Na Baraka Mbolembole
Mtibwa Sugar itaikaribisha timu ya Simba SC katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali jioni ya leo katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo ilimalizika kwa timu ya Simba kuichapa Mtibwa kwa mabao 2-0. Ila, Mtibwa wanajivunia rekodi yao nzuri ya kuifunga Simba katika mchezo wa mwisho kupigwa katika uwanja huo. Novemba mwaka, 2012 Mtibwa iliichapa Simba kwa mabao 2-0.
MECHI YA LEO.....
Wenyeji, Mtibwa wapo katika nafasi ya tano ya msimamo, wakiwa nyuma kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya Simba walio katika nafasi ya nne na pointi zao 30. Endapo Simba watapata ushindi katika mchezo huo wataruka hadi nafasi ya tatu na kuishusha Mbeya City. Mtibwa imekuwa na matokeo yasiyoridhisha tangu kuanza kwa duru la pili, wamefungwa mechi moja, na Azam FC, na wakatoa suluhu-tasa na Kagera Sugar katika michezo yao miwili ya mwanzo ambayo yote walicheza ugenini.
Simba kwa upande wao wanafikiria namna ya kukusanya pointi zote tatu ili kufuta gepu la pointi sita dhidi ya vinara Azam. Wameshinda michezo yote miwili ya mwanzo katika duru hili, huku wakifunga mabao matano katika michezo dhidi ya timu za Rhino Rangers na JKT Oljoro katika uwanja wa Taifa.
MAKOCHA......
Mecky Mexime, kocha huyu wa Mtibwa atakuwa akiifunza timu yake katika mchezo wa nne wa ligi kuu dhidi ya timu ya Simba. Aliifunga mara zote mbili msimu uliopita, na amepoteza mara moja msimu huu. Kwa upande wa kocha Z. Logarusic yeye atakuwa anaiongoza Simba katika mchezo wake wa kwanza akiwa ugenini, baada ya ushindi mara mbili mfululizo akiwa Dar es Salaam, Logarusic atakuwa na kazi kubwa ya kufuta matokeo mabaya ya Simba katika uwanja wa Jamhuri katika miaka ya karibuni Simba imekuwa ' nyanya' kila inapotia mguu katika uwanja huo.
PRESHA......
Mtibwa itakwenda kucheza na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya wikiendi ijayo, wakati Simba itakuwa inakwenda mjini Tanga kucheza na timu iliyo mkiani, Mgambo JKT, wikendi ijayo. Hivyo ratiba hiyo inaweza kuwafanya wachezaji, mashabiki, makocha na viongozi wa klabu hizo kuwa na wasiwasi wa kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea endapo watapoteza mchezo huo. Mtibwa, mabingwa wa miaka ya 1999, na 2000 wana malengo ya kumaliza nafasi mbili au tatu za juu, wakati Simba ikihitaji kwa udi na uvumba kurudi juu, baada ya kuangukia nafasi ya tatu msimu uliopita.
WACHEZAJI....
Awadh Juma, kiungo huyu amekuwa chachu ya kuamka kwa timu hiyo katika duru la pili. Atakuwa akicheza dhidi ya timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza. Itakuwa ni vita kubwa kati yake na kiungo mzoefu Shaaban Kisiga. Vicent Barnabas, Mussa Mgosi, Salvatory Ntebe, Dixon Daud, Hussein Sharriff ' Cassilas', Abdallah Juma, Juma Luizio, nahodha, Shaaban Nditti ni baadhi ya wachezaji muhimu wa timu ya Mtibwa.
Kwa, upande wa Simba pamoja na Awadh, timu hiyo inajivunia kuwa na wachezaji wenye kutoa mchango mkubwa, Amis Tambwe, mshambuliaji huyu mwenye mabao 13 hadi sasa, tayari amefunga ' hat'trick' mara mbili msimu huu, huku mara ya mwisho akifanya hivyo jumamosi iliyopita wakati timu yake ikishinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Oljoro siku ya jumasosi iliyopita. Tambwe alifunga mabao yote mawili katika mchezo wa kwanza uliowakutanisha timu hizo. Jonas Mkude alifunga bao lake la nne kwa msimu huu wikendi iliyopita, ni kiungo ambaye anaweza kugeuza matokeo kwa upigaji wake wa mashuti ya mbali. William Lucian, Issa Rashid, Joseph Owino, Donald Musoti, Mkude, Ramadhani Singano, Awadh, Tambwe, na kipa Ivo Mapunda, nyota hawa wote hawakuwepo katika mchezo wa msimu uliopita ila sasa ndiyo wanaotegemewa kuvunja uteja katika uwanja huo.
MSHINDI...
Tofauti ya mbinu na ufundi ndiyo huamua matokeo katika ya timu bora na timu nyingine. Kocha wa Simba tayari amesema ni moja ya michezo migumu kwa kikosi chake, ila wamejiandaa kwa ushindi. Mtibwa imekuwa imekuwa na matokeo mabaya kwa kuwa washambuliaji wake wamekuwa wakikosa shabaha, ila ni timu imara katika maeneo ya katikati ya uwanja na wana safu ngumu ya ulinzi.
Simba imeshacheza michezo miwili, na wamefanikiwa kufunga mabao matano huku safu yao ya ulinzi ikiwa ngangari na kutoruhusu bao lolote hadi sasa. Kujiamini kupitiliza wanaweza kujikuta wakiadhibiwa na washambuliaji Luizio na Abdallah Juma ambao kwa pamoja wamefunga mabao 13. Luizio amefunga mabao nane wakati mshambuliaji wa zamani wa Simba, Juma akiwa tayari amrfunga mabao matano. Ni vigumu kubashiri mshindi katika mchezo huu kwa kuwa rekodi imekuwa ni nzuri zaidi kwa Mtibwa kuliko Simba ndani ya uwanja wa Jamhuri, ila Simba ya sasa imeonekana kuwa na makali hivyo wanaweza kushinda na kuwaduwaza wengi. Endelea kufuatia mtandao huu kwa habari zaidi kuelekea mchezo huu wa jioni ya leo.....
No comments:
Post a Comment