MAKOCHA wa kigeni wanaoajiriwa kuzinoa timu za
soka za taifa Tanzania – Taifa Stars, Kilimanjaro Stars, Ngorongoro Heroes na
Serengeti Boys – wana bahati.
Matokeo mabaya uwanjani huwa hayana athari
zozote katika mikataba yao. Hata baada ya timu zao kufungwa vibaya, huendelea
hadi mwisho na hata kuongezewa mpya.
Marcio Maximo wa Brazil aliletwa nchini na
serikali kwa mbwembwe mwaka 2006, akaingia mkataba wa kuinoa Taifa Stars kwa
miaka mitatu. Alipewa kazi ya kuipeleka Stars fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika (CAN) 2008 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa
ndani (CHAN) mwaka 2009.
Baada ya kufanikiwa kuipeleka Stars CHAN,
Maximo aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja ili aipeleke Stars fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika 2010 na Kombe la Dunia 2010. Hakufanikiwa.
Akaja Jan Poulsen wa Denmark akachukua dola
zake akaondoka Stars haikufuzu kokote. Jahazi akapewa ‘mdogo wake’ Kim Poulsen
ambaye alikuwa akizinoa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys, hajafanikiwa kwa
lolote na haelekei kabisa kujisukuma ajiuzulu labda asukumwe.
Matokeo mabaya chini ya makocha hawa Maximo,
Poulsen na Kim yalizindue Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka kipengele
katika mikataba ya makocha kwamba wasipopata matokeo mazuri waachie ngazi;
mkataba usitishwe.
Mfano, Chama cha Soka Malawi (FAM) kimeachana
na kocha mkuu Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji baada ya kushindwa kuipa timu ya
taifa, The Flames, tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014.
FAM iliingia mkataba wa muda wa miezi ya miwili
na kocha huyo na angeongezewa mkataba ikiwa kungekuwa na matokeo mazuri, lakini
baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Nigeria siku chache zilizopita
ziliifanya FAM kumtupia virago Mbelgiji huyo kwa kutoingia naye mkataba mpya.
Kocha wa Tunisia, Nabil Maaloul alitangaza
kujiuzulu nafasi yake wikiendi iliyopita baada ya timu yake kutolewa katika
harakati za kufuzu Kombe la Dunia 2014, kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka
kwa Cape Verde.
Matokeo hayo yaliyoiwezesha Cape Verde kufuzu
hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia, yalimkatisha tamaa Nabil huku akishindwa
kuamini kilichotokea katika mchezo dhidi ya taifa hilo changa kisoka.
Hata hivyo, Tunisia imerejeshwa kufuzu Kombe la
Dunia 2014 baada ya Cape Verde kubainika imemchezesha mchezaji asiyehalali
kinyume cha kanuni zinavyoelekeza. Hii ina maanisha, Tunisia imerejeshwa kwa
mlango wa uani.
Huko Libya, kocha wa timu hiyo Abul Hafidh
Erbeesh naye alibwaga manyanga baada ya kuona timu yake imefungwa bao 1-0 na
Cameroon na kukosa nafasi ya kusonga mbele. Japokuwa Libya haina historia kubwa
katika soka Afrika, mategemeo yao yalikuwa makubwa kama ilivyokuwa kwa
Tanzania.
Kwingineko duniani, kocha wa Czech, Michal
Bilek ameamua kujiuzulu nafasi yake baada ya kuona mambo hayaendi sawa katika
kikosi chake. Huyu anaonekana kutumia busara zaidi kuhusu nafasi yake na
anafahamu namna wananchi wanavyojisikia uchungu kwa nchi yao.
Bilek amejiuzulu baada ya timu yake kufungwa
mabao 2-1 na Italia hivyo kukosa nafasi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014.
JAMBO LA KUJIULIZA:
Malawi imeachana na Saintfiet, Nabil amejiuzulu
Tunisia, Erbeesh amebwaga manyanga Libya na Bilek ameamua kukaa kando Jamhuri
ya Czech wote kutokana na matokeo mabaya, kwa nini Tanzania inakaa na akina
Maximo, Poulsen na Kim hadi mwisho wa mikataba yao?
Baada ya Kim kushindwa kuipeleka Stars kwenye
michuano ya CHAN, fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia
amebakiza nini kwenye mikoba yake ya ukocha kitakachoisaidia Stars kuwa na
matumaini ya kucheza CAN mwaka 2015? Je,
bado anahitajika?
Makocha waliojiuzulu wameogopa aibu ya
kutimuliwa kama mikataba yao inavyosema wasipofikia malengo, lakini kwa
Tanzania makocha hawana hofu yoyote kwa vile mikataba yao haina kipengele cha
kulazimishwa kujiuzulu.
Wakati umefika TFF na mkurugenzi wa ufundi wa
TFF wawape makocha wa kigeni mikataba inayowawajibisha kwamba wasipofikia
malengo waondoke bila fidia, la sivyo watafukuzwa.
Ni aibu kuendelea kukaa na kocha ambaye
ameshindwa kuipeleka Stars hatua ya kupata ushiriki hata wa CHAN baada ya kutolewa na Uganda ambayo ligi
yake si bora kulinganisha na ile ya Tanzania Bara.
Wachezaji wengi Afrika Mashariki hupenda kuja
kucheza Ligi Kuu ya Bara kutokana na msisimko wa ligi hiyo na malipo mazuri.
Udhaifu unaoonekana sasa kwa Stars ni
uwajibikaji wa Kim na kurugenzi ya ufundi ya TFF. Hakuna anayeweza kumkemea Kim
wala kumwajibisha kama ilivyo kwa makocha wa mataifa mengine.
Kim Poulsen apime uzito wa kazi yake kama
makocha wa Libya, Czech na Tunisia asisubiri kutimuliwa kama Saintfiet
aliyewahi kubangaiza akiwa na klabu ya Yanga, Dar es Salaam.
Pia Shaff, watu wengi wanasahau nafasi ya kamati ya ufundi pia na mkufunzi wa ufundi wa TFF,.Hao watu wote wanatakiwa wabadilishwe.kwa maana wameshindwa kumpa ushauri mzuri kocha.Makocha wanafanya makosa yaleya, timu inashindwa kuwa na mafanikiokwa karibu miaka kumi, graph yake inashuka chini.
ReplyDelete