Timu 15 zinazoshiriki michuano ya mwaka huu ya Kombe la Uhai zimepangwa katika makundi matatu ambapo mechi zitachezwa katika viwanja viwili; Uwanja wa Karume na Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Mbande.
Mashindano hayo yanashirikisha timu zenye umri chini ya miaka 20 za klabu zote 14 za Ligi Kuu ya Vodacom wakati timu mwalikwa mwaka huu ni timu ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys).
Mabingwa watetezi Ruvu Shooting Stars ndiyo wanaoongoza kundi A katika michuano hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia bidhaa yake ya maji Uhai. Timu nyingine katika kundi hilo ni Oljoro JKT, Kagera Sugar, Azam na Mtibwa Sugar.
Kundi B lina timu za JKT Ruvu Stars, Polisi Dodoma, Moro United, Yanga na Villa Squad wakati kundi C ni Simba, Coastal Union, Toto Africans, African Lyon na Serengeti Boys. Mbali ya sh. milioni moja za maandalizi kwa kila timu, mdhamini pia anatoa zawadi kwa washindi watatu wa kwanza, mchezaji bora, mfungaji bora, timu yenye nidhamu na nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa timu kutoka mikoani.
Campaign Against Malaria yenyewe inatoa seti moja ya jezi kwa kila timu inayoshiriki mashindano hayo ambayo yataanza Novemba 12 na kumalizika Decemba 13 mwaka huu.
Kila siku kutakuwa na mechi tatu katika kila uwanja. Siku ya ufunguzi Toto Africans itacheza na Serengeti Boys saa 3 asubuhi Uwanja wa Karume, Ruvu Shooting Stars vs Oljoro JKT (saa 8 mchana- Karume) na Kagera Sugar vs Azam (saa 10 jioni- Karume).
Simba vs Coastal Union (saa 3 asubuhi- Chamazi), JKT Ruvu Stars vs Polisi Dodoma (saa 8 mchana- Chamazi) na Moro United vs Yanga (saa 10 jioni- Chamazi).
No comments:
Post a Comment