KATIBU
Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui amesema kitendo cha
wanamichezo wengi kutojiandaa na maisha baada ya kung’ara katika michezo ndicho
chanzo cha wanamichezo wengi kujiingiza katika biashara ya dawa za kulevya.
Hivi
karibuni wanamichezo Joseph Kaniki (mwanasoka) na Mkwanda Matumla (bondia)
walikamatwa wakituhumiwa kukutwa na dawa za kulevya nchini Ethiopia wakiwa
njiani kwenda Sweden.
Mpaka
sasa watuhumiwa hao wanasota katika mahabusu za nchi hiyo huku wakisikiliza
kesi yao ambayo inaweza kusikilizwa na kama wakitiwa hatiani wanaweza kufungwa
Ethiopia kwa kuwa nchi hiyo haina makubaliano ya kubadilishana wafungwa na
Tanzania.
Nyambui
aliuambia mtandao huu kwamba, wanamichezo wengi wanaingia katika michezo bila
kujiandaa na maisha ya uanamichezo na hata wanapopata fedha huwa hawawezi
kuziingiza katika mfumo wa kujizalisha.
“Wanamichezo
wengi hawana usimamizi wa mambo ya kiuchumi, tazama wanapata fedha nyingi
lakini wakitoka nje ya mchezo huo maisha yao yanakuwa magumu na yenye
kusikitisha ndipo hapo wanapoamua kujiingiza katika matumizi na biashara ya
dawa za kulevya.
“Kitu
kingine kinachowafanya wanamichezo kuingia katika biashara hii ni tamaa za
kutaka kutajirika bila kufuata taratibu husika. Haraka hii ya maisha ni tatizo
kwa vijana wetu na ndiyo maana kila kukicha wanakamatwa,” alisema Nyambui
ambaye wakati wake alikuwa mkimbiaji maarufu.
Kabla
ya Kaniki ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars kukamatwa na
dawa za kulevya huko Ethiopia, msanii wa filamu na ‘video queen’, Agnes Gerald
‘Masogange’ naye alikamatwa hivi karibuni huko Afrika Kusini akiwa na shehena
ya dawa za kulevya na raia mwingine wa Tanzania.
Wimbi
la biashara ya dawa za kulevya limeshamiri nchini Tanzania miongoni mwa
wanamichezo kutokana na urahisi wa safari zao kwenda nje ya nchi na hata sasa
wamekuwa wakifanyiwa upekuzi wa hali ya juu kila wanapotaka kuingia katika nchi
nyingine.
Tayari
serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza imeshaweka
mitambo maalum ya kung’amua madawa hayo katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Nyerere jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment