Pichani kulia ni Nuhu , Dk Mwankemwa (katikati) na Karim Mapesa (kushoto) wakiwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
(Picha na Tovuti ya Azam)
(Picha na Tovuti ya Azam)
Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam
IKIWA ni sehemu ya
kuwajali wanandinga wake, vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc, alfajiri ya leo wamemsafirisha beki wao wa
pembeni Samih Hajji Nuhu kwenda Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa
upasuaji wa goti la mguu wa kushoto.
Taarifa iliyotolewa na Azam fc kupitia
Tovuti yake, Nuhu ameongozana na Daktari Mkuu wa
klabu hiyo, Dk Mwanandi Juma Mwankemwa pamoja na Mweka Hazina wa timu,
Abdulkarim Shermohamed Bahadour.
Nuhu atafanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vincent Palocci mjini Cape Town
na Mtaalamu, Dk. Nicholas, ambaye ameweza kuwarudisha uwanjani wachezaji wengi
wa Afrika Kusini waliopata maumivu makubwa.
Hii itakuwa mara ya
tatu kwa Nuhu kufanyiwa operesheni ya goti hilo, baada ya awali kufanyiwa mara
mbili nchini India, kwanza katika hospitali ya Mumbai chini ya Dk. Tanna na ya
pili hospitali ya Pune.
Nuhu amekuwa nje ya
Uwanja tangu mwaka jana na msimu huu wote hajagusa mpira kwa sababu ya maumivu
hayo.
Wakati huo huo Taarifa
njema kwa mashabiki wa Azam fc ni kwamba
mshambuliaji wake, Joseph Kimwaga Lubasha ameanza mazoezi mepesi baada
ya kupata ahueni ya maumivu ya goti yaliyokuwa yakimsumbua.
Kimwaga amepewa
programu maalum na dawati la tiba la Azam FC, chini ya Daktari Mkuu, Mwanandi
Mwankemwa ambayo anaendelea hivi sasa.
Mchezaji huyo
anatarajiwa kurejea rasmi uwanjani msimu ujao, baada ya kuwa nje kwa miezi
miwili ya mwisho ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu
huu.
Mbali na Kimwaga,
wachezaji wengine majeruhi Azam FC ni beki wa kati, Ismail Gambo ‘Kussi Jr’
ambaye ataendelea kuwa nje kwa miezi miwili zaidi, viungoFarid Mussa na Ibrahim
Mwaipopo ambao wote watakuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja, maana yake kwa msimu
huu hawatacheza tena.
Azam fc wanajiandaa na
mchezo wa kesho kutwa ligi kuu soka Tanzania bara kwenye uwanja wa Mabatini
Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting.
Hii itakuwa mechi
muhimu kwa Azam fc katika mechi tatu zilizosalia kuhitimisha msimu huu wa
2013/2014.
Mpaka sasa Azam fc wapo
kileleni baada ya kujikusanyia pointi 53 kwa kucheza mechi 23.
Kama Azam fc wanataka
kutwaa ubingwa msimu huu wanahitaji kushinda mechi mbili kati ya tatu walizobakiza
ili kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao wakubwa, Yanga SC.
Yanga wapo nafasi ya
pili kwa pointi 49, na wamebakiza mechi tatu ambazo wakishinda zote watafikisha
pointi 58 ambazo Azam fc watazivuka endapo watashinda mechi mbili kati ya tatu walizosaliwa
nazo.
Mechi ya jumatano
mabatini itakuwa na changamoto kubwa kwa Azam fc kwasababu Ruvu Shooting ina
kikosi cha vijana wanaojua kucheza mpira.
Hata kama hawahitaji ubingwa
wala nafasi tatu za juu wala kukwepa kushuka daraja, Shooting wataingia kwa
lengo la kuvunja rekodi ya kutofungwa kwa Azam fc msimu huu.
Afisa habari wa Ruvu
Shooting, Masau Bwire alinukuliwa na mtandao huu kuwa wao watakuwa wa kwanza
kumfunga Azam fc baada ya kushindikana katika mechi zake 23 alizocheza mpaka
sasa.
“Azam ni kisiki cha
mpingo. Timu zote zimeshindwa kuwang`oa. Sisi Ruvu Shootinga tutawang`oa hata
kwa gereda. Tunajianda vizuri kuwaonesha Lambalamba kuwa sisi si timu ya kubeza
hata kidogo”. Alisema Masau.
Wakati hayo yakijiri
kwa Ruvu Shooting, Jafar Idd Maganga, Afisa habari wa Azam fc, aliueleza mtandao huu kuwa kazi bado ipo mbele
yao na wanashindana mpaka mechi ya mwisho.
“Hatuwezi kuwaza
ubingwa kwa sasa, kwasababu mechi bado zipo. Ligi bado. Mpaka tutakapocheza
mechi zote na kushinda ndio tutajihesabia kutwaa ubingwa”. Alisema Jafar.
Wakati Azam fc
wakijiandaa na mchezo wa keshokutwa, nao mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Dar
Young Africans watakuwa na kibarua kizito dhidi ya `Wanankulukumbi` Kagera
Sugar katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Huu utakuwa mchezo
muhimu kwa Yanga kwani watahitaji ushindi tu na si matokeo ya aina nyingine.
Hans Van Der Pluijm
anayesemekana kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu, atakuwa anakabiliana na
Kagera Sugar ambao hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.
Mpaka sasa Kagera Sugar
wapo nafasi ya 5 baada ya kushuka
dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 24.
No comments:
Post a Comment