Search This Blog

Thursday, December 22, 2011

JABIR AZIZ: Atoa bao lake la Brazil kwa Maximo na mkewe.

IKIWA imepita takribani miaka miwili tangu timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilipoandika rekodi ya kufungwa mabao 5-1 na Brazil, huku bao lake pekee likifungwa na chipukizi Jabir Aziz.
Nimepata nafasi ya kuzungumza na kiungo huyo anayeunda kikosi cha Taifa Stars tangu mwaka 2008 na kutueleza maisha yake akiwa ndani na nje ya uwanja.

Jabir mbali ya kuwa mwanasoka, ni mwanariadha mzuri na mtunza familia yake muda wote.


Kitu gani kilikufanya hadi ukaamua kuwa mcheza soka?
Jabir:Maisha yangu tangu utotoni yalinipelekea hadi nikaamua kucheza soka kwa sababu nilianza kutumia kipaji changu tangu nikiwa shuleni.


Ulianza kucheza mwaka gani?
Jabir: Niseme nilianza rasmi mwaka 2002 kipindi ambacho nilikuwa nacheza katika timu ya DYOC iliyopo Sigara, Chang'ombe mwaka huo huo tulichaguliwa kuunda timu ya Tanzania kwa vijana waliochini ya miaka 15 ambapo nilishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa ya ‘Gothia Cup’ kwa vijana iliyofanyika Denmark na Sweden.
Mwaka uliofuata tulichaguliwa tena kushiriki katika michuano hiyo ambayo kila tunaposhiriki huwa tunachukua ubingwa.




Mlikuwa na wachezaji gani?
Jabir: Kipindi hicho nilikuwa na miaka 14, nilicheza na wachezaji wengi sana baadhi yao ni Adam Kingwande (aliwahi kucheza Simba na sasa anaelezwa kuwa African Lyon), Ramadhan Chombo 'Redondo' wa Azam FC, Seif Mlanzi na Jabir Khalid Badra 'Dude'
.

Tuambie kuna wakati ilisemekana wewe na wenzako mliitoroka timu ya Taifa hiyo ya DYOC mlipokuwa Denmark, ilikuwaje?
Jabir: Umenikumbusha mbali sana, wakati tulipokwenda katika michuano ya vijana ya mwaka 2003 nikiwa kidato cha pili, tulishawishiwa tukacheze nchini Norway ambako soka lao lipo juu, na sisi kweli tukakubali, siku timu yetu ya DYOC ilipoondoka kutoka Denmark kwenda Sweden nasi tukatoroka kwenda Norway. Tulikuwa wachezaji watano, mimi, Chombo, Seif Mlanzi, Jabir Khalid na Godfrey Benedict.

Maisha ya Norway yalikuwaje?

Jabir: Tulipoondoka uongozi wa timu yetu ulianza kututafuta lakini hawakutupata, tulipofika Norway tulipata timu za ligi daraja la nne, mimi nilipata timu ya FK Vang na Chombo akapata timu ya Lindal.

Ilikuwaje tena ukawa mwanariadha?
Jabir: Unajua kipindi hicho tunatoroka nilikuwa mdogo kiasi ambacho sitakiwi kucheza katika ligi kutokana na kuwa mdogo, hivyo nikajiunga na timu ya riadha inayoitwa Renning Hill, nilikaa na timu hiyo tangu mwaka 2004-2006 nikiwa mchezaji na mkimbiaji riadha mbio ndefu.

Ikawaje hadi mkarudi nchini?
Jabir: Chombo cha serikali kipo kila mahali, wakati tupo kule tulikuwa tukifuatiliwa sana na serikali ya Tanzania, pia kuishi nchi za watu bila kibali ni tabu sana lakini kwa kuwa tulikuwa wachezaji haikutusumbua sana.
Baada ya serikali yetu kugundua sehemu tulipokuwa ikaamriwa turudishwe nchini mara moja, ndipo mimi na wenzangu tuliporejeshwa nchini Oktoba mwaka 2006.

Uliporejea nchini maisha yako ya mpira yalikuwaje?
Jabir: Baada ya kurejea nchini nilijiunga na timu yangu ya mtaani ya Friends Rangers ambayo baada ya muda mchache nikasajiliwa na klabu ya Ashanti United ya Ilala katika dirisha dogo la usajili wakati ilipokuwa ikicheza ligi kuu, lakini timu hiyo ilishuka msimu uliofuata wa 2007/08
.

Baada ya hapo?
Jabir: Nikiwa na Ashanti United kiwango changu kilikuwa kizuri, nikapata nafasi ya kujiunga na Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili, kipindi hicho nilikuwa na wenzangu Juma Jabu na Adam Kingwande.

Ilikuwaje ukatoka Simba na kwenda Azam FC?
Jabir: Nilihamia Azam FC baada ya kumaliza mkataba wa miaka miwili na Simba, hivyo Azam FC wakaonesha nia ya kunihitaji na kwa kuwa mkataba ulikuwa umeshaisha nikaamua kujiunga na Azam FC.


Hii itakuwa timu yako ya tatu katika ligi kuu, ni tofauti gani unaiona kutoka timu zote?
Jabir: Maisha ya mpira yanafanana kwa kiasi fulani, lakini kuna vitu vichache ambavyo vipo tofauti kidogo.


Nafasi yako katika timu ya Taifa ikoje?
Jabir: Nilianza kuitwa katika timu ya Taifa nikiwa nacheza na Ashanti United, na nilipoenda Simba nashukuru nilipata nafasi hiyo tena.



Kitu gani unadhani kilipelekea wewe kutopata nafasi ya kucheza mechi nyingi za timu ya Taifa?
Jabir: Unajua kipindi naingia Taifa Stars kulikuwa na wachezaji wakongwe na sisi chipukizi, hivyo nafasi yetu ilikuwa kupata uzoefu na timu ya Taifa, hivyo tulikuwa tukipewa nafasi chache hasa katika mechi za kimichuano.
Nakumbuka nikiwa na Taifa Stars nimecheza mechi kadhaa ikiwemo Kombe la Africa Mashariki na Kati (Challenge Cup) na mechi dhidi ya Mauritius katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2010.


Wewe ni maarufu sana kucheza ukitokea bench yaani 'Super Sub', unalizungumziaje hilo?
Jabir: Kutokea benchi ni utaratibu wa kocha, huwa anachagua wachezaji wa kuunda kikosi cha kwanza na sisi tunakaa benchi, huwa naichukulia hiyo kama nafasi pia kwani kuna wengine hata benchi huwa hawakai wanaishia katika mazoezi tu.



JABIR AZIZ ( KUSHOTO ) ALIPOKUA NCHINI NORWAY.






Uliwainua watanzania wakati ulipoipatia goli la kufutia machozi baada ya kufungwa na Brazil, ulijisikiaje?
Jabir: Siku ile nilijihisi kama shujaa mkubwa kwani kuwapa furaha mamilioni ya watu ni kitu cha pekee sana, namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hiyo iliyoandika rekodi ya nchi yetu katika medani ya soka nchini kwani kuifunga Brazil ni kitu adimu sana kutokea kwa nchi kama yetu.

Ulifunga bao katika mechi ya mwisho kwa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars Marcio Maximo,unaichukuliaje hali hiyo?
Jabir: Nalichukulia kama zawadi kubwa sana kwa Maximo, aliweza kutuongoza na kusaidia kuinua mpira wa Tanzania, hivyo bao hilo ni la shukrani yangu kwake kwa mema yote aliyoifanyia nchi yetu.
Pia bao hilo nali 'dedicate' kwa mke wangu, Jasmin Ismail Mkupete kwa msaada wake wa mawazo muda wote ninapokwama na kunipa ushauri pale ninapouhitaji. Vilevile natoa bao hilo kwa Watanzania wote wanaopenda maendeleo ya mpira wa miguu nchini.


Katika maisha yako ya kawaida familia yako ilikuchukuliaje pindi ulipoanza kuingia katika soka?
Jabir: Walikuwa wakali sana na walitaka nisome sana lakini kocha wangu Ramadhani Aluko wa DYOC, aliwaeleza kuwa mpira ni maisha, hivyo wakanikubalia hadi kuanza safari hizo nikiwa mdogo.


Wakati gani ulihuzunika sana katika mpira?
Jabir: Nilipoumia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2008/09 nilipokuwa na Simba SC tulipocheza na Toto African nilipata jeraha ambalo liliniweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Pia nakumbuka nilipotonesha jeraha langu katika mechi ya Simba na Yanga ya Kombe la Tusker mwaka jana.


Siku gani ulifurahi sana katika maisha yako ya soka?.
Jabir: Sitasahau siku nilipoipatia Simba bao pekee la ushindi dhidi ya Polisi Dodoma katika ligi ya msimu wa 2008/09, ushindi uliokuwa muhimu kwa timu yangu.


Kila binadamu ana matarajio yake, wewe unatarajia kufika hatua gani katika mpira?

Jabir: Natarajia kuwa mchezaji wa kimataifa, pia natarajia kuitumikia zaidi Taifa Stars.


Matarajio kwa familia?

Jabir: Kwa kweli natarajia kuwa na familia bora, kusaidia familia yangu na Mungu akinijalia kupata watoto nitawatunza vema.


Umecheza nje na ndani ya Tanzania umegundua kuna tofauti gani?
Jabir: Tanzania bado tupo nyuma kimpira kuliko nchi za Ulaya, tunahitaji muda na malengo mengi kufikia hatua ya kimataifa.

Nini mafanikio yako?
Jabir: Sijapata mafanikio makubwa sana lakini nimeweza kuendesha maisha yangu vizuri, na kufikia baadhi ya malengo yangu kifamilia. Upande wa mpira, kipaji changu kimeweza kukua kwa kiasi kikubwa tofauti na nilivyokuwa miaka iliyopita
.


Kila kitu kina faida na matatizo, je ni matatizo gani unakutana nayo katika soka?
Jabir: Tatizo kubwa ni upande wa matibabu kwa majeraha ya wachezaji mpira kwani tatizo la kupona miezi miwili linaweza kuchukua miezi sita hadi mwaka
.


Timu gani unaipenda kutoka bara la Ulaya?
Jabir: Naipenda Liverpool ya England na navutiwa na Steven Gerald wa timu hiyo.


Jabir Aziz alipoteza wazazi wake wote wawili akiwa bado mdogo na ilipofika mwaka 2000 bibi yake aliyekuwa akimlea, naye alifariki hivyo akawa analelewa na kaka na dada zake.
Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto saba, wanaume watatu na wanawake wanne.
Amesajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa miaka mitatu kuanzia Juni mwaka huu, ameoa mwezi uliopita na hajabahatika kupata mtoto.

No comments:

Post a Comment