Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa
barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.
Rage
ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga
barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo
kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira
Tanzania zinavyoeleza.’
Amekataa
ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa
kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea
kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia kusimamia sheria na kanuni hizo
kama inavyotakiwa badala ya kujiuzulu.
“Kutokana
na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu, ni
vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama
inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu
za maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga.
Pia
Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa
kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati zote za
TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala
kupendelea upande wowote.
Rais
Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili
bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati
zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo,
uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa
miguu kuongozwa kwa sheria na haki.
No comments:
Post a Comment