Search This Blog

Thursday, November 14, 2013

ADRIAN MUTU NI KIPAJI KILICHOPOTEA



Kununuliwa kwa Chelsea na tajiri Roman Abromovoch kulimaanisha wachezaji nyota kama Adrian Mutu walikuwa na kila nafasi ya kupewa shavu katika kikosi kazi cha Jose Mourihno. Kipaji cha Adrian Mutu kilianza kung’ara pindi tu aliposajiliwa na Chelsea, pamoja na ukweli kwamba alikuwa amepita katika vilabu vikongwe barani Ulaya kama Inter Milan na Parma, lakini kutua kwake Stamford Brigde kulimaanisha kuwa safari ya kuelekea kwenye mafanikio kwa Mutu ilianza kuonekana waziwazi.
Kama ambavyo tumekuwa tukiona katika sehemu hii ya vipaji vilivyopotea, wachezaji wengi, wamekuwa wakipotezwa na soka lao na mambo nje ya uwanja, iwe ni wanawake, pombe au hata kuumia. Mutu, hayuko mbali sana hayo yote, skendo yake ya ‘kuchovya’, yaani kutumia madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa kimeifanya dunia kuanza kumsahau Mutu kama straika hatari bali kama Mutu teja la kutupwa. Na katika dunia ya sasa ambayo soka ni biashara basi kumekuwa na kila sababu ya mameneja kuanza kumuona Mutu kama Bundi katika vyumba vya kubadili nguo vya klabu zao.
Akiwa na Mourihno
Mnamo mwezi Agosti, 2003, Chelsea waliridhia kumwaga kitita cha paundi milioni 15.8 kwa ajili ya usajili wa Mutu akitokea Parma. Kwa mechi nne za awali ilidhihirisha kuwa Roman hakutupa pesa yake bure, alitupia bao tatu, huku akipiga bao mbili katika mechi dhidi ya wapinzani wao wakuu wa jijini London, Tottenham Hotspurs katika ushindi wa 4-2. Lakini hadi msimu unaisha alikuwa na mabao sita tu kati ya mechi 27 alizocheza.
Anaharibu akiwa Chelsea
Alianza kwa kugombana na kocha wake Mourihno juu ya ukweli kwamba yeye (Mutu), kudai kuumia katika mechi ya timu yake ya Taifa dhiidi ya Czech, mechi ya kufuzu kucheza kombe la dunia. Lakini, kama vile haitoshi, Septemba ya mwaka huohuo ilibainika kwamba Mutu amekuwa akitumia madawa aina ya Cocaine hivyo kufungiwa kucheza soka kwa miezi 7 na chama cha soka Uingereza huku pia akipigwa na faini ya paundi 20,000 na chama cha soka.
Chelsea wanadai chao
Kuvunjika kwa mkataba kati yake na Chelsea kulimaanisha kuwa Mutu amevunja kwa makusudi kipengele ndani ya mkataba wake aliongia nao, hivyo kumaanisha kuwa anapaswa kuilipa faini klabu yake ya Chelsea, kesi yake pamoja na kuamuriwa kuwa Mutu ailipe klabu yake hiyo ya zamani (Chelsea), jumla ya paundi milioni 17, lakini, Mutu bado amekuwa mgumu kuweza kutoa hata thumuni, na mara ya mwisho, kamati ya usuluhishi ya FIFA; na  endapo hatolipa basi FIFA inayo idhini ya kumfungia kucheza soka maisha. Mutu, bado hajakata tamaa, safari hii amekata rufaa katika mahakama ya  haki ya Ulaya.

Hajifunzi tu kutokana na makosa
Mutu alikumbwa na skendo nyingine ya kumvunja pua mhudumu wa baa, mara baada ya kutokea kutoelewana kati yao. Lakini hiyo ilikuja mara baada ya Mutu kushindwa tena vipimo vya afya, na hivyo kufungiwa mwaka mmoja kucheza soka kabla ya adhabu yake kupunguzwa hadi kuwa miezi sita. Goli lake la kwanza kutoka kifungoni lilikuwa ni dhidi ya Cagliari, ambako timu yake ilipata ushindi mwembamba wa bao moja kwa bila, na mara baada ya mechi anakiri, ‘Leo ni siku yangu ya furaha kupita zote mwaka huu 2010, nawashukuru wapenzi wangu walionisapoti katika kipindi nikiwa kifungoni na mara baada ya kumaliza kifungo’ alisema streka huyo.
Tayari akiwa na  miaka 34, Mutu, bila shaka tusitegemee jipya toka kwake, kipindi alipokuwa na umri wa kucheza katika ‘peak’ ni kipindi alipokuwa anahangaika katika mahakama za rufani kupinga faini aliyopigwa, tayari, makocha wa vilabu vikubwa Ulaya wameshaona kuwa kumsajili Mutu ni sawa na kununua mbuzi kwenye gunia, unaweza kumsajili leo, halafu mwezi tu anafeli vipimo na hivyo kufungiwa mwaka kucheza soka. Hiyo ni hasara kwa klabu na kwa mashabiki wake. Kwaheri Mutu, Dunia ya soka itakukumbuka zaidi kwa muda uliokaa jela za soka kuliko dakika za maajabu ndani ya dimba.

No comments:

Post a Comment