Na baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976 ua 0764302956
WAKONGWE wa ligi kuu soka Tanzania bara, Simba sc na Yanga hakika msimu huu wanahenyeshwa vilivyo na timu mpya katika medani ya soka la Tanzania, Azam fc na Mbeya City.
Simba sc jana walitoneshwa kidonda na Coastal Union baada ya kulala bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Yanga wenyewe angalau wamepumua baada ya ushindi wa mabao 3-0 jumamosi ya wiki iliyopita katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, mjini Tabora dhidi ya Rhino Rangers.
Ulikuwa ushindi wa kwanza tangu Yanga itupwe nje ya mashindano ya kimataifa na Ally Ahly ya Misri machi 9 mwaka huu jijini Alexndria.
Mpaka sasa Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 43, huku Mtani wake akiendelea kusuasua katika nafasi ya nne baada ya kujikusanyia pointi 36.
Nafasi ya kwanza wapo wageni Azam fc ambao hawajawahi kutwaa ubingwa wa Tanzania bara tangu kupanda mwaka 2008/2009.
Nafasi ya tatu wapo wageni zaidi, Mbeya City FC wenye pointi 42.
Simba sc na Yanga ni klabu kongwe na zenye mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania.
Timu hizi zinapendwa zaidi na kusababisha matatizo makubwa kwa mashabiki wake ikiwemo kuzirai viwanjani na wakati mwingine kupoteza maisha.
Lakini msimu huu wa 2013/2014, zimekumbana na changamoto kubwa kutoka kwa timu mpya.
Haikuwa rahisi miaka ya nyuma kukuta Yanga na Simba wanahenya kiasa hiki katika kutafuta nafasi za juu.
Mpaka sasa Yanga bado wana matumaini ya kutetetea ubingwa wao, huku wakiwaombea dua mbaya Azam fc wenye dhamira kama yao.
Kikosi cha Azam fc chini ya kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog kinahitaji ubingwa tu kwasababu tayari kwa zaidi ya misimu miwili kimeshika nafasi ya pili.
Kwa uwekezaji wa Azam fc katika kikosi chao, ubingwa ndio faraja yao na si vinginevyo.
Wakati wakihaha kuwapoka Yanga Ubingwa, Hans Van Der Pluijm, kocha mkuu wa wanajangwani anaumiza akili kutetea ubingwa ulioachwa na mholanzi mwenzie, Ernie Brandts.
Kwa upande wa kocha wa Simba Dravko Logarusic amekuwa katika hali tete zaidi kutokana na kushindwa kuwapa mafanikio mzunguko huu wa pili.
Haijulikana kama wachezaji wake ndio wanamuangusha au yeye amekosa mbinu za ushindi.
Lakini ukiwaangalia wachezaji wake, mfano jinsi ambavyo Haruna Chanongo alikuwa anachekelea kukosa mabao jana, utagundua kuna mdudu anawatafuna Simba nyuma ya pazia.
Nilishawahi kusema matatizo ya wana Simba yatatatuliwa na wanasimba wenyewe.
Nirudi uwanjani sasa. Yanga wanajiandaa na mchezo wa kesho kutwa dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Mechi hiyo muhimu itachezwa uwanja wa Taifa, na ushindi kwa timu zote mbili unahitajika sana.
Ugumu wa mchezo huo upo katika mazingira ya aina mbili;
Mosi; Yanga wanasaka pointi tatu muhimu ili kuwasogelea Azam fc waliopo kileleni.
Wataingia kwa malengo ya kutafuta ushindi tu na si matokeo mengine.
Mawazo ya wachezaji, viongozi, na benchi la ufundi ni kupata pointi tatu.
Bila shaka kocha Pluijm anatambua umuhimu wa mechi hiyo kwake. Hivyo lazima awatulize akili vijana wake.
Kwa kiwango walichoonesha Yanga katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Azam fc na Rhino Rangers kule Tabora, wana asilimia kubwa ya kupata ushindi dhidi ya Prisons.
Uzuri Yanga wamegundua kuwa ligi ni ngumu ndio maana kocha wake, Hans Van Pluijm akisaidiwa na Boniface Mkwasa wanajitahidi kuiandaa timu kwa nguvu zote.
Yanga wana kikosi kilichosheheni nyota wakali msimu huu, kinachokosekana kwao ni namna ya kukitumia.
Sio kwamba Pluijm anashindwa kupanga timu, la hasha!, lakini kuna shida ndogo ndogo katika kikosi chake.
Mfano safu ya ushambuliaji inayoongozwa na nyota wa kimataifa, Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na watanzania, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Hussein Javu na Jery Tegete imekuwa ikishindwa kutumia nafasi wanazopata.
Wanao viungo bora kama Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Athuman Idd `Chuji`.
Sina shaka katika kutengeneza nafasi za mabao. Hapo Yanga wanaweza, lakini umaliziaji ni ugonjwa kwao.
Kama Yanga watabadilika na kuwa makini na nafasi wanazotengeneza, basi tunatarajia mabao katika mchezo dhidi ya Prisons.
Pili; Ugumu wa mechi hii pia, unatokana na mazingira ya Prisons.
Wajelajela wapo nafasi ya 10 kwa kujikusanyia pointi 22.
Kwa nguvu zote wanahitaji ushindi ili kuendelea kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kuna wakati mechi inayowakutanisha watu wanaohitaji ubingwa na wanaotafuta njia ya kukwepa daraja inakuwa ngumu zaidi.
Prisons chini ya kocha wao, David Mwamwaja wamekuwa bora zaidi na wamepoteza mechi moja dhidi ya Kagera Sugar tangu mzunguko wa pili uanze.
Wanaonekana kubadilika na kucheza mpira wa malengo tofauti na mzunguko wa kwanza.
Wamekuwa watulivu na wanapanga mipango ya uwanjani na kuoenesha ufundi wa soka.
Waliwabania Simba sc uwanja wa Sokoine na kudhihirisha kuwa si wepesi tena kupoteza mechi.
Bila shaka wataingia kwa nguvu na kupambana na Yanga ambao watakuwa nyumbani.
Kwa miaka mingi Uwanja wa Taifa umekuwa mgumu kwa timu za mikoani hasa zinapokutana na Simba au Yanga, lakini msimu huu mambo yamebadilika kidogo.
Inafahamika kuwa Yanga inashangiliwa na mashabiki lukuki inapokuwa uwanja wa Taifa kwasababu wamekuwa na makali msimu huu, huku wakisaka taji lao kwa mara nyingine.
Prisons watakumbana na `presha` kubwa ya mashabiki wa Yanga, lakini kitakachotakiwa kwao ni kupuuza kelele za maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanja Taifa.
Kupata pointi tatu mbele ya Yanga itakuwa ngumu kwao, lakini aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Zambia, Chipolopolo, Herve Ranard alisema mpira wa miguu ni mipango.
Timu itakayokuwa na mipango uwanjani inaweza kupata matokeo chanya.
Hakuna ushindani wa majina kati ya Yanga na Prisons, lakini si ajabu kuona wajelajela wanaibuka na ushindi, kwasababu wapo katika harakati za kukwepa daraja.
Uchambuzi wako sio mzuri kwasababu husemi azama ana pointi ngapi ili ugumu uonekane, hauko makini
ReplyDelete