Search This Blog

Friday, October 19, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




ELECTIONS COMMITTEE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAAMUZI KUHUSU  RUFAA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MBEYA (MREFA), MKOA WA SHINYANGA (SHIREFA) NA MKOA WA DAR ES SALAAA (DRFA).

19 OKTOBA 2012


1.                   Kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF, Ibara  ya  10(6), 12(1) na 26(2) na (3), Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika vikao vyake vilivyofanyika tarehe 12 na 18 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Mbeya (MREFA), Shinyanga (SHIREFA) na  Dar es Salaam (DRFA) na  kutoa maamuzi kama ifuatavyo:

(a)                 Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)

(i)                  Rufaa ya Ndg. Charles Makwaza: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Charles Makwaza dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kumpitisha Ndg. John Mwamwaja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwamba hakutekeleza wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu wa MREFA kwa muda wa miaka 3.

Baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa vielelezo na maelezo ya Ndg. Charles Makwaza yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kwa kiwango kikubwa hayakuwa ya kweli. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.

(ii)                Rufaa ya Ndg. Lusekelo E. Mwanjala: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Lusekelo E. Mwanjala ikipinga  maamuzi ya  Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea  nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu wa uongozi wa mpira wa Miguu.

Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Mwanjala anakidhi kigezo cha uzoefu. Kamati inakubaliana na rufaa ya mrufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA na hivyo imemrejesha Ndg. Mwanjala kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA. 


(iii)              Rufaa ya Ndg. Thadeo T. Kalua: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa  mbele yake na Ndg. Kalua ikipinga  maamuzi ya  Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea  nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa hii na kubaini kuwa Katiba ya MREFA iliyosajiliwa haina sharti hilo kwa waombaji uongozi.  Kamati inakubaliana na maombi ya


(iv)               mrufaa na inamrejesha Ndg. Thadeo Kalua kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. 

(v)                 Uchaguzi wa MREFA utafanyika Jumamosi, tarehe 27 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.


(b)                Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).

(i)                   Rufaa ya Ndg. Ibrahim Magoma: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Magoma ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA, kwa kigezo cha kuingilia Mchakato wa Uchaguzi kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na pia kutozingatia matakwa ya Kanuni hizo katika kujaza fomu za maombi ya uongozi wa SHIREFA.

Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa ya Ndg. Magoma na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Magoma  aliingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF akiwa Katibu Mkuu wa SHIREFA kwa kushiriki kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA iliyokuwa ikendelea na mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA.  Kamati inakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA wa kumwondoa Ndg. Magoma kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA.  Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.

(ii)                 Uchaguzi wa SHIREFA umesogezwa Mbele kwa siku nne. Uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012, mjini Shinyanga.


(c)                 Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili Mchakato wa Uchaguzi wa DRFA na rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA  na kuamua kama ifuatavyo:

(i)                   Marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA: Hoja ya rufaa iliwasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura ilikihoji uhalali wa marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA, kwamba usajili wa Katiba ya DRFA si halali. Kamati ilibaini kuwa marekebisho ya Katiba hiyo yalifanyika kwa kufuata maagizo ya TFF na kwamba DRFA ilizingatia maagizo hayo. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliridhika kuwa Katiba ya DRFA imesajiliwa na Msajili wa vyama na vilabu vya michezo baada ya kuridhiwa na TFF, na hivyo, Kamati iliitupa hoja hiyo ya Mrufani kuhusu uhalali na usajili wa Katiba ya DRFA.

(ii)                 Kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF : Hoja ya rufaa ya Ndg. Michael R. Wambura iliomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa tamko kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA imeundwa bila kufuata Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 3(2). Kamati iliridhika kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliteuliwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF hususan, Ibara ya 3(2), hivyo uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo haukukiuka Kanuni za Uchaguzi. Kamati iliitupa rufaa hiyo.

(iii)                Wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA: Hoja za rufaa za Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir ziliomba kuyaondoa majina ya Ndg. Abeid Mziba, Ndg. Salehe Ndonga, Peter Muhinzi na Ndg. Daudi Kanuti katika orodha ya wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA na uongozi wa wanachama wa DRFA, kwamba hawana sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba za wanachama wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikupata vielelezo kuhusu hoja iliyowasisilishwa mbele ya Kamati na hivyo kuitupa hoja hiyo ya mrufani.

(iv)               Rufaa dhidi ya Ndg. Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA.  Rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kumpitisha Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA iliyowasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir iliomba jina la Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) liondolewe katika orodha ya wagombea uongozi wa DRFA kwa nafasi ya Mwenyekiti, kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2) inayotamka kwamba ‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya Warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na Ndg. Amin Mohamed Salim na ilijiridhisha kuwa Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo hakidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara 29(2). Kwa kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inakubaliana na maombi ya Warufaa.

(v)                 Rufaa kupinga kuenguliwa kugombea Uongozi DRFA:  Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir waliwasilisha rufaa  wakiomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutengua uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kuwaengua kugombea uongozi kwa madai ya kugushi sahihi ya Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA). Katika vielelezo mbalimbali vilivyoletwa mbele ya Kamati na baada ya kuwahoji warufani, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Katibu wa KIFA, Ndg. Seif Ally Mailo aliyeshuhudia maelezo ya fomu za waombaji uongozi DRFA na baadhi ya waombaji uongozi ambao kupitishwa kwao na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kulilalamikiwa, Kamati ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na pia ama KIFA au wagombea wenyewe. Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kwamba:

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Ndg. Gungurugwa Tambaza, Ndg. Mohammed Bhinda, Ndg. Benny Kisaka na Ndg. Hamisi Ayoub Mpapai bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).

·         Hoja ya kughushi saini ya Katibu wa KIFA katika kushuhudia maelezo ya  baadhi ya wombaji uongozi, ambayo  ilitumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kuwaondoa kugombea uongozi waombaji uongozi watano (5)  Ndg. Hamis Ambar, Ndg. Hamisi Kisiwa, Ndg. Andrew Tupa, Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir  haikutumika kuwaondoa baadhi wagombea ingawa fomu za waombaji uongozi saba zilisainiwa na Ndg.  Ndg. Seif Ally Mailo.

·         Ndg. Seif Ally Mailo ambaye si mwajiriwa na si kiongozi wa KIFA hakuwa na mamlaka ya kushuhudia maelezo ya wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.

·         Kulikuwa na hali ya kumficha Ndg. Seif Ally Mailo aliyesaini fomu za wagombea walioenguliwa kwa kigezo cha kughushi saini asifike kwenye kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa maelezo kuhusu ushiriki wake katika mchakato wa uchaguzi wa DRFA.

·         Fomu za wagombea Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda zilizojadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo kupitishwa na Kamati hiyo zilichezewa (tempered-with) kwa kunyofolewa baadhi ya kurasa na kuwekwa kurasa zenye maelezo na saini ambazo si za Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda. Wagombea hao ambao walikuwa wamepetishwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kwa maelezo kwamba fomu zao zilikuwa zimeshudiwa kwa sahihi halali ya Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo



walikana kwa maandishi na kutoa vielelezo vilivyothibitisha kwamba fomu zao zilichezewa na maelezo yaliyo kwenye kurasa zilizobadilishwa siyo wao walioyandika na kusaini.

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwaondoa baadhi ya waombaji uongozi kwa maelezo kwamba maelezo kwenye fomu za wagombea hao hayakushuhudiwa na viongozi vyama wanachama wa DRFA wenye mamlaka ya kushuhudia maelezo ya waombaji uongozi lakini bila kuzingatia matakwa hayo ya kikanuni ikawapitisha kugombea Ndg. Muhsin S. Balhabou na Ndg. Benny Kisaka ambao maelezo ya kwenye fomu zao hayakushuhudiwa na kiongozi wa chama mwanachama yeyote wa DRFA.

·         Kamati ya Uchaguzi ya DRFA inahusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa Kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya Katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara  ya  10(6), 12(1) na 26(2) na (3):

(i)                   Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. DRFA inaagizwa kuteuwa Kamati mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya DRFA ufanyike kabla ya tarehe 25 Oktoba 2012

(ii)                 Imefuta mchakato wa Uchaguzi wa DRFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya tarehe 29 Oktoba 2012 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Desemba 2012. Wagombea wote waliokuwa wamelipia Fomu za maombi ya uongozi (Fomu Na. 1) wanaokidhi sifa za kugombea uongozi kwa mujibu wa Katiba ya DRFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wajaze upya Fomu Na.1 bila kutozwa ada kwa nafasi zinazoendana na zile walizokuwa wameomba kugombea.




Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI TFF















BREAKING NEWS! AMINI BAKHRESSA APIGWA CHINI,KAMATI YA NDOLANGA YAVUNJWA

Hatimaye gwiji la chama cha soka mkoa wa Dar Es Salaam, Bwana Amini Bakhressa ameondolewa kuendelea kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa DRFA baada ya kushindwa kukidhi vigezo.
pia kamati ya uchaguzi ya DRFA chini ya mwenyekiti Alhaj Muhidini Ndolanga imevunjwa kutokana na kushindwa kuusimamia mchakato wa uchaguzi wa DRFA.

Habari zaidi zitafuata!!!!

NEYMAR ATIMIZA MECHI YA 200 NA SANTOS NA GOLI LA HATARI DHIDI YA TIMU YA RONADINHO

Usiku wa juzi nchini Brazili mchezaji Neymar alitimiza mechi ya 200 akiwa na Santos, na kwa bahati nzuri mechi ya 200 ikawa dhidi ya timu anayoichezea Ronaldinho Gaucho Atletico Mineiro. 

Katika kuipa heshima mechi hiyo Neymar akavaa jezi  maalum yenye namba 200 mgongoni kwa usiku huo.  

Huku Santos wakiwa tayari mbele kwa 1-0 kutokana na goli la Miralles alilofunga sekunde kadhaa baada ya mchezo kuanza, Neymar akaja kushindilia msumari kwenye jeneza katika dakika ya 10 ya mchezo kwa goli safi na la uwezo binafsi akiwapita mabeki kadhaa wa Atletico na kwenda kufunga bao kali, na kuifanya siku yake kuwa nzuri zaidi.
Hapa akimsalimia mkubwa wake Ronaldinho

CHEMSHA BONGO YA WIKI: TAJA JINA NA KAZI ANAYOIFANYA MWANAMICHEZO HUYU

TIP: NI KOCHA WA MOJA YA TIMU KUBWA DUNIANI.

UCHAMBUZI: LIGI KUU RAUNDI YA 8 - SIMBA NA AZAM KAMA MAN CITY NA CHELSEA ENGLAND



Na Baraka Mbolembole
Ligi kuu ya Tanzania Bara umeingia katika raundi ya nane jana kwa timu kumi kucheza michezo .  Simba ndiyo inaongoza ligi hiyo hadi sasa. Ifuatayo ni tathimini na uchambuzi wa timu tano ambazo zinateka hisia za wengi katika ligi ya msimu huu.
 MATARAJIO
SIMBA SC. Miaka miwili iliyopita chini ya kocha, Patrick Phiri walimaliza msimu pasipo kupoteza mchezo wowote, na sasa baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita, kocha wa timu hii, Milovan Curkovic anaamini kuwa timu kadhaa ni nzuri lakini anabaki na imani yake aliyojiwekea ya kutwaa taji bila kufungwa msimu huu, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar , Coastal Union na Kagera Sugar zinaonekana ni timu zinazotoa ushindani mkubwa katika ligi hiyo.
UDHAIFU WA SIMBA.
Bado timu imeweka imani kubwa kwa Emmanuel Okwi ambaye kimsingi ana mchango mkubwa ndani ya timu hiyo. Haruna Moshi amedai bado hajaridhishwa na mchango wa wacheji wapya wa kulipwa, Paschal Ochieng, Kommabil Keita na Danny Akkuffor. Simba wanacheza vizuri hadi sasa lakini bado timu haina safi imara na nzuri ya ulinzi, kwa mchezo wa juzi dhidi ya Kagera walionesha kutokuwa makini huku kipa namba moja Juma Kaseja akionesha kuchoka mwili. Wataenda kucheza na Mgambo JKT jumapili hii katika uwanja wa Mkwakwani ambap walitoka kuuulalamikia kuwa si mzuri wikiendi iliyopita. Wamepoteza kujiamini na tayari wamepata sare mbili mfululizo baada ya ushindi wa mechi tano za kwanza.


AZAM FC. NI KAMA CHELSEA

Kuna timu mbili ambazo hazijapoteza michezo katika raundi saba za ligi kuu ya Tz Bara na ligi kuu England, wakati Chelsea na Manchester City zikifanya hivyo, England, Simba na makamu bingwa mtetezi Azam FC hajizafungwa katika VPL. Azam ambayo imeruhusu mabao mawili tu ilishinda katika mikoa ya Kagera na Morogoro na ilipata sare jijini Mwanza iliweza kulinda rekodi yao ya kutofungwa jijini Mbeya dhidi ya Prisons kutokana na mchezo wao wa ushirikiano tena pasipo kuwa na mchezaji staa, wachezaji wote wapo katika levo inayofanana kimchezo na kiuwajibikaji. 

UDHAIFU Japo hawajapoteza mchezo wowote huku wakionekana kuimarika zaidi ya msimu uliopita, Azam bado hawaonekani ni wenye kujitolea asilimia ya uchezaji wao wakati wa mchezo, ni timu inayokata tamaa mapema. Imeshinda dhidi ya Kagera Sugar, Polisi Moro na kupata sare dhidi ya Toto Africa na Prisons, lakini wakati wanapokabiliwa na michezo migumu zaidi timu huonesha udhaifu wa 'team work' tatizo ambalo liliwanyima ubingwa msimu wa 2010/11 na kuwapatia, Yanga ambayo haikuwepo katika dalili za ubingwa hadi mechi ya tatu kabla ya ligi kumalizikana dhidi yao ( Azam FC) mechi ambayo, Jerry Tegete alifunga mara mbili huku aliyekuwa kipa namba moja Vladimir Niyonkuru akifukuzwa kwa madai ya hujuma. Baada ya sare ya jana dhidi ya Prisons Azam FC imebaki ni timu ‘isiyofungika’ pamoja na Simba hadi sasa.
UTABIRI.
Wanapigania kutwaa taji la kwanza la ligi katika msimu wake wa tano tangu kupanda daraja. Wamekuwa na bajeti nzuri ya msimu mzima na hata wachezaji si wa kulalamika matatizo kama wale wa timu nyingine, bado wana mtihani mkubwa wa kuwapiku KULWA na DOTTO katika mbinu mbalimbali za kutwaa taji. Kuwa na pesa pekee haitoshi ili kuwa juu ya Yanga na Simba na huu ndiyo mzigo uliowashinda, Moro United na hata Prisons katika miaka ya 2002 na 2008 miaka ambayo walitakiwa kuwa mabingwa wa haki kutokana na mchezo wao. Azam itamaliza ndani ya tatu bora na wakijipanga vizuri wanaweza safari hii wakatimiza ndoto yao ya kutwaa  taji.

SIMBA NA KAGERA SUGAR ZAINGIZA MILLIONI 58 - TIMU ZAGAWANA MILLIONI 22

Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar lililochezwa jana (Oktoba 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 limeingiza sh. 58,505,000.
 
Watazamaji 9,842 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 11,013,785.54 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,924,491.53.
 
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 440,000, mtathimini wa waamuzi sh. 254,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
 
Umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 3,183,890. Gharama za mchezo sh. 3,671,261.85, uwanja sh. 3,671,261.85, Kamati ya Ligi sh. 3,671,261.85, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,202,757.11 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,468,504.74.

 
TFF, FKF ZAANZISHA USHIRIKIANO MPYA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuinua kiwango cha mpira wa miguu katika nchi hizo.
 
Akizungumza baada ya mkutano uliowakutanisha vinara wa mashirikisho hayo Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema wameamua kurejesha uhusiano huo uliokuwepo zamani baada ya kuwepo utulivu katika uendeshaji mpira wa miguu nchini Kenya.
 
Amesema maeneo ya ushirikiano ambayo wameagiza yafanyiwe kazi na sekretarieti za pande zote (TFF na KFF) ili baadaye yaingizwe katika Hati ya Makubaliano (MoU) ni mafunzo, waamuzi, mechi za timu za Taifa za wakubwa, vijana na wanawake, na Ligi Kuu.
 
Rais Tenga pia amesema wameamua kuwepo ziara za mafunzo (study tours) katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Kenya wao Ligi Kuu yao iliingia katika mfumo wa kampuni mapema, hivyo itakuwa fursa nzuri kwa Bodi ya Ligi Kuu ambayo iko kwenye mchakato wa kuanzishwa kupata uzoefu kwa wenzao wa Kenya.
 
Naye Rais wa FKF, Sam Nyamweya aliyefuatana na Makamu wake wa Rais, Robert Asembo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria, hivyo wameamua kuuanzisha upya kwa faida ya nchi hizo.
 
Amesema hivi karibuni FKF ilichukua waamuzi kutoka Tanzania waliochezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana), hivyo wameamua kubadilishana waamuzi kwa lengo la kuwaongezea uzoefu.
 
“Waamuzi wa Tanzania walichezesha vizuri mechi ile. Unajua kwetu kuna upinzani mkubwa katika klabu kama AFC Leopards na Gor Mahia, ukipanga refa utasikia wengine wanalalamika, mara huyo ni Mjaluo. Hata akichezesha vizuri bado watalalamika tu kutokana na upinzani uliopo katika klabu hizo,” amesema.
 
Rais Nyamweya ameongeza kuwa ili kuondoa malalamiko katika mechi za aina hiyo wanaweza kuchukua waamuzi kutoka Tanzania, na vilevile waamuzi kutoka Kenya wakachezesha mechi za aina hiyo nchini Tanzania.
 
Amesema vilevile wamepanga kuangalia uwezekano wa kuwa na mechi za kuandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu za nchi hizo ambapo washindi watatu au wanne wa kwanza katika ligi hizo kushindana.
 
Kwa upande wa mafunzo, wamekubaliana kuwa kwa vile kila nchi ina wakufunzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na la Afrika (CAF) watawatumia kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa waamuzi, makocha, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi badala ya kusubiri mafunzo ya aina hiyo kutoka kwa mashirikisho hayo ya kimataifa.
 

Thursday, October 18, 2012

BREAKING NEWS: YANGA YAMALIZANA NA VODACOM JUU YA RANGI YA NEMBO YAO KWENYE JEZI



Kampuni ya simu za mkononi Vodacom, ambao pia ni wadhamini wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, wamefikia muafaka na klabu ya Yanga juu ya kutotumia jezi zenye nembo nyekundu.
Vodacom imefikia hatua hiyo kufuatia Yanga kupeleka maombi yao ya kuomba kutotumia nembo hiyo nyekundu katika jezi zao.
Kufuatia maombi ya klabu ya Yanga kupitia kwa viongozi wake na baraza la wazee, vodacom imeona ni busara kuwasikiliza Yanga maombi yao na hivyo kuamua kuipa nafasi ya kuchagua nembo moja kati ya tatu.
Vodacom imetoa aina tatu za nembo na Yanga inapaswa kuchagua moja kati ya hizi nembo tatu.
Swali kwa mashabiki wa Yanga, ipi nembo nzuri kati ya hizi tatu?

GOLI LA SIKU: LIONEL MESSI VS CHILE

BAADA YA KUPIGWA BENCHI SANA - GOLIKIPA WA BARCA AGEUKIA UTENGENEZAJI MUZIKI

Baada ya kukaa becnhi kwa muda mrefu katika kikosi cha Barcelona golikipa Jose Pinto amethibitisha kupita akaunti yake ya  Twitter kwamba amesaini mkataba wa kutengeneza muziki wa bendi ya rap Delahoja.


Mchezaji huyo wa Celta amesaini mkataba huo na Sony Music Spain kusaidia kutengeneza na kulifanyia promotion kundi hilo ambalo amekuwa na ukaribu nalo kwa zaidi ya miaka 20.

"Mkataba umesainiwa (baada ya miaka 22 ya kufanya kazi ya uproduyza) na Sony Music Spain," aliandika kwa mashabiki wake 168,000 wa Twitter.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Hispania vimekuwa vikimtania Pinto tangu habari hizi zitoke kwamba amepata kazi ya kufanya zaidi ya kukaa kwenye benchi la Barcelona huku akimuacha Victor Valdes akitamba kwenye milingoti mitatu ya Blaugurana

EXCLUSIVE: "BANGI, POMBE NA MADAWA YA KULEVYA NDIO CHANZO CHA KUSHUKA KIWANGO CHETU" - ASEMA MLINZI WA KAMBI

-->
Mojawapo ya vitu vinavyochangia kushusha Perfomance ya Mchezaji au Timu inapokuwa uwanjani ni  Mazingira mabovu ya Kambi pamoja na namna Wachezaji wanavyoishi katika Kambi hiyo, kwa kuendekeza Vitendo vya Starehe zilizopitiliza ama uvivu wa Mazoezi.
Katika Hali isiyokuwa ya Kawaida ni vigumu sana kuona Timu ikiperfom katika kiwango chake kilichozoeleka , wakati Mazingira ya Kambi wanayoishi hayaeleweki kwa Wachezaji wake kuendekeza Starehe zilizopitiliza huku wengine wakisahau wajibu wao.
Hivi karibuni Shirikisho la Mpira Wa miguu nchini TFF lilitangaza Vita dhidi ya Wachezaji watakaobainika  kutumia BANGI ama madawa ya Kulevya, taarifa ambayo ilionekana kupokewa katika Mitazamo tofauti na Wadau mbalimbali wa Mpira wa Miguu Tanzania huku wengine wakihoji Iwapo Shirikisho hilo litaweza kutimiza ahadi hiyo .
Taarifa Hiyo ya TFF mbali na kuzua maswali mengi kwa Wadau wa Michezo nchini pia imezua hofu kubwa kwa Wadau hao kutokana na uwepo wa Taarifa ya kwamba asilimia kubwa ya Wachezaji wa Kibongo wanatumia Bangi pamoja na Madawa ya kulevya huku wengi kati yao Wakitoka katika Vilabu vikubwa na vikongwe hapa nchini.
Swali kubwa linalozuka hapa ni kwamba je TFF itaweza kupambana na nguvu ya Vilabu hivi vikongwe kwa kuwaadhibu wachezaji wake ambao wengi ni nguzo ya Timu hizo??? hilo ndilo swali ambalo hadi sasa wadau wa Mpira wa miguu Tanzania wanasubiri kuona namna sinema hiyo itakavyokuwa.
 Wakati wadau wa Soka nchini wakisubiri Rungu hilo la TFF kuanza kufanya Kazi Mtandao wa www.shaffihdauda.com  umepenyezewa taarifa zinazosema kuwa Mlinzi wa Kambi ya DAR YOUNG AFRICAN(Jina limehifadhiwa) ameuandikia barua nzito uongozi wa Klabu hiyo akielezea namna Wachezaji wa Klabu hiyo kongwe wanavyoisjhi kambini hapo.
Katika Barua yake Mlinzi huyo ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Wachezaji wa Klabu hiyo ikiwemo vya utumiaji wa BANGI, Pombe, pamoja na Madawa ya kulevya(UNGA)
Mlinzi huyo ameuambia  Uongozi wa Klabu ya YANGA kuwa tangu alipobaini vitendo hivyo kufanyika klabuni hapo, baadhi ya Wachezaji wanaofanya Vitendo hivyo wamekuwa wakimchukia na hata wengine kupunguza ukaribu na Mlinzi huyo kama ilivyokuwa hapo awali.
 Miongoni mwa Wachezaji walioelezwa kujihusisha na vitendo hivyo ni Kiungo mkabaji wa Timu hiyo ATHUMANI IDDI CHUJI, ambaye awali aliwahi kukiri kutumia Madawa ya kulevya (UNGA) na kuthibitisha kuwa kwa sasa hana mpango nayo tena.
Taarifa ya Mlinzi huyo pia imethibitisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa hiyo ikawa ni mojawapo ya sababu inayopelekea timu hiyo kutofanya vizuri katika baadhi ya michezo yake ya Ligi Kuu Tanzania bara inayoendelea.
Taarifa hiyo imekuja wakati klabu ya YANGA inatafuta sababu zinazopelekea baadhi ya wachezaji wake kucheza chini ya Kiwango, katika mechi zilizopita za Ligi Kuu Tanzania bara,na suala lililobaki sasa ni kuangalia Klabu hiyo itafanyia vipi kazi ripoti ya Mlinzi huyo.

MDENMARK MWENYE ASILI YA TANZANIA PATRICK MTILIGA APIGWA MARUFUKU TIMU YA TAIFA YA NCHI HIYO KWA UTOVU WA NIDHAMU

Beki wa Kimataifa wa Denmark, Patrick Mtiliga, mwenye asili ya Tanzania ameambiwa hataichezea Timu ya Taifa tena baada ya kugoma kucheza Mechi  ya juzi ya Nchi hiyo ambayo Denmark ilichapwa 3-1 na Italy kwenye Mechi ya Kombe la Dunia.
Kocha wa Denmark, Morten Olsen, alisema Beki huyo awali alijulishwa atakuwa Benchi na Simon Poulsen ataanza badala yake lakini, wakati wachezaji wanapasha viungo moto kabla mechi kuanza huko jijini Milan, Poulsen aliumia na Mtiliga akajulishwa atacheza mechi hiyo lakini akagoma.
Olsena amesema: “Nipo kwenye Soka kwa Miaka 40 sasa lakini sijashuhudia kitu kama hiki. Amewaangusha wenzake!”
Olsen aliongeza: “Nilimwambia Patrick apashe lakini alikuwa amehuzunika baada ya kwanza kuambiwa hachezi mechi hiyo atakuwa benchi na akasema hawezi kucheza. Hapo ndipo nikamwambia aondoke kwenye kikosi changuna hiyo ndio ilikuwa mechi yake ya mwisho kucheza wakati mimi nikiwa mwalaimu wa hii timu."
 Mtiliga ambaye alikuwepo katika kikosi cha Denmark kilichoshiriki kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka 2010, pia mwanzoni alikuwa akiichezea klabu ya Malaga ya Spain kabla ya kuhamia timu ya FC Nordsjaelland.

EDO KUMWEMBE: MBWANA SAMATTA ANATAKIWA AWE NAHODHA WA TIMU YA TAIFA.

Mchambuzi na mwandishi wa habari za michezo Edo Kumwembe leo asubuhi ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba anaamini mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea TP Mazembe kwa mafanikio, anapaswa kuwa nahodha wa timu yetu ya taifa.                                                                  Je wewe kama wewe mdau wa soka una maoni gani? Unadhani Samatta anastahili kuwa nahodha wa timu ya taifa, je huu ni muda sahihi wa Samatta kupewa beji ya timu ya taifa?? Funguka.

WAYNE ROONEY AIBEBA ENGLAND JIJINI WARSAW - IKITOKA SARE NA POLAND


[www.online-soccer.ru] Poland 1-1 England GOALS by all-goals

AZAM: MWAMUZI KATUNYIMA GOLI 2 ZA WAZI NA KUSABABISHA SARE DHIDI YA PRISONS

Uamuzi mbovu wa mwamuzi wa kati na mshika kibendera leo umeipokonya ushindi Azam FC dhidi ya Tanzania Prisons baada ya mwamuzi kukataa magoli mawili ya Abdi Kassim Baby na penati ya wazi baada ya mchezaji Salum Abubakar kuangushwa ndani ya eneo la hatari
Goli la kwanza mwamuzi kulikataa ulikuwa ni mkwaju wa mbali wa Abdi Kassim ambao ulitinga nyavuni kabla ya kurudi uwanjani na mwamuli licha ya kuona kuwa lilikuwa ni goli bado akaamua kukataa
Baadaye Salum Abubakar Sureboy alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la 18 na kwa mshangao wa wengi wakiwemo viongozi na wachezaji wa Prisons ambao walishashika vichwamwamuzi akapeta na mpira kuendelea
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mpira kumalizika, Azam FC ilipata adhabu ndogo na Abdi Kassim aliupiga mpira ule na kutinga ndani ya nyavu lakini kwa mara nyingine tena mwamuzi akakataa kwa madai kuwa kabla ya kufunga Abdi Kassim alikwa ameotea wakati Abdi alifunga kutokana na mpira wa adhabu ndogo.
Kutokana na hali hii mpambano kati ya Azam FC na Tanzania Prisons ulimalizika kwa sare ya 0-0
(Source http://www.azamfc.co.tz)

MAMBO 5 CRISTIANO RONALDO ANAYOMZIDI LIONEL MESSI UWANJANII


Sihitaji kuulezea zaidi huu mjadala mpaka kufikia hapa. Ronaldo vs Messi - mjadala huu kwa sasa hauna mwisho.

Nani mchezaji bora wa dunia kwa sasa? Sijui na sitaki kuingia kwenye mjadala huu usioisha. Pointi iliyopo hapa wote wawili Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wote wana maeneo waliyo dhaifu na imara. Kila mmoja wao amebarikiwa kwa namna yake.

Uimara wa yoyote baina yao unaodhani ni muhimu kwa mafanikio ya timu yake, Ronaldo na Messi ndio wachezaji bora wa kizazi hiki na wanapaswa kupewa kila sifa kutokana na soka safi wanalotuonyesha kila wiki.

Kwa kuanzia leo ebu tumuangalia Cristiano Ronaldo ambaye wiki amekuwa na matukio mawili makubwa kuwa mwanamichezo wa kwanza kufikisha idadi ya mashabiki million 50 kwenye mtandao wa Facebook pamoja na kutimiza mechi 100 akiwa na timu ya taifa ya Ureno. Je katika mjadala wa nani mchezaji bora, ushawahi kujiuliza ni vitu gani ambavyo winga huyo wa Real Madrid anavifanya vizuri kuliko mpinzani wake? Ebu tujaribu kuchambua.

1: MBIO / KASI

 
Lionel Messi anaaminika ndio mchezaji hatari sana linapokuja suala la one on one na mabeki, lakini hamfikii Ronaldo katika suala la spidi.

Hii ni silaha kubwa ya Ronaldo inayomfanya anakuwa bora zaidi ya wenzie. Wachache sana wana mbinu kama zake za kiufundi na uwezo wa kukimbia na mpira, lakini hakuna anaweza kukimbizana na spidi ya Cristiano Ronaldo.

Hili linafanya Ronaldo awe ni hatari kubwa hasa kwenye mashambuliizi ya kushtukiza.
Wakati Messi ni hatari zaidi anapokuwa na mpira, then hakuna ubishi Cristiano Ronaldo ni hatari zaidi anapokuwa bila mpira.

2: FREE-KICKS/ ADHABU NDOGO

 
Messi amekuwa akiongeza ubora kwenye eneo hili kila anapopata nafasi ya kupiga adhabu ndogo.

Japokuwa, ikiwa nitatakiwa kumchagua mchezaji wa kupiga adhabu ndogo ya umbali wa yadi 25, hasa ikiwa katika eneo la kati kati lilotazamana na goli, kwa mimi bila shaka nitamchagua Ronaldo.

Hakuna mchezaji anayeweza kupiga mashuti kwa namna anayoweza kuipiga Ronaldo ikiwa kwa hali ya kasi na kushtukiza, ushahidi mzuri anao golikipa wa mbrazili Julio Ceaser. Ana uwezo wa kupiga mashuti ambayo mueleko wake ni danganyifu.

Pindi Ronaldo anapokwenda kuchukua mpira na kuweka kwenye eno la kupiga faulo, huku akirudi nyuma hatua zisipungua tatu na kushusha pumzi kwa nguvu, uwanja mzima unakuwa kimya na kuweka umakini kwenye miguu ya mreno huyo - hii inaonyesha ni namna gani nahodha huyu wa Ureno anavyotisha katika eneo hilo.

3: MAPAMBANO YA HEWANI


Nafikiri kwamba Lionel Messi anapata wakati mgumu kupiga mipira ya kichwa kwa sababu ndogo tu ya kimo chake cha 5'7, lakini hilo halimaanishi hawezi kuiumiza timu pinzani kwa mipira ya hewani - unabisha waulize washabiki wa Man United alichowafanya katika fainali ya UEFA mwaka 2009.

Kwa upande wa Ronaldo, akiwa na kimo cha 6'1 anaweza kupambana na karibia mabeki wote huku akiwa na wepesi wa kuruka na kupiga vichwa katikati ya mabeki hata waliomzidi urefu.

Hili ni moja ya eneo mojawapo ambalo Ronaldo anamzidi Messi kwa kiasi kikubwa.

KUZUIA / KUKABA

Wote wawili Ronaldo na Messi wanaweza kurudi nyuma na kuzia mashambulizi wakati wapinzani wanapokuwepo kwenye eneo la hatari la goli lao.

Kwa wafuatiliaji wazuri tumekuwa tukishuhudia utofauti wawili katika kukaba, kiuhalisia kutokana na umbo lake dogo Messi akiwa na kimo cha 5'7, njia sahihi yake ya kukaba bila kujipa shida na kuingilia pasi za maadui, wakati Ronaldo kutokana na maumbile yake anaweza kuweka ukuta katika upigiwaji wa adhabu ndogo, anaweza kukaba kwa kutumia kasi yake pamoja na nguvu alizonazo, na amekuwa akifanya hivyo mara tu timu yake inaposhambuliwa.

Hawatofautiani sana lakini kwa namna ambavyo tumekuwa tukiwaona, Ronaldo amedhihirisha kwamba ni mzuiaji mzuri kuliko Messi.

NGUVU


Kwa sababu tu ya maumbile ya Ronaldo alivyoumbwa na mwili wake ulivyojengeka, anakuwa na uwezo wa kufanya vitu kadhaa vizuri zaidi ya Messi.

Tofauti yao moja kubwa, Ronaldo anaweza kukufunga kwa shuti la umbali wowote kutoka katika nusu ya kiwanja na hilo mara kadhaa limekuwa likiwapa hofu magolikipa.Kwa upande wa Messi kutokana na jinsi alivyo ni vigumu kuweza kufikia uwezo wa nguvu za Ronaldo katika eneo hilo.

Messi kiuhalisi amejaaliwa zaidi ujuzi wa kumiliki mpira na touch nzuri, lakini Ronaldo ana nguvu na uwezo wa kuchezea mpira vile vile, kwa maana hiyo kutokana na nguvu alizonazo Ronaldo zinampa nafasi ya kumzidi mpinzani wake kwenye eneo lingine.

SIMBA 2:2 KAGERA SUGAR KWENYE PICHA



 Mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu akishangilia bao la kwanza aliloifungia timu yake dhidi ya Kagera Sugar wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka sare ya 2-2. (Picha na Habari Mseto Blog)
 Beki wa Kagera Sugar, Salum Kanoni (kushoto) akichuano na mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi
Kiungo wa Kagera Sugar, Malegesi Mwangwa akichuana na mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngassa
Beki wa Kagera Sugar, Amandus Nesta akimiliki mpira huku akizongwa na beki wa Simba, Amir Maftah katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka sare ya 2-2