kwa muda wa miezi miwili kupitia matukio mbalimbali. (Picha: Mpiga Picha Wetu, Arusha)

UTUMISHI YAIKUNG'UTA MAHAKAMA,KUCHEZA FAINALI NA IKULU SHIMIWI.

 
Timu ya Mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma .
 Timu ya Mpira wa Pete ya Mahakama kabla ya kuanza mechi kati yake na Timu ya Mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma katika nusu fainali za mashindano ya SHIMIWI mjini Dodoma leo .
 Timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikiomba dua kabla ya kuanza kwa mpambano dhidi yake na timu ya mpira wa Pete ya Mahakama kwenye nusu fainali za mashindano ya SHIMIWI mjini Dodoma mapema
Mchezaji wa timu ya mpira wa pete ya Utumishi Perice Makau (GS)(wa pili kutoka kushoto) akijaribu kutoa pasi wakati wa nusu fainali za mashindano ya SHIMIWI kati ya timu yake na timu ya Mahakama Mjini Dodoma mapema leo.Mbele yake ni wachezaji wa Mahakama Sharifa (WD),Ruth (GD) na Joyce Mfyuji (GK) wakijaribu kukaba mpira usitoke.

UAMUZI KAMATI YA MAADILI KUFANYIWA MAPITIO



Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es salaam.

Hivi sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.

Hata hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.

Sekretarieti si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi yake kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia mapitio (revision) na pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.

Sekretarieti imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia panda baada ya kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo ambalo kwa kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba revision na mwongozo.

Pia mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka mwelekeo mzuri wa masuala ya Maadili katika siku zijazo.

Miongoni mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi zao ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo hapo kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao kwa sababu za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi.

Ili haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti imeona ni vizuri masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa mwongozo ili kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na wadau na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya wagombea.

Uamuzi huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya Maadili, bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo husika pindi inapotokea ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.

Sekretarieti imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa manajiri ya kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia Shirikisho kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.

SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.

Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.

Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine inazopata hapo.

Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.

“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu,” amesema.

Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.

WASHABIKI WENYE SILAHA MARUFUKU VIWANJANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.

Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.

Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.

Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.

Pia tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.

SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu)  kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

FDL KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika viwanja kumi tofauti.

Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea) na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).

Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).

Idara ya Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Mbeya City ikikubali kuwa tawi la Simba au Yanga, imekwisha



KATI ya timu tatu mpya katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu wa 2013/ 14, Mbeya City ndiyo imeanza kwa moto mkali kuliko Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United ya Dar es Salaam.
City imekuwa gumzo nchi nzima na sababu yake ni moja tu, ilizitoa jasho Yanga katika mechi yake mjini Mbeya na Simba katika mchezo wao Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kocha Ernie Brandts wa Yanga hana hamu na Abdallah Kibaden ameivulia kofia timu hiyo.

Katika kipindi hiki ambapo Tukuyu Stars ‘imepotea’, Mecco imekufa na Prisons ikichechemea, City ndiyo imewaunganisha wapenzi wa soka katika mkoa wa Mbeya. City ikicheza katika dimba la Sokoine huunganisha hata pande hasimu za kisiasa na kuishangilia timu hiyo ambayo ilinunuliwa na jiji la Mbeya kutoka kwa Rhino ya Arusha.

Kimsimamo, City iko nafasi ya nane ikiwa na pointi nane kutokana na mechi sita ilizocheza, pointi moja nyuma ya Yanga iliyoko nafasi ya tano. Mbeya City imeshinda mechi moja na imetoka sare tano, haijafungwa hata mechi moja.
City ikishinda mechi ya keshokutwa dhidi ya Oljoro JKT na Yanga ikafanya vibaya dhidi ya Mtibwa Sugar, inaweza hata kuchupa nafasi ya pili. Hata hivyo itategemea matokeo ya mechi nyingine kati ya Kagera Sugar na JKT Ruvu.

City iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1 na kutoka sare na Yanga (1-1), Simba (2-2), Azam (1-1), Coastal (1-1) na Kagera (0-0). Kiuchezaji Mbeya City huonekana wakipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
City namilikiwa na kusimamiwa vizuri na Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Mashabiki wa Simba na Yanga sasa ‘wamepungua’ jijini Mbeya na wote huishabikia na kuiunga mkono City kutegemea inacheza na timu ipi. Iko huru haijajipambanua kuwa tawi la Yanga au Simba, jambo linalosababisha klabu nyingi za mikoani kusambaratika.

Mmoja wa wachezaji wa City, kiungo mshambuliaji Richard Peter anathibitisha kwa kusema hawana ushabiki wala uhusiano na timu yoyote ya ligi kuu ndiyo maana wameweza ‘kuzibania’ timu zote walizokutana nazo.
“Hatuna urafiki wala undugu na timu yoyote hata hizo Simba na Yanga hatuna urafiki nazo, ndiyo maana tumeweza kuzibana na kutoka nazo sare. Hatuwezi kuwa tawi la Simba au Yanga, sisi tunatazama zaidi katika ushindi na kufanya vizuri katika ligi na si vinginevyo,” anasema Richard.

Jijini Mbeya, kila unapokaribia mchezo wowote wa  City, jiji la Mbeya hupambwa kwa rangi ya zambarau ambazo ndizo zinazotumiwa na timu hiyo na hata unapoingia uwanjani, mashabiki wa timu ni wengi na wakati mwingine hufikia hatua ya kukaa sehemu zilizozoeleka kukaliwa na mashabiki wa Simba au Yanga.

Idadi ya mashabiki wanaojitokeza uwanjani kutazama mechi za City na ushahidi ni mapato ya mlangoni. Mechi ya City na Yanga hivi karibuni iliingiza zaidi ya Sh. 93 milioni wakati Yanga na Prisons kilipatikana kiasi chini ya hicho. Hii ina maana mvuto wa City ni mkubwa kuliko Prisons.
Nje ya uwanja, Mbeya City ni timu yenye mashabiki wenye hamasa kubwa ya kuishangilia na hata matajiri hujisikia raha kuichangia na kusafiri nayo kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam kuipa nguvu.

Ndani ya uwanja, Mbeya City ni timu yenye nidhamu kubwa ya mchezo na hata kocha wake, Juma Mwambusi anakiri kuwa wachezaji wake ni wasikivu na wenye hamasa ya hali ya juu kutaka kuona timu yao inafanya vizuri.
“Tupo kama kitu kimoja na tunasikilizana wakati wote, tumekaa pamoja kwa muda mrefu na ndiyo maana leo hii tunafanya vizuri katika ligi. Hakuna kitu kingine cha ziada ukiacha hilo na wananchi kuiona ni timu yao hivyo wanapaswa kuiunga mkono wakati wote,” anasema Mwambusi aliyewahi kuinoa Prisons.

Wachezaji wanaonekana wenye pumzi na wanaocheza kwa malengo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo jambo ambalo Mwambusi anasema ni matokeo mazuri ya mazoezi ya kujiandaa kwa msimu huu wa ligi.
City inaonekana imejipanga zaidi ndani na nje ya uwanja, lakini inaweza kuingia katika matatizo na kupoteza mwelekeo wake endapo itaingia katika mkumbo wa kukubali kutumiwa na moja ya klabu za Simba na Yanga.