Na Baraka Mpenja
Ligi kuu soka visiwani Zanzibar inazidi
kuchanja mbuga baada ya leo hii michezo miwili ya vuta ni kuvuta kushuhudiwa
katika viwanja viwili kisiwani Unguja na Pemba.
Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika
kwa michezo hiyo , katibu mkuu wa chama cha kandanda visiwani humo, ZFA, Masud Ettei,
amesema kisiwani Unguja klabu ya Mafunzo imeshuka dimbani na kuitungua bao 1-0
timu ya Zimamoto.
Kisiwania pemba vinara wa ligi hiyo
wenye ndoto ya kutwaa taji msimu huu na kuibeba bendera ya Zanzibar ligi ya
mabingwa barani afrika mwakani, klabu ya KMKM , imeshusha daluga zake na
kushinda mabao 3-2 dhidi ya timu bora ya Jamhuri ya Pemba.
“Mechi ya Unguja ilikuwa ngumu sana
kwa timu zote na ndio maana ushindi wa mbinde umepatikana, lakini kwa upande wa
pemba, washambiliaji hatari wa KMKM wameonesha jeuri kubwa sana baada ya
kufunga matatu, lakini Jamhuri wameonesha upinzani mkubwa sana”. Alisema Ettei.
Katibu huyo aliongeza kuwa kwa sasa
ligi ya visiwani humo ambayo KMKM wapo kileleni kwa kufikisha pointi 50 kufuatia
matokeo ya leo, ipo hatua za mwisho kwani kuna timu zimebakisha mechi tano na
nyingine mechi nne.
Ettei alisema timu za Mafunzo,
Jamhuri pamoja na Chuoni zinapambana kufa na kupona ili kupata nafasi za juu na
kuwakilisha taifa michuano ya kimataifa.
Baada ya mechi za leo ligi hiyo
itaendelea kesho kwa mechi moja kupigwa kisiwani pemba, Bandari ya unguja
itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Duma ya kisiwani Pemba.
Akizungumzia ushindani wa ligi hiyo,
Ettei alisema hali ni ngumu sana kwa timu zinazotaka kujinusru na mkasi wa
kushuka daraja msimu huu.
“Ushindani wa timu ni mkubwa sana, lakini hali
ni hatari zaidi kwa timu za Malinzi, wakongwe Zanzibar, Mundu , Super Falcon na
Duma ambazo zinachuana kukwepa mkasi wa kuporomoka daraja”. Alisema Ettei.
Zanzibar ni moja kati ya wanachama wa
shirikisho la soka barani Afrika CAF na timu zake huwa zinacheza ligi zake
yaani kombe la shirikisho na ligi ya mabingwa barani Afrika.
No comments:
Post a Comment