KAMATI YA MAADILI TFF YATANGAZA UAMUZI
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza hukumu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake kwa kumsafisha mlalamikiwa mmoja, kutowaadhibu zaidi washtakiwa sita na kuahirisha kusikiliza shauri moja baada ya mlalamikiwa kutokuwepo.
Riziki Juma Majala, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ndiye pekee aliyesafishwa na Kamati ya Maadili dhidi ya mashtaka ya kutoa kauli zilizosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya TFF.
Vilevile Kamati imesita kuwachukulia hatua Shafii Dauda, Nazarius Kilungeja, Wilfred Kidao, Omar Isaak Abdulkadir na Kamwanga Tambwe kutokana na kuridhika kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi, hivyo hawawezi kuadhibiwa mara mbili.
Pia imesema haiwezi kumuadhibu Richard Julius Rukambura, aliyeshtakiwa kwa kukiuka Katiba ya TFF kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, baada ya kubaini kuwa si mwanafamilia wa TFF kutokana na kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Hoja hiyo pia ilitumika kutomchukulia hatua Dauda na mwamuzi wa zamani Omar Abdulkadir kwa hoja kuwa walipoteza sifa za kuwa wanafamilia wa TFF baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi.
Shauri la Omary Mussa Mkwaruro la tuhuma za kutumia cheti cha elimu kisichotambuliwa na mamlaka husika, limeahirishwa kutokana na Mlalamikiwa kutowasilisha utetezi wake, hivyo Kamati imeagiza Sekretarieti kuwasiliana naye ili awasilishe maelezo yake.
Watu hao walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF na baada ya usaili walibainika kuwa na matatizo ya kimaadili, hivyo ili iamue juu ya hadhi yao katika familia ya mpira wa miguu kwa kuwachukulia hatua au kuwaweka huru.
Katika hukumu iliyotolewa leo (Septemba 26 mwaka huu), Kamati ya Maadili imeeleza kuwa Majala hakiuka Kanuni za Maadili kwa kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na TFF vinaonyesha kuwa klabu ya Kiluvya United imesajiliwa na Serikali na vyama wanachama wa TFF.
Kuhusu Rukambura, ambaye alilalamikiwa kwa kuipeleka TFF kwenye mahakama ya kiraia, hivyo kukiuka Kanuni ya 73 (3) (b) ya Kanuni za Maadili, Kamati imesema ushahidi uliowasilishwa na TFF hauonyeshi kama mgombea ni mwanafamilia wa TFF; alishaondolewa katika uchaguzi na hivyo si kati ya wagombea na hivyo mikono ya Kamati kufungwa kwa mujibu wa kanuni ya pili ya Kanuni za Maadili.
Kamati pia imeeleza kuwa Kanuni ya 73 (3) ambayo ingepaswa kutumika kumchukulia hatua, chimbuko lake ni Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF ambayo inawalenga wanachama tu na hivyo kuamua kuwa malalamiko hayo hayana mashiko na kwani Rukambura alishapoteza sifa za kuwa mwanafamilia na hivyo kushindwa kumchukulia hatua.
Kidao alishtakiwa kwa kosa la kumiliki nyaraka za Kamati ya Utendaji kinyume na taratibu na pia kuwasilisha malalamiko yake Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) bila ya kufuata taratibu, lakini Kamati imesema kwa vile mlalamikiwa ameenguliwa kwenye uchaguzi, anatumikia adhabu ya kinidhamu na hivyo haiwezi kumuadhibu mara mbili.
Kuhusu Shafii Dauda, Kamati imesema malalamiko dhidi yake hayana mashiko kwa kuwa si mwanafamilia wa TFF na kwamba lalamiko dhidi yake linatupiliwa mbali kwa kuwa tayari ameshaondolewa kwenye uchaguzi kutokana na kosa la kinidhamu.
Kamati iliona hakukuwa na haja ya kushughulikia mashauri dhidi ya Nazarius Kilungeja, ambaye alishtakiwa kwa kukaidi maagizo ya vyombo halali vya TFF, na Kamwanga Tambwe kwa kuwa tayari wawili hao wanatumikia adhabu ya kufungiwa na Kamati ya Nidhamu.
Hizi kamati za TFF hazifai maana kuenguliwa ni adhabu? na kama ni adhabu inaisha lini? je uchaguzi mwingine wataruhusiwa kugombea au ndio mwisho wao kwenye uongozi wa soka? Haya ndio Richard Wambura alikuwa analalamikiwa maamuzi ya kutoonesha ukomo wa adhabu. Wao walitakiwa watoe ukomo wa adhabu ili ieleweke. Na je kama hawa watu si wanafamilia wa TFF inamaana uchaguzi mwingine ukitokea watagombea kama wanafamilia huru? Huu ubabaishaji mwingine.
ReplyDeleteNakumbuka ile kamati ya uchaguzi ilitangaza kuwa wamewaengua kwa sababu ya kila mmoja na yake, na kuwapeleka kwenye kamati ya maadili kwa ajili ya kuwaadhibu sababu wao hawana mamlaka ya kuadhibu, sidhani kama kamati ingepeleka ili ikaengue maamuzi yake yenyewe. Ingekuwa ni rufaa imekatwa na walioenguliwa na kuwakuta hawana hatia ingekuwa masuala mengine. kwa hili kamati iko sawa sababu wao wanadili na TFF na organ zake kutoa adhabu, sasa kama mtu sio familia hiyo kamati haina mamlaka kutoa adhabu. Sijajua taratibu vizuri hapa ina maana hakuna muda wa rufaa ili wakakate rufaa huko? au muda umeisha? Kwa hili kamati hii imefanya kazi yake kwa ufasaha ili wengine waendelee maamuzi mengine. usijali bw. Shaffii endelea kutetea ambition yako ipo siku utakuja kutuongoza
ReplyDeleteTatizo tunateua wanasheria ambao hawajui uendeshaji wa soka kama walivyofanya kwenye issue ya Ngassa kutuambia hawawezi kuiadhibu Simba kwakuwa hawana mamlaka halafu haijulikani nani mwenye mamlaka, wenye mamlaka wanakwepa {kamati ya katiba, sheria na hadhi .za wachezaji}.
ReplyDeleteKamati ni ya maadili , watu wanatuhumiwa kukosa maadili na kuzuiwa kugombea na wanapelekwa huko kwa hatua zaidi wao wanakwepa kuamua. Kutuambia wamesha adhibiwa inamaana jamaa kweli wanamakosa ila kwakuwa wamesha adhibiwa basi hatuwezi kuwaadhibu tena , kwahiyo mchezo sasa utakuwa wakigombea wanaenguliwa na kamati ya uchaguzi basi mchezo unaishia hapo. Hii kamati iliundwa ili kutuondoa hapo, sasa inavyoonekana haiwezi , hawa watu wanajua kuendesha kesi za kisutu (beyond reasonable doubts) siyo TFF (SOKA ), huku tunahitaji wanasheria ambao wanajua kuendesha soka. Ushahidi wa mazingira tu unakufunga, Mgambo haiwezi kuifunga Coastal Union 15-0 tukaiacha ligi kuu, hawa wanasheria tunao waingiza kwenye soka wanajua haya ?
ili tupate mafanikio katika soka letu la bongo lazima tufanye mapinduzi na mapinduzi pekee ni kuwaondoa watu wote walio zidi miaka 45 kwenye ngazi zote za uongozi tuache makocha tu.vinginevyo wazee wameshaona kuenda kwenye vyama vya soka ndio sehemu pekee ya kustafia
ReplyDeletelazima kieleweke la sivyo tutaendelea kushuhudia vipigo ndani nje kuanzia vilabu mpaka timu ya taifa