Search This Blog

Tuesday, April 9, 2013

MADUDU YA LIGI KUU, SUPERSPORT YAPANGUA RATIBA, KISA KUONYESHA BURE MECHI ZA LIGI, YANGA YAKATAA



WAKATI ikiwa imebaki michezo michache kuelekea mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2012/13, wasimamizi wa ligi hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati ya Ligi wamepangua ratiba ya ligi hiyo ili kuruhusu baadhi ya mechi kuonyeshwa live na kituo cha luninga cha SuperSport, imefahamika.

Ratiba mpya imetangazwa leo lakini kwa mujibu wa chanzo chetu, viongozi wa vyombo hivyo viwili wanahangaika kuzungumza na klabu za ligi kuu ili ziweze kukubali kupanguliwa kwa ratiba hiyo ili SuperSport iweze kuonyesha mechi hizo live BURE.

Kituo hicho cha luninga kinatarajia kuonyesha mechi hizo live katika kile kinachoitwa SUPER WEEK ambapo baadhi ya mechi hizo zitaonyeshwa live kutoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lengo la SuperSport la kuonyesha mechi hizo live ni ‘kuipromoti’ ligi ya Tanzania na wachezaji wake ili waweze kupata kuonekana na watu wengine na kuingia katika biashara nzuri ya soka.

Mojawapo ya faida za mechi hizo kuonyeshwa live ni mchezaji kuweza kuonekana uwezo wake uwanjani hivyo kuweza kuitwa kwa majaribio au kusajiliwa na timu nyingine kutoka ndani na nje ya Afrika.

Faida nyingine ni kuutangaza Uwanja wa Taifa kwa timu za mataifa mengine ambazo zinaweza kuweka kambi ya muda nchini ikijiandaa na michuano mbaimbali. Lakini hata umakini wa waamuzi huongezeka pindi michezo inapokuwa inaonyeshwa moja kwa moja.

Hakika uonyeshwaji huu wa mechi live, ni moja kati ya maendeleo makubwa katika soka la Tanzania ukilinganisha na tulipotoka.



MICHEZO ZILIZOPANGULIWA


     
 
Kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini kitaonesha moja kwa moja mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom katika Super Week kati ya Aprili 11 na Mei 18 mwaka huu.

Mechi hizo ni kati Azam na African Lyon itakayochezwa Aprili 11 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Yanga na Oljoro JKT ambayo sasa itachezwa Aprili 13 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam na Simba itakayochezwa Aprili 14 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na mechi kati ya Coastal Union na JKT Ruvu itakayochezwa Aprili 16 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu.

Mechi nyingine ya Super Week itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga itakayofanyika Aprili 17 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu.

Pia mechi nyingine itakayooneshwa live na SuperSport ni kati ya Yanga na Simba itakayofanyika Mei 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na mechi za Super Week, mechi kati ya Mtibwa Sugar na Oljoro JKT iliyokuwa ichezwe Aprili 13 mwaka huu sasa itachezwa Aprili 17 mwaka huu Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.



YANGA YAGOMA

 


Inaelezwa kwamba, Yanga imekuwa klabu ya kwanza kukataa ombi hilo baada ya kubaini kuwepo kwa ubabaishaji katika mchakato mzima wa uonyeshwaji wa mechi hizo.

Yanga katika majibu yake kwa TFF na Kamati ya Ligi wikiendi iliyopita, imesema haiwezi kucheza Jumamosi na Oljoro kwani imeshafanya maandalizi yake ya mechi ya Jumatano, hivyo kukubali kucheza Jumamosi kutawaingiza katika hasara.

Kiongozi mmoja wa Yanga ameandika barua pepe kwa waendeshaji wa ligi akieleza klabu yake kuwa imeshamaliza maandalizi ya mchezo dhidi ya Oljoro.

Kinachoonekana hapa ni Yanga kushtukia mbinu chafu zinazoendelea kati ya SuperSport na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Ligi na TFF katika kukamilisha zoezi zima la SUPER WEEK.

Yanga imelalamika kwa kutojulishwa jambo hili tangu mapema kwani lianonekana lipo katika mchakato wa muendelezo. Kumbuka hii ni mara ya tatu kwa SUPER WEEK kuwepo.



TATIZO LA SUPER WEEK


Hiki kitu kinachoitwa SUPER WEEK sasa kinafanyika kwa mara ya tatu katika misimu miwili lakini kunakuwa hakuna maelezo ya kutosha kutoka kwa TFF, Kamati ya Ligi na SuperSport wenyewe na kila kitu hakipo wazi.

Wote wanapiga chapuo kwamba, hii ni nafasi pekee ya kuifanyia ‘promosheni’ ligi ya Tanzania lakini hawafafanui zaidi wanaposema SuperSport inafanya hivyo kama kuisaidia Tanzania kujitangaza.

Matangazo haya ya SUPER WEEK yanatangazwa kama ni ya BURE na ni kama msaada kwa ligi ya Tanzania ili iweze kujitangaza.

Hivi tujiulize kati ya ligi ya Tanzania, Kenya na Uganda, ipi ni bora zaidi ya mwenzake? Jibu lazima litakuja ni Tanzania kutokana na vigezo kadhaa ikiwemo Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuendesha michuano yake hapa nchini kila mara.

Katika Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo mashabiki hujitokeza kwa wingi uwanjani kulinganisha na nchi nyingine kama Kenya na Uganda.

Ajabu ni kwamba, ligi ya Kenya inaonyeshwa live na SuperSport tena kwa mkataba mnono unaozinufaisha klabu hivyo kuongeza ushindani katika ligi ya nchi hiyo. Hata hadhi ya viwanja vingi vinavyoonyesha ligi hiyo haitofautiani na vile vya Tanzania.

Pamoja na mambo yote haya, bado SUPER WEEK inafanyika bure kwa misingi ya kuendelea kuitangaza ligi ya Tanzania.



UKWELI WA MAMBO


Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, baadhi ya klabu zimebaini mchezo mchafu unaofanywa miongoni mwa viongozi wanaosimamia ligi na SuperSport ili kuweza kuonyesha mechi hizo BURE bila klabu kulipwa chochote.

Inaelezwa kuwa viongozi hao wamekuwa wakipata sehemu fulani ya fedha ili kuruhusu SUPER WEEK kufanyika huku klabu zikiambiwa zinafanyiwa ‘promo’ ya kutangaza wachezaji wake kupitia kituo hicho cha luninga.

Sasa viongozi hao wanasimamia dili la mechi hizi kuonyeshwa live wanahangaika kuziomba klabu hizo kukubali kuonyeshwa kwa mechi zake live.



UDHAIFU WA KLABU WAENDELEA


Bado klabu ambazo hazina nguvu kubwa kiuchumi zimeendelea kuburuzwa na kukubali kirahisi kuonyeshwa moja kwa moja kwa mechi zao na hata katika SUPER WEEK hilo limejitokeza.

Klabu hizo ama kwa viongozi wake kutofahamu au kufahamu na kupuuza au kutoelewa hadhi ya soka la Tanzania wamejikuta wakiingia mkenge na kukubali kubadilishwa kwa mechi zao.

Kinachosimamiwa hapa ni haki ya kila mtu katika nafasi yake, haki ya SuperSport inapaswa kuwepo, TFF, Kamati ya Ligi basin a hata haki ya klabu pia iwepo kwani ndiyo inayocheza mpira na kuingia gharama nyingi hadi kuonyeshwa live.

Inaonekana viongozi wengi kuanzia TFF, Kamati ya Ligi na hata klabu husika, hawatazami ni namna gani timu zinaingia gharama katika maandalizi hadi kufikia siku ya mchezo halafu mechi inaonyeshwa live bila ya wao kulipwa chochote.



MSIMAMO WETU


Tunaendelea kupigania haki ya klabu katika ligi kuu hasa tunapoona kuna kinaenda ndivyo sivyo lengo likiwa ni kuwa na ligi bora inayotokana na timu bora na siyo bora ligi.

Kuonyeshwa live kwa mechi si tatizo, tatizo ni kufuata haki na misingi ya kuonyeshwa live kwa mechi hizo. Tutaendelea kupigania hili kwa muda wote bila kuogopa maneno au vitisho vyovyote kwa kuwa hii ni kazi ya mtandao huu.

HATUWEZI KUWA MAADUI KWA KUSEMA UKWELI…..!


3 comments:

  1. Mi sielewi, ina maaana timu ndo zimeambiwa jana? Hii kali jamani. Klabu ziungane na yanga zijitambue zikatae kuburuzwa, huwezi kuuza wachezaji kwa mechi moja, dstv wanaitaka tanzani, tusiwe wanyonge, tukae chini tuongee biashara kitaeleweka tu..

    ReplyDelete
  2. Haiwezekani kubadilisha ratiba ya ligi kwa ajili ya tukio kama hili lisilo na faida kwa timu wala wachezaji wetu.Ratiba ya ligi lazima iheshimiwe,Makocha wanapanga programu ya mechi kwa kuangalia tarehe ya mechi inayofuata na hivyo kitendo cha kuahirisha mechi siku mbili kabla ya mechi kinavuruga programu ya kocha na utayari wa wachezaji kwa kuwa programu inamalizika siku moja kabla ya mechi.

    ReplyDelete
  3. Safi kaka vilabu vyetu vinapaswa viwe na umoja visiwe wasindikizaji au vyanzo vya mapato vya watu wachache wenye uchu na pesa

    ReplyDelete