KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Abdallah Kibaden inaelekea amejiuliza “makocha wazungu wanaweza wana nini, na makocha wazawa wanashindwa wana nini?”
Msimu uliopita, akiwa kocha mkuu wa klabu ya Kagera Sugar ya Bukoba alihakikisha inazichapa klabu za Simba ya Yanga ambazo zilikuwa zinanolewa na makocha wazungu katika Ligi Kuu ya Bara.
Msimu huu, Kibaden aliitosa Kagera Sugar akaingia mkataba na Simba. Klabu hiyo na nyingine inazoshiriki Ligi Kuu zinafanya vizuri tofauti na zile zinazofundishwa na wageni au makocha wa Kizungu.
Simba ndiyo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 11, ikifuatiwa na JKT Ruvu iliyo chini ya mzawa Mbwana Makata yenye pointi tisa.
Hadi mzunguko wa tano Jumapili iliyopita, timu zinazonolewa na makocha wageni zinaonekana kuchechemea. Azam FC iliyo chini ya Mwingereza, Stewart Hall ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa huku Kagera Sugar inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja ikiwa nafasi ya sita na pointi nane.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga chini ya Ernie Brandts raia wa Uholanzi, ipo nafasi ya nane ikiwa na pointi sita. Timu zote hizo zimecheza michezo mitano.
Kwa muda mrefu Simba ilikuwa chini ya makocha wa kigeni hasa wazungu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya, wa mwisho wa kigeni alikuwa raia wa Ufaransa, Patrick Liewig.
Simba haikuwa katika kiwango chake chini ya kigeni hasa kuanzia miaka hii ya 2000, na hata mwaka huu ilipoachana na Liewig haikuwa katika kiwango cha kuridhisha.
Ukimwacha Patrick Phiri wa Zambia aliyewahi kuipa ubingwa klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, makocha wengine kama Neider dos Santos (Brazil), Nielsen Elias (Brazil), Krasmir Benzinski (Bulgaria), Milovan Cirkovic na Liewig hawakuwa na matokeo ya uhakika japokuwa timu ilikuwa ikipata ushindi na hata ubingwa.
Hata makocha wageni waliofanikiwa katika kikosi hicho, mara nyingi wasaidizi wao walikuwa wazawa kama Amri Said, Kibadeni na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’. Kazi kubwa ya wazawa ni kuwa kiunganishi kati ya kocha na wachezaji.
Kitu kinachoitafuna Simba inayoundwa na wachezaji wengi chipukizi, ni saikolojia. Vijana wengi wanaonekana kucheza vizuri, lakini bado hawajiamini wawapo uwanjani.
Hilo huwa jukumu la kocha na benchi zima la ufundi (wasaidizi hasa), lakini kwa vile benchi la ufundi linadhibitiwa na wazawa Kibadeni na Julio, inawawia rahisi kuzungumza nao kwa Kiswahili kuwaweka sawa vijana hao ambao sasa wanafanya vizuri. Ukiwachanganya na wazoefu kama Hamisi Tambwe, Henry Joseph na Amri Kiemba, Simba sasa ipo moto.
Inapotokea kocha wa kigeni akawa na jukumu moja tu la kufundisha timu na kurudi hotelini, huku akiwa hana muda wa kutazama hali za kisaikolojia za wachezaji wake huku akishindwa kujua matatizo ya wapiganaji wake, mambo huwa tofauti uwanjani.
Itazame Yanga sasa, inaonekana moto uwanjani kutokana na kuwa na wachezaji wengi wazoefu huku uwepo wa kocha msaidizi Fred Minziro ukisaidia kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji wote.
Katika miaka ya 2000, Yanga imewahi kufundishwa na Jack Chamangwana (Malawi), Milutin Sredojevic ‘Micho’, Dusan Kondic, Kosta Papic (wote Serbia), Sam Timbe (Uganda), Tom Saintfiet (Ubelgiji) na Brandts raia wa Uholanzi ambaye hadi sasa anainoa timu hiyo.
Mara nyingi makocha wote hao wamepata mafanikio kutokana na usaidizi wa karibu na makocha wazawa. Na mbaya zaidi makocha hao wazawa wengi wao wana elimu ama zinazolingana au zinazokaribiana na zile za makocha wa kigeni.
Tatizo linaloikabiri Simba inapokuwa na makocha wa kigeni ni lile lile lililopo kwa makocha wa Yanga. Tena mbaya zaidi kwa timu hizi, ni kuwa na lundo la wachezaji ambao lugha ya Kiingereza inakuwa tatizo kwao.
Ukichanganya kocha wa kigeni kutokuwa na mazoea ya kutazama hali ya kisaikolojia kwa wachezaji ambao hawana msingi wa kufundishwa, halafu tatizo la lugha likihusika hapo timu lazima itayumba hata kama inakuwa na mwalimu mwenye ujuzi mwingi.
Makocha hawa wa kigeni hasa wasiofahamu lugha ya Kiswahili, hupenda kuwatumia wazawa kama wakalimani, hapo ndipo tatizo linapotokea. Katika hali ya kawaida, tafsiri inaweza kuwa tatizo, kile anachomaanisha kocha si kinachowafikia wachezaji.
Tazama Azam ikiwa chini ya Hall, bila ya ushindi wa mechi ya wikiendi iliyopita dhidi ya Yanga, mambo yangekuwa tofauti. Ana kikosi kilichosheheni wachezaji kutoka sehemu kubwa ya Afrika lakini mambo bado ni magumu.
Kuwa na wachezaji bora kunasaidia kutengeneza timu bora. Azam yenye wachezaji bora ama wachezaji hawauelewi mfumo au haukubaliki. Pia mambo mengine nje ya uwanja yanachangia hasa kutokana na tabia ya misimamo ya kocha.
Aidha, kuna matatizo katika mfumo wetu wa soka. Kuna wakati mchezaji anafika Yanga au Simba bado anafundishwa namna ya kukokota mpira. Kwa nini? Sababu ni kwamba walisajiliwa si kwa ubora bali ‘kufanikiwa’ kuzifunga Simba na Yanga na ghafla anateuliwa Taifa Stars.
Kibaden anajua udhaifu wa mfumo, anajua kuurekebisha. Hata hivyo, mfumo wa uongozi Simba na Yanga unawapenda akina Kibaden klabu ikichacha au ikiwa haipo kwenye mashindano ya kimataifa. Wakati mwingine klabu zetu huona ufahari kuwa na makocha wa kigeni hata kama hawaongezi thamani yoyote katika Ligi Kuu ya Bara.