Jina langu ni Francis Boniface Cheka, mimi ni mshabiki
wa Liverpool.
Swali: Lini ulianza kuishabikia Liverpool?
Cheka: Nakumbuka nilianza kuipenda Liverpool mwaka
2002 na kipindi hicho ni mchezaji
Michael Owen ndiye aliyenihamasisha kwa jinsi alivyokuwa anafunga.
Swali: Ni siku gani uliyofurahi kuliko zote kama
mshabiki wa Liverpool?
Cheka: Siku niliyofurahi kuliko siku zote nikiwa
mshabiki wa Liverpool ilikuwa ni mwaka 2005 wakati liverpool ilipochukua klabu
bingwa ya Ulaya kwa kuifunga AC Milan.
Swali: Unafikiri matatizo yanayoikumba Liverpool kwa
sasa yamesababishwa na nini?
Cheka: Matatizo kwenye timu yanatokea pale ambapo watu
wanakuwa hawatimizi wajibu wao kwenye timu, nadhani hilo ndio linaloikuta
Liverpool kwa sasa, pia kuna baadhi ya wachezaji ambao hawatimizi wajibu wao
nafikiri hayo ndio yanayoiathiri timu.
Swali: Na je ni nini kinapaswa kufanywa ili kuinusuru
timu yako?
Cheka: Nadhani wachezaji wanapaswa kuwa na juhudi za
dhati za kuiokoa timu kwa kuwa nadhani wao ndio wenye wajibu na uwezo mkubwa wa
kufanya hivyo. Kocha atafanya kazi yake atafundisha atamaliza asilimia
inayobaki ni kwa wachezaji.
Swali: Na hapa
nyumbani wewe ni shabiki wa timu gani?
Cheka: Hapa mimi nashabikia Simba lakini baba yangu
mzazi Mzee Cheka ni Yanga damu nakumbuka kuna siku Simba iliifunga Yanga bao
nne mzee alinichapa baada ya kumcheka na timu yake.
Swali: Je, kuna uhusiano wowote na upenzi wako kwa
Simba na bukta za rangi nyekundu na nyeupe unazovaa ukiwa ulingoni?
Cheka: Hapana, unajua mimi nampenda sana Mohamed Ali
na yeye ndio alinivutia mpaka mimi kuvaa kama yeye, kwani nilidhani kuwa ili
bondia apigane vyema kama Mohamed Ali ni lazima avae kama yeye.
Swali: Wakati unacheza soka ulikuwa ukicheza nafasi
ipi na uliwahi kucheza timu gani?
Cheka: Mimi
nilikuwa golikipa, nimeshacheza timu kama FC Nondo, Shoka FC, Care Boys
na nyingine ya Msumbiji ya Sportive De Moeda pamoja na Kilimani Benfica ambayo
ilikuwa ligi daraja la nne Msumbiji. Nakumbuka wakati nadakia Care Boys kuna
mchezaji mmoja Marehemu James Shawa aliwahi kunitegua kidole kwa shuti lake.
Swali: Baada ya kuumia kwenye soka ndio ukaamua
kuingia kwenye ndondi au?
Cheka: Hapana, niliingia kwenye ndondi kwa kuwa
nilikosa nafasi kwenye soka, nakumbuka baba yangu aliwahi kunipeleka Yanga
mwaka 1997 wakati huo usajili ulikuwa wazi kwa watu wote, aliponipeleka
nilikataliwa na ndio ikabidi anipeleke kwenye ndondi.
Swali: Ni wachezaji gani watatu ambao siku zote wako
kichwani mwako?
Cheka: Nizar Khalfan, Juma Kasseja na Mussa Hassan
Mgossi na kwa Liverpool ni Steven Gerald.
No comments:
Post a Comment