Wanasema si sahihi kufananisha vizazi tofauti kwenye soka, kila staa anadumu kwa wakati wake na uzito wake. Lakini kwenye soka hili limekuwa halikwepi, kila siku tunawafananisha Messi au Maradona? Pele au Ronaldo? Ni mjadala unaozidi kuwa mkubwa kila siku iendayo kwa mungu.
Wakati tuliopo kwenye kizazi cha soka, linapokuja suala la wafungaji bora wa muda wote wa timu za taifa, kuna namba kubwa ya timu kubwa ambazo aidha tayari zina wachezaji wapya ambao ndio wafungaji bora wa muda wote au zinakaribia kufanya hivyo hivi karibuni. Inavyoonekana kipindi cha miaka 10 kutoka 2007 mpaka 2017 kinaweza kukumbukwa kama ndio kipindi ambacho historia ziliandikwa upya. Tayari historia zimeanza kuandikwa kuanzia Uruguay, France, Cote d'Ivoire, Spain na United States na pia Germany, Portugal na Holland zipo karibuni kupata wafalme wapya waliofumania nyavu mara nyingi wakiwa na jezi ya timu ya taifa husika, pia England, Sweden, Mexico and Argentina zinaweza zikafuatia.
Miroslav Klose kwa sasa ni majeruhi lakini amebakiza goli moja tu kuweza kuifikia rekodi ya gwiji Gerd Muller ambaye aliifungia Ujerumani mabao 68, wakati Kloseana mabao 67. Inavyoonekana hawezi kustaafu bila kuifikia rekodi hiyo.
Akiwa hajafunga mechi kadhaa ndani ya klabu ya Manchester United, Robin Van Persie amekuwa na hali tofauti ndani ya timu ya taifa ya Uholanzi, katika mechi za hivi karibuni amefunga mabao 3 katika mechi 2 dhidi ya Romani na Estonia, hivyo kufanikiwa kumpita Johan Cruyff kwenye listi ya wafungaji bora wa uholanzi , huku akifanikiwa kumfikia Klaas-Jan Huntelaar wote wakiwa na mabao 34. Van Persie na Huntelaar wote wanatimiza miaka 30 kipindi kijacho cha kiangazi na wote wanapigania namba ndani ya kikosi cha Van Gaal, wote wana nafasi ya kuifikia rekodi ya mabao 40 iliyowekwa na Patrick Kluivert.
Kijana mwingine ambaye anakaribia kuifikia rekodi iliyopo kwenye timu yake ya taifa ni Cristiano Ronaldo. Anashika nafasi ya tatu kwenye listi ya wafungaji bora wa muda wote wa Ureno, akiwa na mabao 38, nyuma ya Eusebio aliyemzidi matatu na Pauleta aliyemzidi tisa - lakini Ronaldo ndio kwanza ana miaka 28 aliyotimiza mwezi uliopita.
Kwa upande wa mabingwa wa dunia na ulaya Spain, David Villa tayari ameweza kuwa mfungaji bora wa muda wote wa La Furia Roja akiwa na mabao 53, akimpita Raul miaka miwili iliyopita. Ana miaka 31, hivyo tutegemee kuona idadi hiyo ikiongezeka mpaka siku atakapostaafu.
Mwezi October 2011, Diego Forlan alimpita mkongwe Hector Scarone -- shujaa wa Copa America 1920s na kombe la dunia mwaka 1930 -- na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Uruguay. Lakini mazingira yaliyopo yanayoonyesha kwamba Forlan, ambaye ana mabao 33, atapitwa siku chache zijazo na mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez mwenye mabao 31, na akiwa na miaka 7 pungufu kuliko aliyonayo Forlan.
Rekodi ya Michel Platini ya ufungaji bora wa muda wote kwa Ufaransa ilivunjwa mwaka 2007 wakati Thierry Henry, wakati huo akiwa na miaka 30, alimpita Platini aliyekuwa na mabao 41. Henry amestaafu kuichezea Les Bleus ingawa rekodi yake ya mabao ya 51 itaendelea kudumu kwa muda fulani. Mfungaji bora wa muda wote wa Cote d'Ivoire ni Dider Drogba ambaye ana mabao 60.
Penginepo? Wayne Rooney ana mabao 35 ndani ya jezi ya England. Ana miaka 27 na rekodi ya England inashikiliwa na Sir Bobby Charlton mwenye mabao 49, hivyo Rooney anahitajika kufunga mabao 15 ili aweze kuivunja rekodi hiyo. Zlatan Ibrahimovic ana mabao 31 na anahitaji mabao mengine 10 kuifikia rekodi ya Sven Rydell, jambo hilo linawezekana kwa kiwango alichonacho Zlatan hivi sasa.
Halafu kuna Lionel Messi: Gabriel Batistuta, ndio mfungaji bora wa muda wote wa Argentina akiwa na mabao 56. Lakini mwenye umri wa miaka 25 tayari ana mabao 32, anahitaji mengine 24 kuifikia rekodi ya Batgoal.
Mexico pia wanakaribia kumpata mfungaji bora mpya: Javier Hernandez ana mabao 30 -- anayeshikilia rekodi Jared Borgetti ana mabao 46 -- lakini Chicharito bado mdogo sana akiwa na miaka 24.
Timu kubwa ambazo inaonekana itakuwa taabu sana kwa rekodi za wafungaji bora wa muda wote kubadilika hivi karibuni ni Brazil na Italia. Pele aliweka nyavuni mipira 77, anayemfuatia Ronaldo ameshaastafu, huku kwa upande wa Italy rekodi ya mabao 35 ya Gigi Riva itakaa sana mpaka Mario Baloteli aje kuifikia.