Na Baraka Mpenja
Wapigwa kwata wa jeshi la kujenga taifa kutoka mkoani
Pwani, Ruvu shooting, wameihofia klabu ya Polisi Morogoro ambayo watakumbana
nayo kesho kutwa katika mchezo wa ligi
kuu soka Tanzania bara kufuatia kasi kubwa ya timu hiyo ngwe hii ya lala
salama.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Charles
Boniface Mkwasa “Master” amesema wapinzani wao wameonekana kujipanga sana huku
wakichagizwa na kampeni iliyoanzishwa na viongozi wa mkoa wa Morogoro kuinusuru
timu hiyo kushuka daraja msimu huu.
“Maandalizi yanakwenda vizuri
japokuwa kipindi hiki ni kigumu sana kwani kila timu inahitaji ushindi, Polisi
ni timu iliyojikusanyia pointi nyingi mzunguko wa pili, lakini hatukubali
kupoteza mechi ya tatu mfululizo”. Alisema Mkwasa.
Kocha huyo aliyewahi kuiongoza timu
ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars kwa mafanikio,aliongeza kuwa
licha ya polisi kuwa nyumbani siku hiyo, wao wanajipanga kuwashushia bunduki
zote ili kung`oka na mzigo wote wa pointi tatu muhimu.
Mkwasa alisema vijana wake wapo
barabara na wanaendelea kupiga jalamba la nguvu ili kupambana na maafande
wenzao ambao kwa sasa wanaongozwa na kocha mkuu Rishard Adolf.
“Hata wawe wagumu vipi hatuwezi
kuwakimbia, lazima tule nao sahani moja, namalizia program yangu ya mazoezi ili
kuwajenga vijana wangu kisaikolojia kwaniwameonekana kuwa na hofu kufuatia
kufungwa mechi mbili mfululizo, Tulifungwa na Yanga D ar es Salaam baada ya
hapo tukapoteza nyumbani dhidi ya Azam fc”. Aliongeza Mkwasa.
Pia kocha huyo mzawa wa Tanzania
aliwataka mashabiki wa klabu yake kuendelea kuwaunga mkono wakati huu wa dakika
za lala salama.
Wakati Mkwasa akiihofia Polisi
Morogoro, kwa upande wao wamesema wanapanga mashine za mauaji ili kupambana na
Shooting ambao ni kama simba aliyejeruhiwa baada ya kuboronga mechi mbili
zilizopita.
Afisa habari wa klabu hiyo, Clemence
Banzo amesema kwa sasa wanaendelea na mazoezi uwanja wa jamhuri na wachezaji
wote wapo katika morali kubwa ya kutafuta matokeo ya ushindi siku hiyo.
“Tukishinda mechi ya jumatano kuna
timu tatu tutazishusha katika msimamo wa ligi, mchezo huu ni kama fainali
ingawa utakuwa na changamotoa sana kutokana na matokeo ambayo wapinzani wetu
wameyapata huko nyuma”. Alisema Banzo.
Akizungumzia hali ya mashabiki mkoani
Morogoro, Banzo alisema wanafurahishwa na kitendo cha wana Morogoro wengi kuwaunga
mkono kila mechi, na kama wataendelea hivyo lazima timu itafanikiwa kubakia
ligi kuu msimu huu.
No comments:
Post a Comment