Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam
WAGONGA nyundo wa
Mbeya, Mbeya City FC wameanza mazoezi
yao leo hii kuwawinda wana Lambalamba, Azam fc aprili 13 mwaka huu katika
mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa dimba la kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
Taarifa iliyotolewa na
afisa habari wa klabu hiyo, Freddy Jackson imeeleza kuwa mazoezi ya leo
yamekwenda vizuri na malengo yao ni kuibuka na ushindi katika dimba lao la
nyumbani ambalo hawajawahi kufungwa tangu waanze ligi kuu msimu.
Wakati huo huo, kocha
mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi ameueleza mtandao huu kuwa wao walijiandaa
kwa mechi zote 26 za ligi, hivyo mchezo ujao dhidi ya Azam fc watapambana
kusaka pointi tatu muhimu.
“Ligi imekuwa ngumu
sana msimu huu. Kila klabu imejipanga kutafuta matokeo. Lakini mimi siwezi kuwaahidi
mashabiki lolote zaidi ya kusubiri mechi yenyewe. Cha msingi waendelee kutuunga
mkono zaidi ili kufikia malengo yetu”. Alisema Mwambusi.
Kocha huyo aliyejijengea
jina kubwa baada ya kuchachafya msimu wake wa kwanza wa ligi kuu akiwa na Mbeya
City, aliongeza kuwa matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Ashanti United ambapo
walitoka suluhu pacha ya bila kufungana yaliwaharibia kwa kiasi kikubwa katika
mbio zao za kuwania ubigwa.
“Nilisema toka mwanzo
kuwa mechi ya Ashanti ingekuwa ngumu kwetu. Mazingira ya uwanja wa ugenini si
sawa na nyumbani”.
“Pia mazingira ya
Ashanti ambao wanakwepa kushuka daraja yaliufanya mchezo uwe na presha kubwa
kwa upande wetu, lakini tunajipanga dhidi ya Azam fc”. Alisema Mwambusi.
Rasmi Mbeya City baada
ya kutoka suluhu pacha dhidi ya Ashanti United,
walishajitoa kuwania ubingwa, huku wakiwaombea mabaya Yanga wasifanye
vizuri mechi zao tatu ili waambulie nafasi ya pili.
Mpaka sasa City wapo
nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi
24 na kusaliwa na mechi mbili tu mkononi.
Kama watashinda mechi
zote watafikisha pointi 52 ambazo Yanga wanaweza kuzivuka katika mechi zao tatu
walizosaliwa nazo.
Kama Mbeya City
wanahitaji nafasi ya pili wanatakiwa kuwaombea Yanga watoe sare mbili na
kupoteza mechi moja ili wafikishe pointi 51 ambazo wataweza kuzivuka kama
watashinda mechi mbili walizonazo mkononi mwao.
Hata hivyo inaonekana
kutokuwa rahisi kwa Yanga kutoa sare mechi mbili kwasababu ya ubora wao.
Ingawa kwenye mpira
lolote linaweza kutokea, lakini bado Yanga wanaonekana kuwa na uchu mkubwa
zaidi katika mechi zilizosalia kuanzia ya jana ambayo walishinda mabao 5-1
dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.
Yanga wanatarajia kukutana
na Kagera Sugar jumatano ya wiki hu uwanja wa Taifa, na baada ya hapo watasafiri
kwenda Arusha kuwafuata JKT Oljoro na kufunga pazia la ligi kuu dhidi ya Simba
sc uwanja wa Taifa Aprili 19 mwaka huu.
Nafasi inayoonekana
kuwa wazi kwa Mbeya City ni ya tatu.
Na kama wataambulia
hiyo, haitakuwa mbaya kwao kwani ni
msimu wao wa kwanza.
Hata hivyo itawauma
kwasababu walikuwa na mategemeo makubwa japokuwa wameshindwa kuyafikia kutokana
na ushindani wa timu zote.
Mechi ijayo wanacheza
na Azam fc na baada ya hapo watamalizia kibarua chao na Mgambo JKT Aprili 19
mwaka huu uwanja huo huo wa Sokoine.
No comments:
Post a Comment