Boniface Wambura ( kushoto ) na Angetileh Osiah ( Kulia )
MUDA mfupi tu baada ya kukabidhiwa ofisi na uongozi unaoondoka madarakani, Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa kushirikiana na kamati ya utendaji, alimvua madaraka aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Malinzi kuiambia kamati hiyo kwamba, hana imani na Angetile, na kamati haikuwa na pingamizi na ombi hilo la Malinzi likapita huku maombi mengine ya kupunguzwa au kuondolewa kwa wafanyakazi wengine yakiendelea kujadiliwa.
Angetile kwa mujibu wa mkataba wake, Desemba mwaka huu ndiyo kipindi ambacho mkataba wake unaisha na kamati ya utendaji imempa likizo ya malipo hadi mkataba wake utakapoisha mwezi ujao.
Baada ya kumtoa Angetile, kamati ya utendaji ikamteua Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kuwa kaimu katibu mkuu wakati mchakato wa kumpata katibu mpya ukiendelea.
Uamuzi huu wa uongozi mpya wa TFF umechukuliwa kwa sura mbili tofauti, MOJA inayokubaliana na mabadiliko hayo na PILI ni upande unaoona kisasi kimetumika katika kumuondoa Angetile kwenye nafasi yake.
Siku zinaenda kwa kasi sana kuliko inavyotegemewa, lakini kuna matukio kadhaa yaliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF na zile chaguzi za mikoa ambazo ziligubikwa na mizengwe mingi.
Lakini tusizungumzie mizengwe ya chaguzi za mikoani, tuangalie uchaguzi mkuu wa TFF na ushiriki wa Angetile kama katibu mkuu wa chombo hicho. Hakuna kificho kwamba alikuwa akienda tofauti na baadhi ya wakimbizi kama Malinzi na wengine ambao walionekana kuwa kambi ya mgombea huyo wa nafasi ya U-rais.
HAKUSIMAMA KATIKA NAFASI YAKE
Muda mwingi Angetile pengine alikuwa anajisahau kuhusu nafasi yake au alikuwa akifanya kwa makusudi, hasa suala la kuonekana yupo tofauti na mtandao wa Malinzi.
Kama katibu mkuu wa TFF, hakupaswa kuegemea upande mmoja wa mgombea hata kama alikuwemo tayari katika mfumo wa kiutawala. Angetile alionyesha wazi kwamba yupo upande wa aliyekuwa mgombea mwingine wa nafasi ya U-rais, Athuman Nyamlani ambaye alikuwa makamu wa rais wa TFF.
Tazama kitu kimoja, hata kama rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga alikuwa anamuunga mkono Nyamlani, lakini hakuna aliyemuona hadharani ama akifanya kampeni ya vitendo au maneno au kukandamiza kambi ya Malinzi.
Hakuna asiyefahamu falsafa ya Tenga ilivyokuwa juu ya uchaguzi huu, ndiyo maana hakuweka kauzibe kuhusu kufanywa kwa mapitio upya kuhusu uamuzi wa kamati za TFF wakati zinawaengua baadhi ya wagombea.
Tazama Angetile alivyohusika katika kukata rufaa kwa baadhi ya wagombea kuhusu kupitishwa kwao kuwania uongozi ndani ya TFF. Kama katibu mkuu, Angetile hakupaswa kujiingiza katika mambo kama haya.
Kuna msemo unaotawala sana katika jamii kwamba, hakuna mwenye uhakika kama Mungu yupo lakini wote tunaamini hicho kitu. Ndiyo maana watu wanaabudu kwa kila mtu na imani yake, wote tukiamini kwenda peponi, lakini hakuna mwenye uhakika kama Mungu yupo, sasa ni bora ukaamini Mungu yupo na kumuabudu lakini ikitokea Mungu hayupo hauwezi kudhurika kama ukiamini kutokuwepo kwake.
Sasa Angetile aliamini Mungu hayupo na sasa amekutana naye, unadhani kipi kitakachofanywa na Mungu? Ndicho kilichotokea.
Kama si nusu, basi robo ya wajumbe wa kamati ya utendaji ni wajeruhiwa wa vitendo vya Angetile huku akiwa na kofia ya katibu mkuu. Wasingeweza kumuacha.
APINGANA NA SERIKALI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo ndiyo inayoisimamia TFF, ndiyo maana wakati fulani serikali ilijitolea kumleta na kumlipa kocha Marcio Maximo ili aifundishe Taifa Stars.
Wakati uchaguzi wa TFF ukishika kasi, Angetile alipingana na naibu waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo, Mh. Amos Makalla, kuhusiana na taratibu za uchaguzi huo hasa baada ya Malinzi kuenguliwa kisha kupeleka malalamiko wizarani.
Makalla ndiye aliyekabidhiwa kushughulikiwa jambo hilo na waziri anayehusika na michezo, lakini kila alilokuwa akiagiza Angetile hakuwa mtiifu kwake huku akidai anayeweza kuzungumza naye ni waziri kamili.
Kama inavyofahamika kwamba, Makalla na waziri husika wa wizara hiyo, wote wameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushughulikia michezo. Sasa unapomkataa mteule wa rais, hapo ina maana hauheshimu maamuzi ya mteuaji ambaye ni rais.
Katika hali kama hiyo, hata ukitoa fikra za kisasi, bado serikali haiwezi kuwa tayari kufanya kazi na mtu ambaye hana utii kwa wafanyakazi wake. Hili lilikuwa tatizo ambalo Angetile hakuweza kulisoma haraka na kufahamu athari zake.
Kama una kumbukumbu nzuri, wakati Tenga anaingia madarakani Desemba 2004, hakuwa na nguvu sana katika medani ya soka kulinganisha na aliyekuwa mgombea mwenzake, Muhidin Ndolanga, lakini Tenga alishinda.
Tenga alishinda kutokana na ‘nchi’ kutaka mabadiliko katika soka na serikali ilikuwa ya kwanza kupongeza ushindi huo wa Tenga na wajumbe walipongezwa juu ya hilo.
Hii ina maana kwamba, hata kama Nyamlani angeshinda nafasi ya U-rais, bado serikali isingekuwa tayari kuona inafanya kazi na katibu anayebishana na naibu waziri huku akimuona mtu mdogo.
KWA NINI ANGETILE NA SIYO WAMBURA
Malinzi na kamati yake ya utendaji baada ya kujiridhisha na utendaji wa Wambura hasa uhusiano wake ulivyo na waandishi wa habari, haraka wakamteua kukaimu nafasi ya katibu mkuu.
Wambura alikuwepo wakati mchakato wa uchaguzi ukifanyika lakini alijitahidi kutokuwa na upande japokuwa alikuwa akitumwa katika mambo mbalimbali kwa mujibu wa kazi yake.
Katika vikao mbalimbali vya kamati za uchaguzi na ile ya maadili, Wambura alikuwa akiiwakilisha TFF ipasavyo, kwa mfano katika mapingamizi mbalimbali waliyowekewa wagombea yeye alikuwa anafanya kazi ya kupeleka mapingamizi waliyokuwa wakiyapokea kutoka kwa wadau wa michezo na siyo yeye mwenyewe kuwa mstari wa mbele katika kuandika.
Malinzi na wenzake wangeweza hata kumpa kazi mtu mwingine kutoka nje ya TFF ili awe katibu mkuu, lakini kwa kutambua ufanisi wa Wambura na kutoendekeza kisasi, ndiyo maana Wambura akapewa nafasi ya Angetile kwa muda.
No comments:
Post a Comment