Search This Blog

Friday, December 23, 2011

YAYA TOURE NDIYE MWANASOKA BORA WA AFRIKA 2011


KIUNGO wa Ivory Coast Yaya Toure (28) ametawazwa kuwa mwanasoka bora wa Afrika kwa mwaka 2011 kupitia tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na kufanyika katika ukumbi wa Banquet uliopo ndani ya Ikulu ya Ghana.
Toure anayekipiga katika klabu ya Manchester City ya Uingereza alitwaa tuzo hiyo baada ya kupata kura nyingi na kuwapiku nyota wenzake aliotinga nao fainali, Mghana Andre Ayew na Seydou Keita wa Mali .

Mbali na tuzo hiyo pia kulitolewa tuzo mbalimbali kama ifuatavyo:

Mchezaji bora wa mwaka (anayekipiga Afrika):
-Oussama Darragi (Tunisia).

Mchezaji bora (Wanawake)
- Perpetua Nkwocha (Nigeria)

Mchezaji anayechipukia:
- Souleymane Coulibaly (Ivory Coast)

Mwamuzi bora:
-Noumandiez Doue (Ivory Coast)

Kocha Bora:
-Harouna Doula (Niger)

Timu bora ya Taifa (Wanawake):
-Cameroon

Klabu bora:
- Esperance ya Tunisia)

Nidhamu ya Mchezo:
-Libya

Tuzo ya Heshima:
-Mustapha Hadji( Morocco) na Austin ‘Jay-Jay’Okocha ( Nigeria)

source:
http://mamapipiro.blogspot.com/

Thursday, December 22, 2011

JABIR AZIZ: Atoa bao lake la Brazil kwa Maximo na mkewe.

IKIWA imepita takribani miaka miwili tangu timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilipoandika rekodi ya kufungwa mabao 5-1 na Brazil, huku bao lake pekee likifungwa na chipukizi Jabir Aziz.
Nimepata nafasi ya kuzungumza na kiungo huyo anayeunda kikosi cha Taifa Stars tangu mwaka 2008 na kutueleza maisha yake akiwa ndani na nje ya uwanja.

Jabir mbali ya kuwa mwanasoka, ni mwanariadha mzuri na mtunza familia yake muda wote.


Kitu gani kilikufanya hadi ukaamua kuwa mcheza soka?
Jabir:Maisha yangu tangu utotoni yalinipelekea hadi nikaamua kucheza soka kwa sababu nilianza kutumia kipaji changu tangu nikiwa shuleni.


Ulianza kucheza mwaka gani?
Jabir: Niseme nilianza rasmi mwaka 2002 kipindi ambacho nilikuwa nacheza katika timu ya DYOC iliyopo Sigara, Chang'ombe mwaka huo huo tulichaguliwa kuunda timu ya Tanzania kwa vijana waliochini ya miaka 15 ambapo nilishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa ya ‘Gothia Cup’ kwa vijana iliyofanyika Denmark na Sweden.
Mwaka uliofuata tulichaguliwa tena kushiriki katika michuano hiyo ambayo kila tunaposhiriki huwa tunachukua ubingwa.




Mlikuwa na wachezaji gani?
Jabir: Kipindi hicho nilikuwa na miaka 14, nilicheza na wachezaji wengi sana baadhi yao ni Adam Kingwande (aliwahi kucheza Simba na sasa anaelezwa kuwa African Lyon), Ramadhan Chombo 'Redondo' wa Azam FC, Seif Mlanzi na Jabir Khalid Badra 'Dude'
.

Tuambie kuna wakati ilisemekana wewe na wenzako mliitoroka timu ya Taifa hiyo ya DYOC mlipokuwa Denmark, ilikuwaje?
Jabir: Umenikumbusha mbali sana, wakati tulipokwenda katika michuano ya vijana ya mwaka 2003 nikiwa kidato cha pili, tulishawishiwa tukacheze nchini Norway ambako soka lao lipo juu, na sisi kweli tukakubali, siku timu yetu ya DYOC ilipoondoka kutoka Denmark kwenda Sweden nasi tukatoroka kwenda Norway. Tulikuwa wachezaji watano, mimi, Chombo, Seif Mlanzi, Jabir Khalid na Godfrey Benedict.

Maisha ya Norway yalikuwaje?

Jabir: Tulipoondoka uongozi wa timu yetu ulianza kututafuta lakini hawakutupata, tulipofika Norway tulipata timu za ligi daraja la nne, mimi nilipata timu ya FK Vang na Chombo akapata timu ya Lindal.

Ilikuwaje tena ukawa mwanariadha?
Jabir: Unajua kipindi hicho tunatoroka nilikuwa mdogo kiasi ambacho sitakiwi kucheza katika ligi kutokana na kuwa mdogo, hivyo nikajiunga na timu ya riadha inayoitwa Renning Hill, nilikaa na timu hiyo tangu mwaka 2004-2006 nikiwa mchezaji na mkimbiaji riadha mbio ndefu.

Ikawaje hadi mkarudi nchini?
Jabir: Chombo cha serikali kipo kila mahali, wakati tupo kule tulikuwa tukifuatiliwa sana na serikali ya Tanzania, pia kuishi nchi za watu bila kibali ni tabu sana lakini kwa kuwa tulikuwa wachezaji haikutusumbua sana.
Baada ya serikali yetu kugundua sehemu tulipokuwa ikaamriwa turudishwe nchini mara moja, ndipo mimi na wenzangu tuliporejeshwa nchini Oktoba mwaka 2006.

Uliporejea nchini maisha yako ya mpira yalikuwaje?
Jabir: Baada ya kurejea nchini nilijiunga na timu yangu ya mtaani ya Friends Rangers ambayo baada ya muda mchache nikasajiliwa na klabu ya Ashanti United ya Ilala katika dirisha dogo la usajili wakati ilipokuwa ikicheza ligi kuu, lakini timu hiyo ilishuka msimu uliofuata wa 2007/08
.

Baada ya hapo?
Jabir: Nikiwa na Ashanti United kiwango changu kilikuwa kizuri, nikapata nafasi ya kujiunga na Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili, kipindi hicho nilikuwa na wenzangu Juma Jabu na Adam Kingwande.

Ilikuwaje ukatoka Simba na kwenda Azam FC?
Jabir: Nilihamia Azam FC baada ya kumaliza mkataba wa miaka miwili na Simba, hivyo Azam FC wakaonesha nia ya kunihitaji na kwa kuwa mkataba ulikuwa umeshaisha nikaamua kujiunga na Azam FC.


Hii itakuwa timu yako ya tatu katika ligi kuu, ni tofauti gani unaiona kutoka timu zote?
Jabir: Maisha ya mpira yanafanana kwa kiasi fulani, lakini kuna vitu vichache ambavyo vipo tofauti kidogo.


Nafasi yako katika timu ya Taifa ikoje?
Jabir: Nilianza kuitwa katika timu ya Taifa nikiwa nacheza na Ashanti United, na nilipoenda Simba nashukuru nilipata nafasi hiyo tena.



Kitu gani unadhani kilipelekea wewe kutopata nafasi ya kucheza mechi nyingi za timu ya Taifa?
Jabir: Unajua kipindi naingia Taifa Stars kulikuwa na wachezaji wakongwe na sisi chipukizi, hivyo nafasi yetu ilikuwa kupata uzoefu na timu ya Taifa, hivyo tulikuwa tukipewa nafasi chache hasa katika mechi za kimichuano.
Nakumbuka nikiwa na Taifa Stars nimecheza mechi kadhaa ikiwemo Kombe la Africa Mashariki na Kati (Challenge Cup) na mechi dhidi ya Mauritius katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2010.


Wewe ni maarufu sana kucheza ukitokea bench yaani 'Super Sub', unalizungumziaje hilo?
Jabir: Kutokea benchi ni utaratibu wa kocha, huwa anachagua wachezaji wa kuunda kikosi cha kwanza na sisi tunakaa benchi, huwa naichukulia hiyo kama nafasi pia kwani kuna wengine hata benchi huwa hawakai wanaishia katika mazoezi tu.



JABIR AZIZ ( KUSHOTO ) ALIPOKUA NCHINI NORWAY.






Uliwainua watanzania wakati ulipoipatia goli la kufutia machozi baada ya kufungwa na Brazil, ulijisikiaje?
Jabir: Siku ile nilijihisi kama shujaa mkubwa kwani kuwapa furaha mamilioni ya watu ni kitu cha pekee sana, namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hiyo iliyoandika rekodi ya nchi yetu katika medani ya soka nchini kwani kuifunga Brazil ni kitu adimu sana kutokea kwa nchi kama yetu.

Ulifunga bao katika mechi ya mwisho kwa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars Marcio Maximo,unaichukuliaje hali hiyo?
Jabir: Nalichukulia kama zawadi kubwa sana kwa Maximo, aliweza kutuongoza na kusaidia kuinua mpira wa Tanzania, hivyo bao hilo ni la shukrani yangu kwake kwa mema yote aliyoifanyia nchi yetu.
Pia bao hilo nali 'dedicate' kwa mke wangu, Jasmin Ismail Mkupete kwa msaada wake wa mawazo muda wote ninapokwama na kunipa ushauri pale ninapouhitaji. Vilevile natoa bao hilo kwa Watanzania wote wanaopenda maendeleo ya mpira wa miguu nchini.


Katika maisha yako ya kawaida familia yako ilikuchukuliaje pindi ulipoanza kuingia katika soka?
Jabir: Walikuwa wakali sana na walitaka nisome sana lakini kocha wangu Ramadhani Aluko wa DYOC, aliwaeleza kuwa mpira ni maisha, hivyo wakanikubalia hadi kuanza safari hizo nikiwa mdogo.


Wakati gani ulihuzunika sana katika mpira?
Jabir: Nilipoumia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2008/09 nilipokuwa na Simba SC tulipocheza na Toto African nilipata jeraha ambalo liliniweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Pia nakumbuka nilipotonesha jeraha langu katika mechi ya Simba na Yanga ya Kombe la Tusker mwaka jana.


Siku gani ulifurahi sana katika maisha yako ya soka?.
Jabir: Sitasahau siku nilipoipatia Simba bao pekee la ushindi dhidi ya Polisi Dodoma katika ligi ya msimu wa 2008/09, ushindi uliokuwa muhimu kwa timu yangu.


Kila binadamu ana matarajio yake, wewe unatarajia kufika hatua gani katika mpira?

Jabir: Natarajia kuwa mchezaji wa kimataifa, pia natarajia kuitumikia zaidi Taifa Stars.


Matarajio kwa familia?

Jabir: Kwa kweli natarajia kuwa na familia bora, kusaidia familia yangu na Mungu akinijalia kupata watoto nitawatunza vema.


Umecheza nje na ndani ya Tanzania umegundua kuna tofauti gani?
Jabir: Tanzania bado tupo nyuma kimpira kuliko nchi za Ulaya, tunahitaji muda na malengo mengi kufikia hatua ya kimataifa.

Nini mafanikio yako?
Jabir: Sijapata mafanikio makubwa sana lakini nimeweza kuendesha maisha yangu vizuri, na kufikia baadhi ya malengo yangu kifamilia. Upande wa mpira, kipaji changu kimeweza kukua kwa kiasi kikubwa tofauti na nilivyokuwa miaka iliyopita
.


Kila kitu kina faida na matatizo, je ni matatizo gani unakutana nayo katika soka?
Jabir: Tatizo kubwa ni upande wa matibabu kwa majeraha ya wachezaji mpira kwani tatizo la kupona miezi miwili linaweza kuchukua miezi sita hadi mwaka
.


Timu gani unaipenda kutoka bara la Ulaya?
Jabir: Naipenda Liverpool ya England na navutiwa na Steven Gerald wa timu hiyo.


Jabir Aziz alipoteza wazazi wake wote wawili akiwa bado mdogo na ilipofika mwaka 2000 bibi yake aliyekuwa akimlea, naye alifariki hivyo akawa analelewa na kaka na dada zake.
Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto saba, wanaume watatu na wanawake wanne.
Amesajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa miaka mitatu kuanzia Juni mwaka huu, ameoa mwezi uliopita na hajabahatika kupata mtoto.

KIKOSI CHA MASTAA WA BONGO WALIOCHEMSHA KABLA YA WAKATI…..

KATIKA kipindi cha miaka kumi iliyopita, nchi yetu (Tanzania) imebahatika kutoa wachezaji mahiri katika ukanda wetu
Mbarouk Suleiman Mbarouk
Wakati kizazi cha magolikipa mahiri kama, Mohammed Mwameja, Steven Nemes, Denis Edwin, Peter Manyika na Ismail Suma kikiishia, kulikuwa na makipa wengi vijana, Juma Kaseja, Mengi Matunda, Noel Pompi, Farook Ramadhani na wengineo, lakini kila mmoja alikuwa anaangalia ni hadi wapi vipaji vya makipa hao vingefika. Mbarouk Suleiman alikuwa ni mmoja ya makipa bora nchi kutokea Visiwani Zanzibar, lakini kutua kwake Yanga mapema mwaka 2006 ilikuwa ni sawa na kuupa kisogo mchezo wa soka akiwa na umri mdogo.

Said Sued
Kijana huyu wa Ilala alikuwa ni mchezaji mdogo zaidi katika ligi kuu ya Bara. Sued alijiunga na Simba mwaka 2001 akiwa kidato cha pili, na ndiyo kwanza alikuwa na umri wa miaka 17 kwa karibu alifuatiwa na Nico Nyagawa aliyekuwa Mtibwa Sugar wakati huo. Sued alikuwa anapanda kama mlinzi wa zamani wa Italia, Christian Pannucci, alikuwa mpigaji mzuri wa mipira iliyokufa kama Deniss Irwin, na mfungaji wa magoli ya mbali kwa staili ya Sergio Ramos. Matatizo ya mara kwa mara ya kinidhamu inasemekana ndiyo sababu kubwa ya Sued kutengwa na soka na kumuacha kinda mwezake wa mwaka 2001, Nyagawa akivaa beji ya unahodha wa Simba.

Twaha Abubakar ‘Abdul Mtiro’
Itikadi ya Usimba na Uyanga imemaliza kipaji cha Mtiro. Inasemekana kuwa mara baada ya kupaisha penati ya mwisho katika fainali ya ligi kuu ndogo mwaka 2007 mjini Morogoro, wakati timu yake ya Yanga ikicheza na mahasimu wao Simba, moja kwa moja aliwatumbukia ‘nyongo’ wana Yanga wote. Lakini ukiangalia kwa makini namna wanavyocheza ‘mafullback’ wa kushoto wa sasa wa Stars unaweza kuona kuwa Mtiro angeweza kuhodhi namba hiyo.

Boniface Pawassa
Kila alipokuwa anatema mate mshambuliaji mahiri wa zamani wa Misri, Hossam Hassan basi Pawassa alikuwa anayakanyaga, achana na stori kuwa Cannavaro anakaba sana, kwa Pawassa hakika usingeweza kumfikiria Cannavaro. Utovu wa nidhamu inasadikiwa ni sababu kubwa ya Pawassa kumaliza kipindi chake cha uchezaji akiwa na umri mdogo.


Hamis Yusuf.
Waziri wa ulinzi’ aliyehukumiwa na ubora wa Mamadou Niang. Ndiyo kabla ya Stars haijakwenda jijini Dakar kila mmoja alikuwa anafikiria ni nani na nani wangeanza katika kikosi cha kwanza (katika nafasi ya ulinzi wa kati), Victor Costa, Salum Sued na Yusuph wote walikuwa katika kiwango cha juu. Ilikuwa ni siku mbaya kwa Yusuph kwani hakuonekana kama ni kweli yeye ni ‘waziri wa ulinzi’ Sasa yupo AFC lakini ni sawa na kusema kuwa Yusuph ni moja ya vipaji vinavyotoweka kabla ya muda.


Waziri Mahadhi ‘Mendieta’
Katika umri wa miaka kati ya 28-30 aliyonayo sasa ni kichekesho kusema kuwa kiungo huyu mahiri wa zamani wa Stars ni kocha!! Mendieta kama alivyokuwa akitambulika kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na kufananishwa na kiungo wa zamani wa Hispania, Gaizka Mendieta. Inasemekana kuwa majeruhi ya mara kwa mara yamemaliza makali ya kiungo huyu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kujiweka kando na soka.

Shekhan Rashid Abdalah
Anavutia mabinti wengi kutokana na muonekano wake, upole wake lakini kikubwa ni namna anavyoupendezesha mchezo wa soka. Mara baada ya kutoroka katika klabu ya Simba mwaka 2003 na kwenda Norway, Shekhan aliporudi tena nchini mwaka mwaka 2004 hakuwa yule aliyepiga penati katika maji dhidi ya Ismailia ya Misri mwaka 2001. Mechi moja tu ilitosha kumuelezea kiungo huyu kuwa hana jipya tena, ni wakati Simba ilipocheza na Zanaco ya Zambia mwaka 2004. Alijitahidi kurejea katika kiwango chake lakini alivunjika mguu mwaka 2007, inasemekana kwa sasa yuko nchi Sweden.





Christopher Alex Massawe
Kama ilivyo kwa Shekhan, Alex pia alikuwa na mvuto kwa kina dada waliokuwa wakienda kutazama mechi za Simba au Stars.Alikuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza kama mlinzi au kiungo mshambuliaji. Kisa cha Mchaga huyu kuachana na soka akiwa na miaka chini ya 28, inasemekana kuwa alipata mwanamke wa kizungu ambaye hakutaka acheze soka, ndiyo maana alikuwa anafanya vituko vingi katika siku zake za mwisho akiwa na Simba.

Abuu Ramadhani ‘Amokachi’
Mshambuliaji Mfungaji wa zamani wa Yanga, Abuu alikuwa ni mmoja wa washambuliaji wenye rekodi nzuri ya ufungaji katika Tanzania. Sijui alikutwa na nini na kutibuana na viongozi wa zamani wa klabu yake ya Yanga. Kasi, uwezo wa kupiga mashuti ni baadhi ya sifa za mshambuliaji huyu wa zamani wa Stars. Wapo wanaosema kuwa majeruhi yamepoteza makali ya kijana huyu.

Aaron Nyanda
Namna anavyocheza Nurdin Bakari kwa sasa ndivyo alivyokuwa anacheza Nyanda. Ni kiraka aliyekuwa na uwezo wa kucheza mahali popote uwanjani, lakini daima alikuwa anavutia akicheza namba 10 au 11, kwani ungeweza kuona vionjo ambavyo si rahisi kuviona kwa Nurdin Bakari. Inasemekana majeruhi na masomo yalimfanya kuachana na soka la ushindani akiwa na umri mdogo.

golikipa azichapa na shabiki uwanjani..

Wednesday, December 21, 2011

Debate: LIGI GANI BORA ULIMWENGUNI: EPL au La Liga?





Tangu msimu wa 1992-93 nimekuwa nikiifatilia ligi kuu ya England lakini kwa mtazamo wangu nadhani LA LIGA ndio ligi bora Ulimwenguni. Je wewe unasemaje ?

Monday, December 19, 2011

RASHIDI MATUMLA VS MANENO OSWARD WAPIMA AFYA ZAO NA KUKUTWA WAOPO FITI KUZIOPIGA DESEMBA 25




MABONDIA Rashid Matumla ‘Snake Man’ na Maneno Osward ‘Mtambo wa Gongo’ wanatarajia kupanda ulingoni kuzichapa Desemba 25 mwaka huu katika pambano lisilo la ubingwa.
Pambano hilo linatarajia kuwa la raundi 10 uzito wa kati litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Heinken, Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam .

Siku kumi kabla ya mpambano mabondia Rashidi Matumla na Maneno Osward walishauliana kupima vipimo mbalimbali vikiwemo ukimwi na madawa ya kuongeza nguvu kama wanatumia na wameshapimwa na Daktali wa mchezo wa ngumi nchini chales kilaga, sheria za mchezo huo azirusu kutumia dawa za aina yoyote ya kuongeza nguvu
Hivyo mabondia wote wamekutwa wapo fiti na wanatarajia kuzipiga jumapili ya tarehe 25

Mkurugenzi wa Kampuni ya Adios Promotion, Shabani Adios 'mwayamwaya' ambaye ndiye muandaaji wa pambano hilo, alisema pambano hilo limeandaaliwa ili kumaliza ubishi baina ya mabondia hao ambapo katika pambano la mwisho Matumla alimchapa Oswald kwa pointi ambaye aliwalalamikia majaji kuwa hawakumtendea haki wakati walishawai kupigana mara mbili nyuma ambapo Matumla kamshinda Maneno Mara mbili na Maneno kashinda mara moja mpambano huo utakuwa wa kumaliza ubishi baina yao.

Utasindikizwa na mabondia mkongwe Rashidi Ally atazichapa na Kulwa Mbuchi, Selemani Jumanne na Ibrahimu Madeusi wakati Shabani Zunga atavaana na Mohamedi Kashinde, na bondia Sweet Kalulu na Saleh Mtalekwa


Katika Mchezo huo kutakua na DVD za mafunzo ya mchezo wa ngumi pamoja na kutambua sheria zake mbalimbali zitakazokua zikisambazwa na kocha wa mchezo huo Rajabu Mhamila 'Super D Boxing Coach' kwa ajili ya kuwapa mambondia mbalimbali mbinu za mchezo na mashabiki kujua sheria za masumbwi.

Super D alisema katika DVD hizo kutakuwa na mapambano mengi ambayo yanaweza kutumika kama mafunzo muhimu kwa mabondia ,makocha marefa pamoja na mashabiki wa mchezo kujua sheria mbalimbali.

'' Kuna mapambano kama ya akina Amir Khan, Manny Paquaio, Floyd Maywhether, David Haye, Mohamedi Ali pamoja na mtanzania Roja mtagwa anaefanya shughuli zake Marekani,

DVD hizo ni nzuri na hata walio tayari tayali katika mchezo huo wanatakiwa kujua sheria na mafunzo ya ngumi mana zinafundisha mambo mengi '' alisema Super D DVD hizo za mafunzo zinapatikana makutano ya barabara ya Uhuru na Msimbazi au katika kambi ya ngumi ILala na klabu ya AShanti nayo ya Ilala.

SANTOS 0:4 FC BARCELONA