WAKATI klabu ya Azam ikituma 'mashushu' nchini Sudan Kusini, Serikali
imewahakikishia wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la
Shirikisho, usalama wao kwa kipindi chote watakachokuwa Sudan Kusini.
Azam
itacheza mechi ya marudiano na timu ya Al Nasri ya nchi hiyo kati ya
Machi 2 na 3, mchezo utakaopigwa mjini Juba nchini humo.
Waziri
wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alikiri
kuwepo kwa vita baina ya Sudan na Sudan Kusini licha ya kuwahakikishia
Azam usalama wao.
" Azam iwe na amani
kwani mapigano hayo yanafanyika mbali na mahali itakapochezwa mechi hiyo," alisema Waziri Membe katika mahojiano na Mwananchi.
Kwa
mujibu wa Membe mapigano hayo yanafanyika mpakani mwa Sudan na Sudan
Kusini ambako ni mbali na Juba itakapochezwa mechi hiyo ya kimataifa.
"Juba
ni mbali na yanapofanyika mapigano na shughuli zinaendelea kama kawaida
hakuna tofauti na Dar es Salaam kuna amani ya kutosha," alisema Waziri
Membe.
Akifafanua umbali wa kutoka Juba hadi yanapofanyika mapigano hayo Waziri Membe alisema ni sawa na Dar es Salaam na Songea.
"Cha
msingi Azam ijiandae kikamilifu kwa ajili ya kupeperusha vema bendera
ya Tanzania bila kuwa na uoga wowote zaidi wazingatie nidhamu ya ndani
na nje ya uwanja kwenye mechi yao.
Azam inahitaji sare ya
aina yoyote ili iweze kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi wa
magoli 3-1 kwenye mechi yao ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam.
Wakati
huo huo klabu ya Azam itaweka kambi nchini Uganda kabla ya kuondoka kwenda Sudan Kusini kwenye mechi yao ya marudiano.
Kocha
mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall alisema timu hiyo itaondoka kati ya
Jumatatu na Jumanne kwenda jijini Kampala itakapoweka kambi hiyo ikiwa
ni baada ya mechi yao ya kesho dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa taifa
jijini Dar es Salaam.
"Mechi yetu na Yanga itakuwa kipimo cha mwisho kabla ya kwenda Uganda," alisema kocha huyo raia wa Uingereza.
Kwa
mujibu wa Hall, klabu yake imetuma wapelelezi nchini humo kwa ajili ya
kuweka sawa mazingira watakayofikia ikiwa ni sambamba na kuangalia hali
ya hewa ya mji wq Juba ambayo wameambiwa haina tofauti na ile Kampala.
Akizungumzia
muonekano wa vijana wake kabla ya mechi hiyo Hall alisema wako katika
hali nzuri na kusisitiza Azam inanafasi ya kusonga mbele kwenye michuano
hiyo na hatimaye kutwaa ubingwa.
No comments:
Post a Comment