Search This Blog
Wednesday, July 3, 2013
MAKALA: YALIYOMKUTA KASEJA KWA SIMBA - LIWE SOMO KWA WACHEZAJI WENGINE NA MFUMO WA USAJILI NA MIKATABA
NA MWESIGWA J CELESTINE.
Kuachwa kwa Juma Kaseja na klabu yake ya zamani, Simba, kumetawala vichwa vya habari takribani kwa wiki nzima sasa.
Mimi ni miongoni mwa watu walioshangazwa na Juma kuachwa ilihali akiwa 'anadai'. Lawama nyingi sana zimekwenda kwa viongozi wa Simba na Klabu kwa ujumla kana kwamba Juma aliumbwa kucheza Simba milele. Yawezekana zengwe la viongozi lilikuwepo, hatuna hakika.
Yaliyomtokea Juma ni changamoto kwa wachezaji,vilabu na mfumo mzima wa soka la Tanzania. Najiuliza iwapo Juma ingekataa kusaini Simba ingekuwaje?Hakika mashabiki wangekuja juu na kumuona kama msaliti.
Na siku zote iko hivyo kwa sababu mashabiki hawapati undani na hadidu rejea za mikataba ya wachezaji. Inashangaza kwamba tumekuwa tunajadili suala la Kaseja ambaye mkataba wake ulishakwisha. Kama kweli Simba wangekuwa wanamuhitaji wangempa mkataba mwaka mmoja uliopita au angalau miezi 6 iliyopita. Chini ya hapo kambi ya Kaseja ilipaswa kuwa imeweka tahadhari kwa lolote litakalotokea. Hata kwa mashabiki hawakupaswa kuhoji sasa hivi, walipaswa kuhoji miezi kadhaa iliyopita.
Tanzania ina mtindo wa aina yake ambapo wachezaji hupewa mkataba na klabu yao ya zamani wakiwa wameshakuwa na hadhi (status) ya wachezaji huru. Hali hii inasababisha wachezaji kukesha wakiota hatima yao wakati ligi inafikia patamu (inaelekea ukingoni). Ligi inakwisha utaona wenyeviti wa kamati za usajili (vilabu vyetu vingi havitumii makocha au wakurugenzi wa ufundi katika usajili) wanahangaika kuwatafuta akina Kiemba, Niyonzima,Kaseja, Nizar na wengineo kwa ajili ya kuwasainisha mikataba mipya.
Katika mfumo wa namna hii,vilabu vinakuwa na nguvu katika kuamua hatima ya wachezaji. Mtu anaachwa kwenye suspense mpaka dakika ya mwisho wakati hana chaguo B. Kujikwamua na hili ni muhimu/lazima kwa wachezaji kuwa na washauri wao kama mameneja, mawakala, washauri wa kibiashara, ndugu, au makampuni wakilishi. Hali ya wachezaji kukaa mezani kujadiliana na mfanyabiashara kama Hans Poppe au Abdallah inajenga mazingira ya mchezaji kutia sahihi asichokifahamu kwa ufasaha. Kwa maana nyingine mfumo huu una faida kwa vilabu na viongozi wao kuliko wachezaji na hata makocha wanaoajiriwa na vilabu.
Ni imani yangu, kama wachezaji watakuwa na wawakilishi na washauri katika kucheza mpira, wataweza kufika mbali na kujiondolea msongo wa kuamkia nyumbani kwa viongozi kuomba pesa za usajili. Ndio maana hadithi za mchezaji kaugua, katelekezwa, kashindwa kulipia kodi ya nyumba zinakuwa nyingi kwa sababu kazi ya mchezaji imekuwa ni kusaini kwenye mkataba na siyo kuuchambua mkataba yeye au mwakilishi wake.
Vilevile ni muhimu kwa wachezaji kujua haki na majukumu yao zaidi ya wanachokifanya uwanjani. Mara kadhaa tumeona mabango ya Kaseja na wengine wanaochezea vilabu vikubwa na timu ya taifa. Ukiwauliza anakwambia hakupewa kitu au alipewa lunch na nauli siku ya kushoot. Hajui kwenye mkataba wake hii haki inamilikiwa na yeye, klabu au timu ya taifa na kwa asilimia ngapi?Bado tuko kwenye enzi ya Jella Mtagwa na stempu za FIFA/World Cup Spain 1982.
Umefika wakati, mchezaji akiona imebaki miezi sita na klabu haijafanya maongezi aanze kuinua macho na kuangalia wapi kwingine kwenye riziki. Mchezaji hawezi kuilazimisha timu kuichezea na wala timu haimlazimishi mchezaji. Wachezaji wakiwa na mtazamo chanya kwa uwezo wao, watacheza kokote bila kuhitaji kubembeleza kucheza Yanga au Simba au kuona kuwa Yanga au Simba ni mwisho wa ndoto bila kujali kama kuna maendeleo ya kipaji au hakuna,kucheza au kukaa benchi. Mpira wetu ni wa kulipwa na mikataba ni ya kulipwa hivyo na wachezaji wanatakiwa wauangalie uhusiano wao na vilabu katika misingi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
mbona mnatetea saana huyu kaseja yeye nani simba, wamepita watu na heshima zao simba hawakuagwa itakuwa yeye? mbona alipoenda yanga hamkushadadia kwenda kkwake yanga. acheni unafiki wenu, wameachwa akina casilas bench itakuwa yeye
ReplyDelete