Search This Blog

Thursday, November 7, 2013

SHERIA YA 11 KWENYE MCHEZO WA SOKA- KUOTEA.



Sheria ya kumi na moja inazungumzia kuotea. Sheria hii ni sheria fupi kuliko sheria zote miongoni mwa sheria 17 za mpira wa miguu.

Hata hivyo sheria hii ni moja kati ya sheria inayotafsiriwa vibaya na
·       Waamuzi
·       Wachezaji
·       Watazamaji
·       Viongozi n.k
Pia sheria hii imeweza kutoa matokeo mabaya kwa baadhi ya timu kwenye mashindano mbalimbali kutokana na kutafsiriwa vibaya kama sheria na kutolewa maamuzi mabaya yaliyofanywa na waamuzi wasaidizi na waamuzi.

Misingi ya uelewa wa sheria.
NAFASI YA KUOTEA. Tunapozungumzia nafasi ya kuotea tunaangalia vitu vitatu yaani:
1. Mshambuliaji
2. Mpira,
3. Na Mlinzi.
KUJIHUSISHA NA MCHEZO.    
1.      Kujihusisha na mchezo
2.     Eneo ambalo mchezo unachezwa
        -       Kwa Kuingilia mchezo
        -       Kwa Kumuingilia mpinzani
-       Kwa Kupata faida baada ya kuwepo kwenye nafasi ya kuotea.      

Tafsiri ya sheria hii inasema ya kwamba, Sio kosa kwa mchezaji kuwepo katika nafasi ya kuotea; na mchezaji atakuwa kwenye nafasi ya kuotea endapo atakuwa karibu zaidi na mstari wa goli la timu pinzani kuliko VYOTE yaani Mpira na Mpinzani wa pili wa mwisho.

Mchezaji atakuwa hayupo katika nafasi ya kuotea endapo;
·       Atakuwa amesimama kwenye nusu yake ya kiwanja cha mchezo
·       Atakuwa amesimama sambamba na mpinzani wa pili wa mwisho.
·       Atakuwa amesimama sambamba na wapinzani wawili wa mwisho.

KOSA LA KUOTEA.
Mchezaji aliyesimama kwenye nafasi ya kuotea ataadhibiwa kwa kosa la kuotea endapo wakati mpira umechezwa au kuguswa na mchezaji wa timu yake, mchezaji huyo kwa maoni ya mwamuzi atajihusisha kucheza kwa:
·       Kuingilia mchezo
·       Kumuingilia mpinzani
·       Kupata faida baada ya kuwepo kwenye nafasi ya kuotea.
       
SIO KOSA.
Sio kosa endapo mchezaji atapokea mpira moja kwa moja kutokana na:
·       pigo la Goli
·       pigo la Kona
·       Au Mpira wa kurusha

MAKOSA NA ADHABU.
Endapo mchezaji atapatikana na kosa la kuotea, mwamuzi atatoa pigo la adhabu ndogo kwa timu pinzani pigo
litakalopigwa kuelekea kwa timu ya mchezaji aliyeotea na pigo hilo litapigwa kutoka mahali ambapo kosa limefanyika kwa kufuata misingi ya sheria iliyoelezewa kwenye sheria ya Kumi na Tatu.

Endapo kwa makusudi mchezaji wa timu inayozuia anatoka nje ya kiwanja cha mchezo bila ya ruhusa ya mwamuzi ili kumfanya mchezaji anayeshambulia kuwa katika nafasi ya kuotea, mchezaji huyo atahesabika kuwa amesimama kwenye mstari wa goli la timu yake au mstari wa pembeni ya kiwanja kwa suala la kuotea, mpaka mpira utakapokuwa haupo mchezoni. Kama mchezaji ametoka nje ya kiwanja cha mchezo kwa makusudi, ataonywa mara mpira utakapokuwa haupo mchezoni.

Sio kosa endapo mchezaji aliye kwenye nafasi ya kuotea atatoka nje ya kiwanja cha mchezo ili kumuonyesha mwamuzi kwamba hataki kujihusisha na mchezo. Hata hivyo, endapo mwamuzi atachukulia ya kwamba mchezaji ametoka nje ya kiwanja cha mchezo ili kuleta ujanja na kujipatia faida kwa kuingia tena ndani ya kiwanja cha mchezo, mchezaji huyo ataonywa kwa kosa la kutoonyesha tabia ya uanamichezo.

Endapo mchezaji wa timu inayoshambulia atasimama bila ya kujitingisha katikati ya milingoti ya goli na ndani ya nyavu za goli wakati mpira unaingia golini, goli litakuwa halali. Hata hivyo kama mchezaji huyo atamuingilia mpinzani, goli halitakuwa halali, mchezaji huyo ataonywa kwa kosa la tabia isiyokuwa ya kiungwana na mchezo utaanza tena kwa kudondoshwa kutoka mahali mpira ulipokuwa kabla ya kusimamishwa, labda kama mpira ulisimamishwa ndani ya eneo la goli ambapo Mwamuzi ataudondosha mpira juu ya msitari wa eneo la goli sambamba na mstari wa goli karibu kabisa na mahali ambapo mpira ulikuwa kabla haujasimamishwa.


Imefasiriwa na

Leslie L. Liunda
KATIBU,
KAMATI YA WAAMUZI TFF/MKUFUNZI WA WAAMUZI




                         

No comments:

Post a Comment