KATI
ya timu tatu mpya katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu wa 2013/ 14, Mbeya City
ndiyo imeanza kwa moto mkali kuliko Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United
ya Dar es Salaam.
City
imekuwa gumzo nchi nzima na sababu yake ni moja tu, ilizitoa jasho Yanga katika
mechi yake mjini Mbeya na Simba katika mchezo wao Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Kocha Ernie Brandts wa Yanga hana hamu na Abdallah Kibaden ameivulia
kofia timu hiyo.
Katika
kipindi hiki ambapo Tukuyu Stars ‘imepotea’, Mecco imekufa na Prisons
ikichechemea, City ndiyo imewaunganisha wapenzi wa soka katika mkoa wa Mbeya.
City ikicheza katika dimba la Sokoine huunganisha hata pande hasimu za kisiasa
na kuishangilia timu hiyo ambayo ilinunuliwa na jiji la Mbeya kutoka kwa Rhino
ya Arusha.
Kimsimamo,
City iko nafasi ya nane ikiwa na pointi nane kutokana na mechi sita ilizocheza,
pointi moja nyuma ya Yanga iliyoko nafasi ya tano. Mbeya City imeshinda mechi
moja na imetoka sare tano, haijafungwa hata mechi moja.
City
ikishinda mechi ya keshokutwa dhidi ya Oljoro JKT na Yanga ikafanya vibaya
dhidi ya Mtibwa Sugar, inaweza hata kuchupa nafasi ya pili. Hata hivyo
itategemea matokeo ya mechi nyingine kati ya Kagera Sugar na JKT Ruvu.
City
iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1 na kutoka sare na Yanga (1-1), Simba (2-2),
Azam (1-1), Coastal (1-1) na Kagera (0-0). Kiuchezaji Mbeya City huonekana
wakipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
City namilikiwa
na kusimamiwa vizuri na Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Mashabiki wa Simba na
Yanga sasa ‘wamepungua’ jijini Mbeya na wote huishabikia na kuiunga mkono City
kutegemea inacheza na timu ipi. Iko huru haijajipambanua kuwa tawi la Yanga au
Simba, jambo linalosababisha klabu nyingi za mikoani kusambaratika.
Mmoja
wa wachezaji wa City, kiungo mshambuliaji Richard Peter anathibitisha kwa kusema
hawana ushabiki wala uhusiano na timu yoyote ya ligi kuu ndiyo maana wameweza
‘kuzibania’ timu zote walizokutana nazo.
“Hatuna
urafiki wala undugu na timu yoyote hata hizo Simba na Yanga hatuna urafiki nazo,
ndiyo maana tumeweza kuzibana na kutoka nazo sare. Hatuwezi kuwa tawi la Simba
au Yanga, sisi tunatazama zaidi katika ushindi na kufanya vizuri katika ligi na
si vinginevyo,” anasema Richard.
Jijini
Mbeya, kila unapokaribia mchezo wowote wa
City, jiji la Mbeya hupambwa kwa rangi ya zambarau ambazo ndizo
zinazotumiwa na timu hiyo na hata unapoingia uwanjani, mashabiki wa timu ni
wengi na wakati mwingine hufikia hatua ya kukaa sehemu zilizozoeleka kukaliwa
na mashabiki wa Simba au Yanga.
Idadi
ya mashabiki wanaojitokeza uwanjani kutazama mechi za City na ushahidi ni
mapato ya mlangoni. Mechi ya City na Yanga hivi karibuni iliingiza zaidi ya Sh.
93 milioni wakati Yanga na Prisons kilipatikana kiasi chini ya hicho. Hii ina maana
mvuto wa City ni mkubwa kuliko Prisons.
Nje ya
uwanja, Mbeya City ni timu yenye mashabiki wenye hamasa kubwa ya kuishangilia
na hata matajiri hujisikia raha kuichangia na kusafiri nayo kutoka Mbeya hadi
Dar es Salaam kuipa nguvu.
Ndani
ya uwanja, Mbeya City ni timu yenye nidhamu kubwa ya mchezo na hata kocha wake,
Juma Mwambusi anakiri kuwa wachezaji wake ni wasikivu na wenye hamasa ya hali
ya juu kutaka kuona timu yao inafanya vizuri.
“Tupo
kama kitu kimoja na tunasikilizana wakati wote, tumekaa pamoja kwa muda mrefu
na ndiyo maana leo hii tunafanya vizuri katika ligi. Hakuna kitu kingine cha
ziada ukiacha hilo na wananchi kuiona ni timu yao hivyo wanapaswa kuiunga mkono
wakati wote,” anasema Mwambusi aliyewahi kuinoa Prisons.
Wachezaji
wanaonekana wenye pumzi na wanaocheza kwa malengo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa
mchezo jambo ambalo Mwambusi anasema ni matokeo mazuri ya mazoezi ya kujiandaa kwa
msimu huu wa ligi.
City
inaonekana imejipanga zaidi ndani na nje ya uwanja, lakini inaweza kuingia
katika matatizo na kupoteza mwelekeo wake endapo itaingia katika mkumbo wa
kukubali kutumiwa na moja ya klabu za Simba na Yanga.
Hii timu haitachukua muda kabla haijaelekea zilipoelekea timu nyingine. Subiri usajili utaona
ReplyDeleteLigi inatimu 13 pinzani na mbeya city kwa nini uiombee au uilinganishe na yanga kama ikifungwa.
ReplyDelete