KOCHA wa Azam FC, Stewart Hall amekiri kuwa mfumo mpya wa uchezaji
alitumia kwa mara ya kwanza dhidi ya Simba uliigharimu timu hiyo ingawa
amemtaja winga Khamis Mcha kuwa ndiye shujaa wake.
Katika mchezo huo
wa ligi uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana
Jumapili na kumalizika kwa timu zote mbili kufungana mabao 2-2.
Mwingereza
huyo alibadilisha mfumo wa uchezaji kwa timu yake na kutumia mfumo wa
3:5:2 badala ya 4:3:3 ambao amekuwa akiutumia kwa kipindi kirefu.
Stewart
aliwatumia mabeki watano ambao ni Mkenya Jockins Atudo, David Mwantika,
Luckson Kakolaki na pembeni wakicheza Wazir Salum na Himid Mao
waliotumika zaidi kama mawinga.
Mfumo huo ulitoa
mwanya kwa vijana wa Simba ambao walikuwa wakicheza fomesheni ya 3:5:2
kupachika mabao mawili ya haraka ikiwa ndani ya dakika 18 za kipindi cha
kwanza.
Kocha huyo alifanya mabadiliko kwa kumtoa beki wa kati,
Luckson Kakolaki dakika 20 ya mchezo badala ya Khamis Mcha 'Vialli'
ambaye kuingia kwake Azam ilibadili mfumo na kucheza 4:3:3
Mcha
ilitumia dakika nne tangu alipoingia uwanjani na kuipa Azam penalti
iliyofungwa na Kipre Tchetche, baada ya kuangushwa na Miraji Adam
akienda kufunga.
Pia, alipiga faulo ambayo iliunganishwa na Mkenya Humphrey Mieno kufunga bao la pili kwa Azam FC.
"Kuingia kwa Mcha kulileta mafanikio kwetu. Nafikiri anastahili kuwa mchezaji bora wa mchezo." alisema Stewart.
Aliongeza;
"Ni mara ya kwanza kutumia mfumo wa 3:5:2. Nadhani mara nyingi
tunatumia 4:3:3, wachezaji wangu walishindwa kuushika kwa haraka na
kulazimika kubadilika."
"Lengo letu kutumia mfumo huo ni kuhakikisha
tunawabana vizuri katikati ya
uwanja na kufanya mashambulizi mengi. Lakini nafikiri hilo
halikuwezekana." alisema kocha huyo aliyetolewa kwenye benchi na mwamuzi
wa mchezo huo, Oden Mbaga.
No comments:
Post a Comment