Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzana bara, Young Africans leo jioni wanatarajia kufanya mazoezi katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi , mjini Tabora kujiwinda na mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers.
Yanga waliwasili mjini Tabora jana usiku wakiwa na tafakuri nzito ya kutafuta pointi tatu muhimu ili kuwasogelea Azam fc waliopo kileleni katika msimamo wa ligi.
Mpaka sasa Yangaa wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 40 baada ya kucheza mechi 19, wakati Azam fc wameshajikusanyia pointi 44 kileleni kwa kushuka dimbani mara 20.
Timu hizi mbili zilitoka sare ya bao 1-1 jumatano ya wiki hii katika mchezo uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Hata hivyo, Azam fc walionekana kuwa bora zaidi kwani kwa dakika 20 za mwisho walicheza wakiwa pungufu kufuatia beki wake wa kulia, Erasto Edward Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwasababu ya kutoa lugha chafu kwa mwamuzi.
Azam fc hawajafungwa mechi hata moja msimu huu, na malengo yao ni kutwaa ubingwa.
Kocha wa Yanga, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm baada ya mechi ya jumatano alisema anajipanga kufanya vizuri mechi ya kesho na nyingine zote zilizosalia.
Kushinda kwa Yanga hapo kesho kutawafanya warudishe hadhi yao ya kutetea ubingwa msimu huu,
Wakati Yanga wakihitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri ya kutwaa taji, wenyeji wao, Rhino wanahangaika kukwepa mkasi wa kushuka daraja.
Kikosi hicho cha kocha Jumanne Chale mpaka sasa kinaburuza mkia kwa kujikusanyia pointi 13 kufuatia kushuka dimbani mara 21.
Rhino wamebakiza mechi 5 ambazo wanahitaji kushinda zote ili kurejesha matumaini, japokuwa inaonekana kuwa ndoto.
Kwa hesabu za haraka, maafande hawa wa JWTZ kama vile wameshashuka daraja, ingawa mpira wa miguu huwa hauendi kwa hesabu rahisi kiasi hiki.
Kama Rhino watashinda kesho na mechi nyingine zote zilizobaki, basi wanaweza kufikisha point 28 ambazo pengine zitaweza kuwaokoa.
Kushinda mechi zote itakuwa ngumu hasa kwa kuanzia na kipute cha kesho dhidi ya Yanga wenye uhitaji mkubwa wa Pointi kwasasa.
Mechi nyingine yenye msisimko hapo kesho ni baina ya JKT Ruvu dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mechi hii ni muhimu kwa timu zote kwani JKT Ruvu wapo katika harakati za kukwepa kushuka daraja.
Kwasasa kocha wake, Fredy Felix Minziro hana cha kupoteza zaidi ya kutafuta ushindi. Hivyo wataingia uwanjani kwa nguvu zote.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa Minziro kupata matokeo mazuri hapo kesho, kwasababu Mbeya City wanahitaji zaidi pointi ili kujikita katika nafasi za juu.
Mpaka sasa Mbeya City wapo nafasi ya tatu kwa pointi 39, hivyo wakishinda kesho watafikisha pointi 42.
Kupanda nafasi itategemeana na matokeo ya Tabora ambapo Yanga watakuwa na kibarua na Rhino.
Kama Yanga atashindwa kupata matokeo ya ushindi na Mbeya City atashinda, basi wanajangwani watazidi kujiweka mazingira hatari zaidi kwasababu wataporomoka kwa nafasi moja.
Ligi kuu itaendelea tena siku ya jumapili, ambapo uwanja wa Taifa, Simba SC watakuwa wenyeji wa Coastal Union .
Hiyo itakuwa mechi ngumu kwa timu zote kwasababu kocha wa Simba, Dravko Logarusic hahitaji kuona anapata matokeo mabaya kwa mara nyingine.
Loga ataingia akiwa na presha kubwa nyuma yake kutokana na ukweli kuwa Simba haijawa katika ubora wake wa siku za nyuma.
Mpaka sasa Mnyama yupo nafasi ya nne kwa pointi 36 kibindoni na ameshuka dimbani mara 21.
Nao Coastal Union hawataki kufungwa tena ukizingatia wikiendi iliyopita walifungwa mabao 4-0 na Azam fc uwanja wa Azam complex Chamazi.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam fc watakuwa nyumbani kwao Azam complex kuumana na JKT Oljoro.
Mechi hiyo ni muhimu kwa Oljoro kwani wapo hatarini kushuka daraja msimu huu, hivyo hawana cha kutafuta zaidi ya pointi tatu kwao.
Lakini utakuwa muhimu zaidi kwa Azam fc, kwani kushinda kwao kutawafanya kuwa katika mazingira mazuri ya kubeba ndoo ya ubingwa kwa mara ya kwanza.
Azam fc wakishinda watazidi kusogelea ubingwa, lakini wakishindwa kupata matokeo mazuri, Yanga wakashinda Tabora, basi watakuwa wamejitia hatiani.
Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ashanti United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment