Na Baraka Mpenja, Dar es Salaam
Wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar, wanaendelea na hesabu zao za kuiwinda nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Akizungumza na mtandao huu, msemaji wa klabu hiyo, Tobias Kifaru Lugalambwike, amesema wanaendelea na mazoezi makali ya kuwawinda vijana wa mitaa ya kishamapanda jijini Mwanza, Toto Africans, mchezo utakaopigwa dimba la Manungu Complex aprili 10 mwaka huu.
“Hivi karibuni tumetoka kucheza na ndugu zetu kule Kaitaba na kufungwa 3-1, sasa tumerejea katika mashamba yetu ya Manungu tukiwasubiri Toto, tunajipanga vilivyo kuhakikisha tunajiweka mazingira mazuri ya kupata angalau nafasi ya tatu au nne ya ligi kuu msimu huu”. Alisema Kifaru.
Kifaru alisema msimu huu kila mchezaji ametambua kuwa soka ni ajira yake na ndio maana ligi imekuwa na changamoto kubwa huku kila timu ikihitaji kupata mafanikio mazuri.
Msemaji huyo aliongeza kuwa wao wamesaliwa na michezo minne ambayo watakutana na daluga za Africa Lyon, Toto Africans, JKT Oljoro, na JKT Ruvu, hivyo wanaijenga timu kuhakikisha wanashinda mitanange yote iliyobakia.
“Mwalimu Meck Mexime anawafua vizuri sana wachezaji wetu, yeye anaelewa matatizo ya timu, kwa hiyo imani yetu ni kuibuka na ushindi dhidi ya vibonde hao wa ligi kuu Toto africans walioko nafsi ya mkiani”. Alijigamba Kifaru.
Akizungumzia hali ya mchezo wenyewe, Kifaru alisema Toto wanapigana kufa na kupona kukwepa mkasi wa kushuka daraja, wao wanahitaji nafasi nzuri katika msimamo, hivyo sura ya mchezo huo inaonekana kuwa ngumu licha ya maandalizi makubwa wanayofanya kwa sasa.
Pia alisisitiza kuwa wao wapo nafasi ya sita katika msimamo, lakini waliopo juu yao yaani Azam fc, Simba, kagera sugar, Coastal union wakikosea hesabu zao basi Mtibwa itapata nafasi nzuri mwishoni mwa msimu.
Kifaru aliwata mashabiki wa klabu hiyo kuondosha mashaka kwani wamejipanga barabara hivyo ni muhimu kwao kufika kwa wingi Manungu Complex wiki ijayo kuishangilia timu hiyo bora nchini Tanzania.
Mbali na mchezo huo wa jumatano ijayo, nao vinara Yanga watavaana na JKT Oljoro uwanja wa taifa, Tanzania Prisons watakuwa nyumbani kwao Sokonne kumenyana na Mgambo JKT, Polisi Moro watakuwa Jamhuri kuvaana na Ruvu Shooting, wagosi wa kaya Coastal unioni watakuwa kwao Mkwakwani kupepetana na JKT Ruvu, na Azam fc baada ya leo kucheza kombe la shirikisho na Barrack Yc ya Liberia watawakaribisha Africa Lyon dimba la chamazi.
No comments:
Post a Comment