DAWA za kulevya ni hatari, ni hatari sana. Maisha ya baadhi ya wasanii na
wachezaji yamepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Aidha, dawa za kulevya husababisha baadhi ya wasanii na wachezaji kushindwa
kuendelea na fani zao.
Orodha ya wasanii waliopoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa za
kulevya ni ndefu lakini baadhi yao ni Elvis Presley, Whitney Houston, Brenda
Fassie wa Afrika Kusini.
Tanzania imepata mshtuko kwamba kimeripotiwa kifo cha msanii kutokana na matumizi
ya dawa za kulevya. Tukiwa tunangoja ripoti kamili ya daktari juu ya kifo
chake, msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’, Albert Mangwea ‘Mangwair
au Ngwea’ anadaiwa kufariki kutokana na dawa za kulevya nchini Afrika Kusini mapema
wiki iliyopita.
Habari hizo ziwe kweli au la, Mangwair amefariki na mwili wake ulirejeshwa
nchini juzi kwa mazishi yatakayofanyika leo hii huko Morogoro. Hata hivyo kifo
chake, kitoe changamoto kwa wasanii wengine akiwemo Ray C aliyeko kwenye kituo
cha kujirekebisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
DAWA ZA KULEVYA
Hizi ni dawa ambazo zimepigwa marufuku kutumiwa na jamii kutokana na
kiwango chake cha athari kwa binadamu. Dawa hizi ambazo miongoni mwake ni bangi,
heroin na cocaine, zina athari zaidi katika mwili wa binadamu kuliko faida.
Wasanii wanaotumia dawa za kulevya husukumwa zaidi na tabia ya kuiga ili waweze
kufanya maonyesho jukwaani kwa ukakamavu mkubwa.
Wasanii hawa wanaamini wanapotumia dawa hizo zinawasisimua mwili ili wapate
uwezo wa kutumbuiza jukwaani kwa muda mrefu bila kuchoka tena bila aibu.
Upande wa wanamichezo hasa soka na riadha, msukumo mkubwa upo katika kuwa
na pumzi ya kuweza kucheza soka kwa dakika 90 bila kuchoka na moyo wa ujasiri
hata kwenye riadha hali ni hivyo hivyo.
ATHARI ZA DAWA ZA KULEVYA MICHEZONI
Serikali duniani kote zinapiga marufuku matumizi ya dawa za kulevya. Kwa
bahati mbaya, dawa hizi hutengenezwa, husafirishwa na hutumiwa kwa kificho
japokuwa madhara hujionyesha wazi.
Kwa mujibu wa wataalam, mtu anapotumia dawa za kulevya, moja kwa moja
huathiri baadhi ya viungo vya mwili kinyume cha imani ya watumiaji.
Mtumiaji hupata ganzi na kutoka katika hali ya kawaida. Kutokana na ganzi
hiyo taarifa hutumwa katika ubongo na ubongo nao hutuma vichocheo katika kiungo
hicho na hufanya kazi maradufu.
Jinsi dawa inavyotumiwa kwa wingi ili kurekebisha hali ya ganzi ndivyo
nguvu inavyozidi kutengenezwa na hivyo ndivyo vinavyowamaliza wasanii na
wanamichezo.
Wataalam wanasema matumizi haya ya dawa za kulevya huufanya mwili wa
mtumiaji kuchoka na kukosa hamu ya kula kutokana na seli nyingi mwilini
kushindwa kufanya kazi.
Matokeo yake, mwili wa mtu huyo hudhoofu kwa kukosa chakula na hata uwezo
wa kutengeneza chembechembe hai za kuulinda mwili na kujikinga dhidi ya magonjwa
hupungua, hivyo mwili huruhusu magonjwa ya mara kwa mara.
Hali hii inapotokea uwezo wa msanii au mwanamichezo huonekana umepungua na
muda wowote mahala popote anaweza kuchukua maamuzi anayoyajua yeye.
KITU CHA KUFANYA
Masomo ya dini
za Kikristo na Kiislamu na elimu maalum ya dawa za kulevya yatumike ili
kuwaweka vijana katika misingi mizuri ya maadili na athari za dawa za kulevya.
Hii itasaidia
vijana kufahamu kwa undani faida za dawa zilizoidhinishwa na Serikali na athari
za dawa zilizopigwa marufuku zikiwemo za kulevya ili kupunguza kwa wimbi la
vijana kutumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya.
MAKALA HII
IMETOLEWA KATIKA GAZETI LA MAWIO NA IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI
somo zuri kwetu vijana,si kw wanamichezo pekeyao hata kwetu wanafunzi wa elimu yajuu(vyuo vikuu)tumechukuli kuwa sasa tuko huru kufanya lolote katika utumiaji wa vilevi vya aina yote.tuwe makini jamani tusipishe siku zetu za kuishi kwa vileo hivi!
ReplyDeleteKambili kaandika ukweli mtupu, bila jitihada za kudhibiti tatizo hili tutaendelea kushuhudia vijana wengi wakitoweka...lazima hatua za haraka zichukuliwe kwa maana ya kudhibiti biashara ya unga hata kama ni kazi ngumu kwa vile hazijaanza kuuzwa leo na mtandao wake ni mkubwa kiasi vigumu kuikomesha...
ReplyDeleteWASANII WALIO WENGI WANAJUA MADHARA YAKE NA WANAPENDA KUACHA LKN KWA KUWA MADAWA HAYO YAMEWATAWALA, WANASHINDWA KUACHA. ELIMU JUU ATHARI ZAKE,USHAURI NASAHA PAMOJA NA MBINU ZA KUACHANA NO MADAWA HAYO NDO SULUU YA KUDUMU KUTATUA TATIZO HILO.
ReplyDelete