Search This Blog

Tuesday, March 25, 2014

NIONAVYO MIMI: MATA NA OZIL WATAKUWA WAMEROGWA.

Na Oscar Oscar Jr 
0789-784858

Huwa sishangai ninapokuwa kijijini kwetu Kaliua pindi ninapoona wazazi wakimpeleka mtoto wao kwa "sangoma" aliyegongwa na baiskeli, hata siku moja sioni ajabu ninapowakuta wazazi wanampleka kwa mganga kijana aliyeumia wakati anacheza mpira shuleni na watoto wenzie. Nitaanzaje kuwabishia, wakati kwao kila tatizo linaletwa na uchawi? Unamkatalia vipi mtu anayeamini kuwa, huwezi kufanikiwa bila nguvu za giza na kila tatizo ni kurogwa?

Siwezi kukataa kwamba uchawi haupo kwa sababu hata vitabu vitakatifu vimethibitisha uwepo wa jambo hilo lakini,ni lazima tukubali kuwa,mpira unahitaji zaidi masuala ya kitaalamu na sio kujipaka majivu usoni. Wakati timu zetu za hapa nyumbani zikiendelea kutamba kwa kombe la "Ushirikina", klabu ya Dedebit kutoka nchini Ethiopia, imezindua mpango imara wa timu za U-13, U-15 na U-17. Vijana hao wanapewa chakula mara 4 kwa siku na mtaalamu na wanaingia darasani kufundishwa saikolojia mara 2 kila wiki.

Mchezaji wa soka anatakiwa kula chakula masaa matatu kabla ya mchezo kuanza, lakini hapa kwetu, unauwezo wa kumpa mchezaji muhindi wa kuchoma na maembe dakika thelethini kabla ya mechi na akala bila kuona tatizo lolote. Kwani kuna mtu anajali? Ukitazama mechi za ligi kuu Tanzania Bara,utagundua kuwa,mpira unachezwa uwanjani kwa dakika 30 tu, zilizobaki,zinamalizika kwa kurusha, kufanya mabadiliko ya wachezaji na malumbano kati ya ama wachezaji kwa wachezaji au benchi la ufundi na mwamuzi. Tumerogwa?

Mesut Ozil ameshindwa kufanya vizuri na Arsenal sio kwa sababu amerogwa, wenzetu wanaangalia mpira kiufundi, kitaalamu na kwa jicho la tatu. Ozil ni mzuri anapocheza na viungo wenye uwezo mkubwa wa kukaba, akiwa na timu ya Real Madrid, alizungukwa na Xabi Alonso na Semi Khedira na anapokuwa timu ya taifa, anakwenda na Khedira huku akiwakuta kina Bastian Schweinstiger, Toni Kroos, Thomas Muller na mafundi kibao wa aina hiyo.

Ozil ni mzuri pale timu inapokuwa na mpira na ukubwa wa jina lake unatokana na uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho. Ana uwezo wa kutengeneza wastani wa mabao 20 kwa msimu mmoja na sikushangaa Cristiano Ronaldo alipolalamika baada ya kupata taarifa za kuuzwa kwa fundi huyo wa kijerumani.

Mesut Ozil alianza maisha yake mapya na Gunners kwa mafanikio na sababu kubwa ni uwepo wa box to box midfielder, Aaron Ramsey ambaye alikuwa na msimu mzuri sana na Arsenal. Ramsey ni mchezaji ambaye haridhiki na kukaa sehemu moja, atakwenda kushambulia timu inapokuwa inamiliki mpira na, atarudi kukaba pale wanapopoteza. Wengi hawalitazami hili, tangu kuumia kwa kiungo huyo kumekuwa hakuna mtu wa kudumu wa kuziba mapungufu ya Ozil hasa timu inapokuwa haina mpira.

Mikel Arteta, Oxlade Chambarlain, Jack Wilshare, Santiago Carzola na Thomas Rosicky hawa wote sio viungo wakukaba asilia na mtu pekee aliopo ni Methew Flamini ambaye naye ubora wake unaonekana timu ikicheza na Cardiff City, Fulham, Sunderland na hupotea kabisa, anapokutana na miamba kama kina Yaya Toure, Fernandinho, Nemanja Matic na mafundi wengine. Na hili nalo linahitaji twende kwa sangoma?

Juan Mata naye, hana tofauti sana na Ozil. Anafanya vizuri sana akicheza kama namba 10 na msimu uliopita akiwa na Chelsea, aliweza kupika magoli 12 ya ligi na kufunga 12 na kumfanya achaguliwe kama mchezaji bora wa mwaka wa klabu hiyo kwa msimu wa pili mfululizo. Namna anavyotumika pale u
United, hawezi kucheza kwenye ubora wake kwa sababu anatumiwa kama winga nafasi ambayo haimudu vizuri. 

Mata anahitaji pia muda wa kutosha uwanjani ili aweze kurejea kwenye kiwango chake, karibu nusu ya msimu huu ameutumia akiwa benchi pale Chelsea kabla ya kujiunga na United na ndiyo maana hata kwenye timu ya taifa ya Hispania iliyochaguliwa kucheza mechi ya kirafiki na Italia, hakuweza kujumuishwa. Unataka afanye nini zaidi au tumpeleke kwa mganga?

Ukiwa na timu ambayo haina kiungo namba 6 na 8 wa maana, huwezi kufurahia huduma ya Juan Mata wala Mesut Ozil.
Hawa jamaa ni "Luxury", hawahitaji bugudha, wanahitaji matunzo mazuri kama mabinti wa pwani. Hali ya sasa ya United haimnufaishi sana Juan Mata kwa sababu kocha David Moyes anahitaji namba 10 mwenye uwezo wa kukaba na kusaidia sehemu ya kiungo hususani timu inapokuwa imepoteza mpira.
Kwa mantiki hiyo huwezi kumtumia Mata na kumuweka nje au mahali pengine "baba wa United" Wayne Rooney. Na hili linahitaji mganga?

Unaweza kudhani kuwa Gunners wamekamilika sehemu ya kiungo lakini, wanafanya vizuri sana wanapocheza na timu zinazoanzia nafasi ya 9 kurudi nyuma. Wanapokutana na timu zinazojua kutumia mapungufu yao unaweza kuwahurumia.

Kama Ozil angemkuta Alex Song na Aaron Ramsey huyu wa msimu huu Gunners wangekuwa mbali sana.
Ingawa ni lazima nisema pia kukosa mshambuliaji makini kunaiumiza Arsenal. Arsenal imekuwa timu ambayo ikipigwa shavu la kulia wanageuza na la kushoto! 

Juan Mata anahitaji kucheza mbele ya viungo bora, natamani kama angemkuta Michael Carrick yule aliyekuwa anakaribiana na Xavi Hernandez kwa idadi ya pasi. Natamani kama angecheza na Giggs yule mzee wa "kijiko" kwa guu lake la kushoto, lakini ndiyo hivyo tena labda tumpeleke kwa mganga. Nadhani kutakuwa na mtu anampiga "misumari" pale Old Trafford. Si ndiyo jamani? Maana hii ndiyo akili yetu, bado hatujui tofauti ya kifo na usingizi.

Kuna muda nabaki nacheka tu. Mtoto akipata "division five" naye karogwa mawazo ya kiganga na ushirikina yanaendelea kutuweka mbali na uhalisia. Kuna uwezekano mkubwa sana hata wale wang'oa viti pale uwanja wa taifa,nao watakuwa wamerogwa. Kila timu inapofungwa hapa kwetu utasikia habari za kutoa rushwa, kuna watu wanahujumu, uchawi na nyingine zinazofanana na hizi.
Hata siku moja huwezi kumsikia kocha au benchi la ufundi likitoa sababu za ndani ya uwanja. Tumerogwa?

Kwa chochote kile unaweza kunipata kwa +255789-784858 au unaweza kunitafuta kwenye ukura wa facebook kwa jina la Oscar Oscar Jr na pia,napatikana twitter kwa jina la "soka stadium"

No comments:

Post a Comment