Ligi Kuu Tanzania Bara ipo mbioni kumalizika. Timu zote 14 zikiwa zimebakisha takribani michezo saba hadi minane kuhitimisha msimu wa 2012/13.
Kila mtu alitabiri mambo yake aliyoyajua mwenyewe na kutoa sababu zake binafsi kwa mtazamo wake kulingana na alivyoziona timu hizo zikishiriki ligi hiyo.
Lakini sasa huenda ukawa wakati muafaka kuangalia mwelekeo wa vikosi hivyo. Tayari timu zinazoweza kupata ubingwa mwishoni mwa msimu huu zimeanza kujiengua taratibu.
Ni wengi ambao wanaweza kuishangaa Yanga kushika usukani wa ligi.
Pia, huenda ni watu wachache sana wanaoweza kushtuka kikosi hicho kikitwaa ubingwa msimu huu.
Awali, Simba ilionyesha kiwango na kukalia kiti cha uongozi wa ligi kwa muda mrefu, sasa ipo nafasi ya tatu, nyuma kwa pointi 11 na vinara Yanga yenye pointi 42 kibindoni.
Mbio za ubingwa MBIO za kusaka taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012/13 zimeanza kuonekana wazi wakati pointi sita zikiwatofautisha Yanga na Azam FC ambazo zina nafasi pana ya kubeba taji hilo msimu huu.
Azam imetulia nafasi ya pili na pointi zake 36 na kuweka 'gap' la pointi sita na vinara Yanga yenye pointi 42 kibindoni.
Bingwa mtetezi, Simba imeketi nafasi ya tatu na pointi zake 31, tofauti ya pointi 11 na mtani, Yanga. Hiyo inaonyesha kuwa wateule wameanza kujitenga taratibu.
Vibonde wajulikana KAMA ambavyo huwezi kushtuka Yanga ikichukua ubingwa. Pia, huwezi kushangaa kuona Polisi Moro, Toto African na African Lyon zikishuka daraja.
Kuna 'gap' la tofauti ya pointi kama 29 kati ya vinara Yanga na timu ya African Lyon inayoburuza mkia. Lyon ina pointi 13 wakati Yanga inayoongoza ligi ina pointi 42.
Pia, Toto inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani ina pointi 14.
Klabu hizo tatu zinatakiwa kupigana kufa na kupona kuhakikisha zinashinda mechi zote zilizobaki kujinasua kwenye eneo hilo hatari. La! sivyo zitakwenda na maji.
Hata hivyo, timu tatu zinazomilikiwa na majeshi, JKT Ruvu, Tanzania Prisons na JKT Oljoro zinatakiwa kujiweka sawa kulingana nafasi zilizopo.
Timu zilizotisha kuna timu ambazo zimekuwa tishio la vigogo msimu huu. Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimeweza kuzifunga Yanga na Simba kwa wakati tofauti.
Kwa hali inavyoonyesha zinaweza kufanya vizuri katika mechi zilizobaki na kushika nafasi tatu za juu.
Pia, Coastal Union imeonyesha kuja kivingine na kuwa kizingiti kikubwa kwa vigogo hasa ikiwa kwenye viwanja wake wa nyumbani Mkwakwani, Tanga.
Nayo Ruvu Shooting inatakiwa kupigiwa 'saluti' kwa kiwango ilichokionyesha kwa mzunguko wa pili wa ligi.
Ndiyo maana ipo nafasi ya saba na pointi 26 huku ikiwa imesaliwa na mechi tisa mkononi.
Ufungaji bora NYOTA wawili, Kipre Tchetche wa Azam FC na Didier Kavumbagu wa Yanga wanawania ufungaji bora.
'Mapro' hao wanatofautiana kwa bao moja tu la kufunga.
Tchetche raia wa Ivory Coast amefunga mabao 10 wakati Mrundi Kavumbagu amepachika tisa na kuzifanya timu hizo kushika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi.
Ingawa washambuliaji, Jerry Tegete wa Yanga, Paulo Nonga wa Oljoro JKT na kiungo Amri Kiemba wa Simba wana kila sababu kuendelea kufunga hata kuwapiku endapo watalewa sifa na kushindwa kuendeleza kasi yao kuzitikisa nyavu za timu pinzani.
Kuna kila hali mfungaji bora msimu huu akamaliza akiwa na mabao 20 na kuvunja rekodi ya straika John Bocco wa Azam FC aliyepachika mabao 19 msimu uliopita.
Timu vinara ufungaji YANGA inaongoza kwa kila kitu. Ikiwa kwa pointi na pia mabao yakufunga.
Shukrani ziwafikie Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na mabeki Mbuyu Twite na Nadir Haroub 'Cannavaro'
Yanga imejikusanyia mabao 35 yakufunga ikiwa ni wastani wa mabao mawili katika kila mechi. Pia, ni timu ambayo imefungwa mabao machache. Imeruhusu mabao 12 tu kugusa nyavu zake katika mechi 18.
Lakini African Lyon ndiyo timu iliyoonyesha udhaifu kwenye ngome yake. Lyon imefungwa mabao 31 katika mechi 19 iliyocheza kwenye ligi. Mabao yakufungwa TIMU mbili, African Lyon na JKT Ruvu ndizo zimeonyesha udhaifu kwenye safu ya ulinzi.
JKT Ruvu imeruhusu kufungwa mabao 27 katika mechi 18 iliyocheza. Ingawa ipo nafasi ya nne kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.
Lyon ipo nafasi ya 13, imefungwa mabao 31 huku yenyewe ikizamisha 13 tu katika mechi 19.
Hat trick HAKUNA mchezaji aliyebahatika kufunga mabao matatu mchezoni, kwa lugha ya kimichezo 'hat trick'.
Mshambuliaji Juma Semsue wa Polisi Dodoma ndiye aliyefunga hat trick msimu uliopita.
Lakini mpaka ligi inaelekea kufika tamati msimu huu hakuna mchezaji aliyeweza kuvunja rekodi hiyo.
Askari huyo alifunga mabao hayo kwenye pambano dhidi ya Moro United mwaka jana wakati timu hizo zikishiriki Ligi Kuu
kabla yakwenda na maji.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, ulimalizika kwa Polisi Dodoma kuibuka na ushindi wa mabao 5-2.
Walioboronga TIMU tatu za Polisi Moro, Toto African na African Lyon ni timu ambazo zimeshinda michezo mitatu tangu kuanza kwa ligi.
Polisi inayonolewa na kocha mpya Adolf Rishard ilimaliza mzunguko wa kwanza pasipo kupata ushindi wowote wakati huo ikinolewa na kocha John Simkoko aliyetupiwa virago.
|
Search This Blog
Friday, March 1, 2013
TATHIMINI YA LIGI KUU: VINARA WA MABAO, NGOME DHAIFU, WALIONG'ARA NA KUBORONGA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
umakini wa viongozi wa TFF na viongozi wa waamuzi unapaswa kuwa makini kwani katika michezo iliyobakia timu zinaweza kucheza mpira nje ya uwanja na kuwa na matokeo yaliyopangwa.
ReplyDelete