Search This Blog
Friday, February 22, 2013
SIMBA VS LIBOLO: SIFA ZA MCHEZAJI BORA NA LIBOLO ILIVYOIKAMATA SIMBA
WIKIENDI iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilicheza na CRD Libolo ya Angola katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo, Simba ilifungwa bao 1-0, bao lililofungwa dakika ya 24 kwa kichwa na Joao Martins akiunganisha krosi ya Carlos Almeida.
Libolo ilionekana kuwa timu iliyosheheni wachezaji wenye miili mikubwa ambao walionekana kuwa na nguvu, uwezo wa kumiliki mpira na akili ya mchezo.
Ungeweza kuona katika mchezo huo kwamba kuna muda Simba ilionekana kucheza soka safi lakini mipango yake mingi ilionekana kufa haraka tofauti na Libolo waliokuwa anaweza kumiliki mpira kwa muda mrefu.
Hapa chini ni sifa zinazomfanya mchezaji aonekane bora wakati wote; Katika zama hizi ambazo soka linahitaji uwezo wa hali ya juu ili mafanikio yapatikane, ni muhimu kufahamu mambo yanayofanya mchezaji awe tofauti na wenzie, zifuatazo ni sifa zinazomtambulisha mchezaji bora.
Nguvu
Kwanza kabla ya kitu kingine chochote, uwezo wa mchezaji kwenye upande wa fizikia lazima ufanyiwe uchambuzi . Hiki siyo kitendo cha haraka wala cha kufanyia wepesi na hii ndiyo hatua ya mwanzo ya kumtofautisha mchezaji wa ukweli au ambaye kwa lugha ya kigeni anaitwa A GREAT PLAYER na mchezaji wa kawaida anayefahamika kama MEDIOCRE / AVERAGE PLAYER .
Tofauti au kinyume na mawazo na imani za wengi kutambua sifa mbalimbali za mchezaji kwa upande wa nguvu au fizikia ndiyo hatua ngumu kuliko zote kwenye mchakato wa kumtambua mchezaji.
Unapotazama sifa za wachezaji kwenye upande wa nguvu lazima uwe na uhakika wa kuwaweka kwa utofauti na sifa zao nyingine za kimchezo na usiwafananishe na wachezaji wengine. Ni muhimu sana kugawanya sifa tofauti za mchezaji.
Unaweza kuona wachezaji wengi wa Simba wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kuuchezea, kupiga chenga kama ilivyo kwa wale wa Libolo, lakini tatizo lilikuwepo katika nguvu, Libolo walikuwa na nguvu zaidi ya Simba. Hilo halina ubishi.
Viungo kama Manuel Lopez na Sidnei Mariano waliweza kuwazidi nguvu viungo wa Simba, Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Lopez na Mariano waliweza kukimbia haraka pindi Kiemba au Kazimoto walipopata mpira na kuwazuia kisha kuwapokonya mipira kadiri walivyotaka. Wakati mwingine wachezaji wa Libolo hasa beki Gamaliel Musumari alikuwa akitumia nguvu tu na akili kidogo kuzima mashambulizi ya Simba yaliyokuwa yakitokea pembeni kwa Mrisho Ngassa.
Kasi
Baada ya hapa kuona nguvu, sasa tunaanza kutazama sifa mbalimbali zinazomtengeneza mchezaji wa ukweli au mchezaji mwenye uwezo mkubwa. Tunaanza na sifa zile ambazo ni za wazi kwa kila mmoja. Kasi au Spidi.
Chini ya mwavuli wa kasi kuna maelezo mengine madogo madogo. Kwa makocha na wachezaji, spidi yenyewe kama yenyewe haitoshi. Hata hivyo, wachezaji wakubwa wanaonyesha uwezo mkubwa wa kubadilisha kasi yao wakati wa mchezo.
Zaidi ya hapo haya mabadiliko ya kasi nayo yako kwenye migawanyiko mingi midogo midogo. Kuzielewa sifa hizi ndogo ndogo kwa sifa ya mchezaji kiujumla kama kasi ni muhimu sana na si katika kujua kuwa kasi ni muhimu tu, bali kumfanya mchezaji ajue jinsi ya kuifanya kasi yake imsaidie kuwa mchezaji bora.
Katika mchezo dhidi ya Libolo, Ngassa wa Simba amezoeleka kuwa na kasi mchezoni hata chipukizi Haruna Chanongo anaweza kuwa hivyo pia. Kasi inaweza kutumiwa na mchezaji kutengeneza nafasi kwa ajili yao na hata wenzao, Je, Ngassa alikuwa na uwezo wa kutumia kasi yake kujitengenezea nafasi akiwa amebanwa?
Unaweza kuona jibu likikuwa hapana, kwani Ngassa mara nyingi alikuwa akirudisha nyuma mipira alipoona amebanwa na hata wachezaji wenzake hawakuwa wakienda sawa na kasi yake anapokuwa na mpira.
Pia kuna wakati Ngassa hakuweza kuendana na wenzake katika matumizi ya kasi, anawajua vyema wenzake kuhusu uwezo wao wa kasi, hivyo hakupaswa kuwa na haraka ya kukimbia na mpira huku akiwaacha wenzake nyuma.
Katika kiungo, mwanzo Mussa Mudde alikuwa anacheza kwa kasi lakini mpira ukifika kwa wenzake ulikuwa ukipozwa na kucheza kwa kasi ndogo, hilo lilikuwa tatizo. Rhythm ya kasi haikuwa sawa kwa Simba
Ukiwa unatazama kasi ya mchezaji, unapaswa kuweza kutambua kuwa mchezaji anatumia kasi kwa wakati gani na anaitumiaje kasi yake na zaidi ya hapo lazima uwe una uwezo wa kutambua kuwa kasi ya mchezaji ina sababisha hatari kwa timu pinzani wakiwa nao mpira na wakiwa hawana mpira.
Kuhusu hilo, Libolo walikuwa na kasi ya mpira mara zote, wakiwa na mpira na wasipokuwa nao. Tazama Almeida alivyopiga krosi ya bao, hakuna aliyedhani kama angeweza kufanya hivyo na ndiyo maana mfungaji aliruka kichwa peke yake na kufunga kirahisi.
Wachezaji wa Simba hawakudhani kama krosi itapigwa, tena mbele ya beki Shomari Kapombe aliyedhani labda Almeida angemgongesha mpira ili uwe wa kurushwa ama kona.
Libolo waliweza kuwa na kasi ile ile wanapokuwa na mpira hata wasipokuwa nao, waliweza kutengeneza mipira mingi kuelekea lango la Simba na mara nyingi mipira yao ilipotea nje ya kidogo ya eneo la hatari la Simba.
Kutokana na kucheza bila kasi, wachezaji wa Simba mara nyingi walikuwa wakipokonywa mipira miguuni na wenzao wa Libolo waliokuwa na kasi muda wote.
Uwezo wa kimwili
Kipengelea kingine cha kasi ni uwezo wa kimwili wa kimichezo yaani ATHLETICISM. Hii ni jinsi ya mchezaji anavyotumia wepesi wa mwili pamoja na mienendo yake akiwa kwenye mapambano ya uwanjani.
Hapa kama ilivyokuwa kwenye nguvu na kasi unapaswa kufahamu kama mchezaji anatumia wepesi wake wa kimichezo au hiyo ATHLETICIMS yake kufanya mambo fulani yatokee uwanjani.
Je, ndiyo kitu pekee anachokitegemea mchezaji awapo uwanjani au anatumia uwezo wa mwili wake kimichezo kama kitu cha kawaida?
Mtazame beki wa kulia wa Simba, Nassoro Masoud ‘Chollo’, huyu ni mwepesi wa kuanzisha mashambulizi, kupandisha timu na hata kupiga mashuti langoni. Simba haikutumia vyema uwezo wa Chollo ili kuikabiri vyema Libolo.
Mchezaji anayetumia uwezo wa mwili wake kimichezo ni aina ya mchezaji ambaye ana uwezo mkubwa wa kujiendeleza kimichezo kuliko mchezaji anayetegemea uwezo wake wa kimichezo.
Kumbuka siku zote kuna mchezaji ambaye ana kasi, nguvu ana akili na siku zote anafanya vizuri uwanjani lakini haimaanishi kuwa mchezaji amejiandaa kwa ubora.
Ukubwa au udogo wa kimo cha mchezaji
Ukubwa au udogo wa kimo cha mchezaji umeonekana kuwa jambo muhimu sana kwenye mchezo wa soka kwa sasa na dhana hii inazidi kupata nguvu kadri siku zinavyozidi kwenda mbele.
Libolo ilikuwa na wachezaji wengi warefu na wenye nguvu kuliko Simba. Mabeki wa kati Pedro Ribeiro na Musumari ni warefu na wanaotumia nguvu kupita kiasi katika kuzuia. Sasa beki wa namna hiyo anapokutana namchezaji kma Ngassa au Chanongo hali haiwezi kuwa ya kawaida.
Kuna njia nyingi ambazo mchezaji anaweza kuonyesha au kudhihirishwa uwezo wake huku akiwadhuru wapinzani, kwa mahusiano na nguvu ya mchezaji.
Ni muhimu kutazama kuwa mchezaji ana uwezo wa kutimiza malengo yake kwa wenzie na kwa wapinzani. Hiki ni kitu ambacho timu ingependa mchezaji binafsi akifanye kama timu inataka kutafuta ushindi.
FITNESS
Sehemu nyingine ya nguvu za mchezaji ni kuwa kwenye hali nzuri ya kimchezo kimwili yaani FITNESS na pamoja na uwezo wa kuvumilia na kubakia na nguvu pale ambapo mapambano yanazidi kuwa magumu uwanjani.
Hii inaweza kuwa sehemu muhimu kuliko zote kwenye maendeleo ya mchezaji kwani angalau kila mchezaji ana uwezo wa kucheza ila performance inaathiriwa na FITNESS.
Katika mchezo dhidi ya Libolo, Simba haikucheza katika kiwango chake kwa muda mrefu na kutoa mwanya kwa Libolo kucheza wanavyotaka. Kuna muda Simba walionekana kupungua nguvu na hata kasi yao.
Tazama dakika ya 90, Libolo waliweza kugongeana pasi kama 25 hivi bila Simba kugusa mpira. Wachezaji wa Simba walionekana kukata tamaa, na kushindwa kuwakaba Libolo wasiweze kucheza pasi hizo hadi mpira unaisha.
Kama mchezaji akiwa katika hali nzuri basi ataonyesha kiwango cha hali ya juu na kinyume na hapo haijalishi kipaji alichonacho, kama FITNESS inakosekana uwezo wa mchezaji lazima utashuka.
Zaidi ya hapo bila kuwa na FITNESS mchezaji hawezi kuwa na bidii mchezoni na hapo ndiyo umuhimu wa PHYSIQUE ya mchezaji unapokuja, bila nguvu WORK RATE ya mchezaji itakuwa chini.
Katika soka la leo mchezaji anahitajika kuonyesha WORK RATE ya kiwango cha juu maradufu.
USIKOSE SEHEMU YA PILI….
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment