Search This Blog

Thursday, November 14, 2013

BAADA YA KUMSAJILI KASEJA, NAFASI YA LIBERO TATIZO YANGA


Na Baraka Mbolembole

Yanga ilimsajili mlinda mlango, Juma Kaseja kama mchezaji huru wiki iliyopita. Kipa huyo mzoefu na mahiri nchini amejiunga na Yanga kwa mara nyingine kwa mkataba wa miaka miwili. Ikiwa katika maboresho ya kikosi chake kilichomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga wanalenga pia walau nafasi ya kucheza michuano ya Ligi yamabingwa Afrika, hatua ya nane bora, nafasi ambayo walifikia kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1998.

Usajili wa Kaseja ni sehemu ya kuongezea ubora idara ya golikipa, ambayo sasa itakuwa na makipa, Ally Mustafa, Deogratius Munishi 'Dida' na Kaseja.

SAFU YA ULINZI WA KATI
Nadir Haroub na patna wake katika safu ya beki wa kati ya Yanga ni walinzi ambao wakati wanapokabiliana na washambuliaji wasumbufu huishia kupoteza mawasiliano yao uwanjani. Kwa muda mrefu sasa walinzi hao wameonekana kufanya vizuri katika soka la ndani.

Wamejenga uhusiano mzuri sana uwanjani, na wamekuwa wakicheza kwa maelewano, lakini katika mchezo wa soka mchezaji unatakiwa kupiga hatua mbele na si kurudi nyuma. Uimara wa beki kama safu muhimu kwenye timu ni moja kati ya sifa muhimu kwa michuano ya kimataifa.
 Yanga ambao wamewekeza akili yao katika michuano hiyo wanatakiwa kuongeza pia mlinzi mahiri wa nafasi ya kati ambayo imekuwa ikionesha udhaifu hasa katika michezo muhimu ya klabu. Kelvin Yondan ni mlinzi ' ngangari' kama ilivyo kwa Nadir, ila hawa wote si walinzi ambao wanaweza kucheza pamoja. Wote ni wakabaji wazuri kwa mtindo wa 'Man to Man'. Ila katika mifumo mingi ya kileo, huwa wanashindwa kufanya vizuri wanapokutana na washambuliaji wasumbufu, ambao hucheza kwa mtindo wa kuhama hama nafasi.

WALITESWA NA AZAM WAKAONESHA UDHAIFU MKUBWA DHIDI YA SIMBA
Ukitoa mabao 11 waliyofungwa Yanga katika michezo 13 ya duru la kwanza katika ligi kuu. Walinzi hao walisumbuliwa mno na safu ya mashambulizi ya Azam FC, katika mchezo waliopoteza kwa mabao 3-2. Yanga wanahitaji mchezaji ambaye anaweza kuwaongoza wenzake uwanjani huku akiusoma mchezo. 
Ukitazama kikosi chao kwa sasa, akihitaji kufanyiwa marekebisho mengi, idara nyingine zimekuwa zikifanya kazi nzuri, ingawa jukumu la ulinzi ni la timu nzima, safu ya ulinzi inatakiwa kuwa na mchezaji ambaye ana uwezo wa kusimama na kuzuia vizuri. 

Walifungwa na Azam kwa mtindo wa counter attack, na wakafungwa mabao mawili ya vichwa na Simba. Hili linaweza lisionekane sana kama ni tatizo kwa kuwa katika soka la ndani bado wachezaji wetu wengi si mahiri wa kutumia mipira ya counter, kona na faulo. 
Ila unapokwenda kucheza michuano kama ya klabu bingwa ni wazi hali hii inaweza kuwaondoa mapema.
Wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa yao wenyewe huku wakitambua kuwa michuano ya kimataifa, si muhimu kwao tu
bali pia kwa maendeleo ya soka la Tanzania. Mwaka 2011, Simba waliweza kufikia hatua ya 16 bora, na waliadhibiwa na Wydad Casablanca kutokana na udhaifu wa safu yao ya ulinzi, jambo Kaseja alikuwepo umakini mdogo wa safu ya ulinzi katika dakika tatu tu za mwisho ukawanyima nafasi ya kufikia hatua ya mikwaju ya penati. 2012, kwa mara nyingine Simba ilifanikiwa kufikia hatua ya 16 bora ya michuano ya Afrika na kutolewa
na Shandy ya Sudan, kwa mikwaju ya penati baada ya kushindwa kulinda ushindi wa mabao 3-0 walioupata katika mchezo wa kwanza.
Azam wao walitolewa kutokana sababu kama hizo, ila hawakuathirika sana kutokana na udhaifu wa safu ya ulinzi, bali matatizo ya kiuzoefu, ambayo yalichangiwa na umakini wao mdogo. 
Kufanya vizuri mara kwa mara kwa klabu zetu inaweza kutufungulia ' kufuri' na siku moja nasi tukawa tunatoa wawakilishi wawili kwa kila michuano ya CAF. Naisubiri Yanga
chini ya uenyekiti wa Yusuph Manji katika michuano ya Afrika hapo mwakani. Muda wa kuimarisha timu ni huu. 
Wakati huu safu ya utawala ikijipanga vizuri, nitapenda kuona safu ya ulinzi ikiwa na mlinzi mwenye sifa kama za Rio Ferdinand au Per Mertersacker. Kwenye fullbacks hakuna tatizo kubwa zaidi ya yale ya kiufundi tu kama uzuiaji wa krosi.

1 comment:

  1. Kaka Nakubaliana na maoni haya, Tatizo walinzi wa kama Lucio au Rio Fed hawapo nchini. kwa hivi sasa. Wazo Langu ni kumbadilisha Kiungo Mkabaji mwenye umbo kubwa acheze nafasi hiyo. Ila kwa kuwa vilabu vyetu havipendi kuwekeza, basi utaona vinataka kwenda sokoni. Wanaweza kumbadilisha yule dogo aliyetoka Mtibwa na wakampa mechi na majukumu hayo kidogo kidogo tungeona mabadiliko.


    ReplyDelete