Search This Blog

Friday, September 27, 2013

TUNAWAENDELEZAJE WACHEZAJI WETU WANAOIBUKA KWA MTINDO WA WAYNE ROONEY?



Na Baraka Mbolembole 
Miaka 11 iliyopita soka la Uingereza lilimpokea mchezaji ‘ wa aina yake’, wakati timu ya Everton ikicheza na Arsenal katika mchezo wa ligi kuu, mwanzoni mwa msimu wa 2002/ 03. Alikuwa ni kijana wa miaka 16 ambaye kocha David Moyes ( wakati huo) alimuinua katika bechi la wachezaji wa akiba, na kwenda kufunga ‘ bao kali la mkwaju wa mbali’, Everton ikashinda mchezo huo kwa mabao 2-1, lakini habari kubwa ilikuwa ni Wayne, alikuwa ni mchezaji kijana zaidi kuwahi kufunga bao katika historia ya ligi kuu ( wakati huo).

‘ PELE mweupe’ alifikia hatua ya kufananishwa hivyo kutokana na kile alichokionesha uwanjani. Ni mmoja wa wachezaji bora ‘ namba kumi’ anayeweza kucheza katika mfumo wowote na kutoa matunda. Mtaalamu wa mashuti ya mbali ( kabla hajaumia sehemu ya enka yake mara mbili) Rooney angeweza kufunga bao hata akiwa umbali wa mita 30, anaweza kufunga akitokea pembeni, iwe upande wa kulia au kushoto, pia anakuwa hatari zaidi katika eneo la ushambuliaji wa kati. Alijiunga na Everton wakati akiwa mtoto mdogo, na akapandishwa katika kikosi cha wakubwa na kuwa mchezaji wa kulipwa, 2002. Akatumia misimu miwili katika klabu hiyo ya ‘Mersyside’ kabla ya kujiunga na Manchester United, wakati wa majira ya kiangazi, 2004.
Kuanzia hapo ameweza kushinda mataji matano ya ligi kuu England, taji moja la Mabingwa wa Ulaya, lingine moja la Klabu bingwa ya dunia, huku akiwa na medali mbili za ushindi wa pili katika ligi ya mabingwa Ulaya na mbili za ligi kuu England, na mapema mwezi huu aliifungia United bao la 201 na kuwa mfungaji bora wanne wa muda wote katika timu hiyo ya Old Trafford. Akiwa na medali nyingine za ushindi wa vikombe vya FA, Capital One, Ngao ya Jamii na tuzo nyingi binafsi ambazo amezipata akiwa na United.
Katika ngazi ya soka la Kimataifa, Wayne alianza kuichezea England, mwaka 2003 na hadi sasa ameicheza jumla ya michezo 84 na kuifungia mabao 36, akiwa karibu kuvunja rekodi ya muda wote ya ufungaji katika kikosi cha ‘ The three l.ions’, mabao manne nyuma ya Michael Owen, aliyefunga mabao 40, na 13 nyuma ya kinara Bobby Charlton ambaye alifunga mabao 49. Aliweka rekodi ya mchezaji mdogo zaidi kuiwakilisha England ( kabla ya Theo Walcott) kuvunja rekodi hiyo, ni ni mchezaji mdogo zaidi kufikisha michezo 50 ya kimataifa kwa upande wa England. Rooney aliweka redi ya mfungaji bora zaidi kijana katika historia ya michuano ya Euro. Alifanya hivyo mwaka 2004 katika michuano iliyopigwa nchini Ureno. Wayne ni mshindi binafsi, akiwa tuzo tano za mchezaji bora wa mwezi wa ligi kuu, sambamba na Steven Gerrard, wawili hao ndiyo wenye rekodi ya kutwaa tuzo hiyo mara nyingi zaidi. Rooney msindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mara mbili ( 2008, 2009) Ameshiriki mara tano katika tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Na ameiwakilisha England mara mbili katika fainali za kombe la dunia, 2006 na 2010, pia amecheza fainali mbili ya Euro, 2004 na 2012.

YUPO WAPI HERRY MORRIS? NAOMBENI REKODI YAKE YA UCHEZAJI 
Ninakumbuka wakati ule Rooney akichomoza katika klabu ya Everton, nchini Tanzania katika timu ya Tanzania Prison ilikuwa na rundo la wachezaji bora, kuanzia kwa Dixon Osward, Samson Mwamanda, Osward Morris na wengineo, kiburudisho kilikuwa wakati mpira ukiwa katika miguu ya kiungo Primus Kasonso, Misango Magae ‘ Diego wa Mbeya’, au kwa mshambuliaji kinda wakati huo, Herry Morris ( mdogo wake na Osward) Morris alikuwa mfungaji mwenye kipaji hasa cha kufunga, aliweza kufunga akitokea kulia, kushoto au katikati, alikuwa akitega na kuivunja ‘ mitego ya offside’ na akatamba kwa staili yake ya kufunga mabao ya kuvutia. Achana na Morris, katika timu ya CDA ya Dodoma kulikuwa na mshambuliaji mmoja hivi, Dominick Meshaki, aliwafunga Simba, Yanga popote pale alikuwa na mashuti, uwezo wa kumili mpira na kasi ambayo mshambuliaji anatakiwa kuwa nayo, katika timu ya Mtibwa kulikuwa na Nicco Nyagawa, kuna mtu anaweza kusema Nicco hakuwa bora sana kama mchezaji wa kiungo lakini wakati yupo Mtibwa alipata uzoefu kutoka kwa kina Monja Liseki, Thomass Masamaki ( marehemu), na kinda mwenzake Abuu Mkangwa, Nicco alikuwa na shabaha hasa, kipaji kizuri cha ufungaji na mchezaji mwenye nidhamu muda wote. Hawa ni wachache tu kati ya wengi ambao hawakutamba kwa muda mrefu na kupotea.
KWA NINI ROONEY YUPO HERRY HAYUPO 
Tumekuwa tukiwatumia wachezaji wetu kama ‘ nguo tu’ . Wakati nikichezea timu ya Burkina Faso ya Morogoro, 2008 nilipata bahati ya kukutana na mmoja wa wachezaji wa Prisons ambao walikuwa ni sehemu ya wachezaji wa kikosi cha Herry. Niliwahi kumuuliza ni kwa nini hawakuweza kutwaa ubingwa wa Bara, 2002 wakati nafasi ilikuwa ni yao. Prisons wakati huo ilikuwa ikihitaji sare tu ili kuwa mabingwa lakini wakapigwa mabao 4-1 na Yanga ambao hawakuwa na nafasi wakatwaa ubingwa mbele yao. Aliniambia kwa uwazi kuwa tatizo lilikuwa ni kuwepo kwa watu wa Yanga katika timu yao. Aliniambia wakati Yanga ikipata bao la tatu, aliyekuwa kocha wa Prisons wakati huo, alitaka kushangilia kutokana na mapenzi yake kwa Yanga. Ila akajikaza, ‘ wajanja’ walikuwa tayari wameshtukia, wakajifanya hawajui, timu ilikuwa ikicheza vibaya uwanjani, wachezaji waliokuwa wakitegemewa walikuwa katika benchi na wale ambao walikuwa na msaada wa wastani kwa msimu mzima walikuwa ndani ya uwanja. Wakapigwa bao la nne, kwa maelezo ya mchezaji huyu ambaye alikuwa katika bechi wakati huo, ni kwamba kocha wao ( Prisons,) alikwenda katika moja ya vyoo vya uwanjani hapo na kujifungia ndani . Unafikiri alipatwa na haja, hapana. “ Watu walimkuta anashangilia kwa kurukaruka chooni” . Unajua ukiwa mbali sana na wahusika wa mpira wetu unaweza kufikiri muda wowote timu zetu zitacheza fainali ya vilabu Afrika na pengine kutwaa taji hilo ‘ ambalo ni ndoto isiyokuwepo kwa wenye dhamana ya kuviongoza vilabu vyetu’.

Hata mimi naunga mkono, Simba kwanza, Yanga kwanza, nyingine zifuatie. Ila inakuwaje kocha ambaye anakuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wa nchi na kung’arisha ‘ CV’ yake anaingia katika mkumbo wa kupanga kikosi ‘ kibovu’ katika mchezo muhimu ili timu anayoishabikia itwae taji. Bahati mbaya hali hii imekuwa ikifanywa na wale wenye mapenzi na Simba au Yanga, siyo mapenzi ya maendeleo hapana, bali kulinda nyazifa zao katika klabu zao.

Kumekuwa na ahadi ambazo baadhi ya wachezaji wa timu ‘ ndogo’ ambazo zinakuwa na nafasi ya kufanya vizuri katika ligi na pengine kutwaa ubingwa kuahidiwa kusajiliwa na timu kubwa kama ‘ tu wataregeza’ ili timu zao zifungwe na timu kubwa. Rejea kuhusu Prisons, na baadae Moro United, 2005 kuna rundo la wachezaji waliisiwa kuziumiza timu hizo kwa sababu ya kupata nafasi katika timu zetu kubwa. Kumbuka wachezaji wangapi walikwenda Yanga kutoka Prisons, 2002 na waliotoka Moro United kwenda Yanga, 2005. Hapa hatuwaendelezi wachezaji wetu vijana zaidi ya kuwashusha thamani.

“ Fabio ( Capello) mimi ni kichaa, nimetoka kutumia kiasi kikubwa cha pesa kumsajili mchezaji yosso” ni maneno ya Sir Alex Ferguson alipokutana na kocha Fabio Capello wakati wa upangaji wa makundi ya ligi ya mabingwa, agosti, 2004 jijini Lyon, Ufaransa. Ferguson alikuwa ametoka kumsaini Rooney kwa ada ya uhamisho euro 25 million ambayo ilifikia hadi euro 27 million na pamoja na matatizo yake yote ya kinadhamu fergie aliweza kumfanya Rooney kuwa mchezaji bora. Alimsimamia na kumuongoza hata alipokuwa akisumbuliwa na mambo ya nje ya uwanja, ulevi, ufuksa na mambo ambayo wakati Fulani yalitishia usalama wa kipaji chake, bado Fergie alimthamini na kutambua umuhimu wa Rooney.

Kwa nini wachezaji wetu hawadumu kwa muda mrefu. Hata Ulaya wapo wa auina hiyo, lakini bado wachezaji wakorofi kama Nigel De Jong, Mario Balotelli, Joey Barton wanaendelea kuthaminiwa na makocha wa timu zao. Wanajaribu kuwasimamia kwa mambo mengi kubwa wakitaka kupata kile walichonacho ili kuwasaidia katika kuwaweka salama kazini mwao. Lakini sisi tuna matatizo mengi. Wachezaji wenyewe hawana imani. Hawaamini kama kuwa wakati kiwango kinaweza kushuka na kupanda tena, hawaamini kama kuna kuumia katika soka. Wao wanapopata majeraha ya mara kwa mara hufikiri kuwa wamerogwa. Vipi Owen alirogwa na nani? Phillipo Inzaghi je, vipi kwa Ricardo Kaka’? Imani inasaidia. Katika soka ni lazima kuwe na ratiba ya kumpumzika, kutembea na kufanya kazi.

Tatizo linguine ni viongozi kushindwa kuwasimamia wachezaji vijna, viongozi namaanisha kuanzia katika benchi la ufundi hadi ule wa juu, kama tunakuwa tunawaona wachezaji wa nje walio na tabia mbaya wanadumu katika soka kwa kipindi kirefu bila shaka wana wasimamizi wazuri wa ndani ya uwanja. Wako wapi kina Abuu Ramadhani, Omari Matutta, Julius Mrope, Yussuph Soka, na wengine? Karibu Joseph Kimwaga katika soka la Tanzania, mchezo wako umezungukwa na Simba, Yanga kila mahali, wanaweza kukutumia wanavyotaka kama hautakuwa makini, ila ukipata msimamizi mzuri unaweza kucheza kwa muda mrefu kama Wayne Rooney, ana miaka 11 katika soka la kulipwa na umri wa miaka 28 tu. Kama kocha wa Prisons, 2002 hakutaka kuona timu yake ikichukua ubingwa mbele ya Yanga, kama Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Wazir Mahadhi, na Lulanga Mapunda walikosda ubingwa wakiwa Moro United, 2005 baada ya kukosa pointi 15 katika michezo 15 ya raundi ya pili, wakati walimaliza raundi ya kwanza wakiwa na pointi 45 baada ya kushinda michezo yote, basi nitaendelea kuweka kete yangu kwa Simba au Yanga. Kila mahali zipo hadi katika mifuko na mioyo ya wachezaji wa timu nyingine, ila Wayne ni motto wa ‘ Mersyside’ anatangaza kipaji chake na kufanya kazi akiwa Manchester. Herry Morris aliondoka na rekodi ‘ mbovu kabisa katika soka, tunawatazama vijana wa sasa wenye majina ‘ mazito’ katika masikio yao, na midomo ya mashabiki wa klabu zao. Daima Rooney alishindwa kufanana na Pele, nap engine sifa za kuitwa ‘ Pele mweupe’ hakustahili kupewa ila atabaki Wayne Rooney, mwenye kipaji, usongo wa mataji na kiu ya mafaniko. Sijui ni vipi kwa Ramnadhani Singano ‘ Messi’. Rooney tayari ana mabao 201 OT.... 0714 08 43 08

No comments:

Post a Comment