Kumekuwepo
na taarifa tofauti kuhusu kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara ambayo kwa mujibu
wa kalenda ya Shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
inatakiwa kuanza Septemba 01, 2012. Baada ya kikao cha pamoja baina ya
TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika Jumatatu ya Agosti
20, 2012 kwenye ofisi za TFF, TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1. Baada
ya kikao cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu
zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa
mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa, yaani
Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii
inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande
husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2. Mazungumzo
baina ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni
mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza
kusainiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
3. Kukamilika
kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila
ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa
kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika
kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa
muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na masuala mengine
muhimu.
4. Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu
5. Kutokana
na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao
ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao
sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa
Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku
itakayotangazwa baadaye.
6. Kuhusu
chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya
Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu
kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya
TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili
ya hatua za mwisho.
No comments:
Post a Comment