Search This Blog

Tuesday, June 12, 2012

UFARANSA VS ENGLAND: ROY HODGSON NA FALSAFA YA KUPAKI BASI - KAPATA ALICHOTAKA

Hii ilikuwa mechi ambayo ilikuwa na ubunifu mdogo sana huku ikichezwa kwa kasi ya chini sana .
Laureant Blanc aliteua kikosi ambacho kilicheza mfumo ambao kila mmoja alitarajia mfumo wa 4-3-3, huku Florent Malouda akihangaika mbele akitokea katikati ya uwanja.
Roy Hodgson aliwashangaza watu wengi kwa kumpanga Alex Oxlade Chamberlain ambaye alicheza upande wa kushoto huku James Milner akicheza upande wa kulia  na Danny Welbeck akiongoza mashambulizi .
Kama ilivyotarajiwa, Ufaransa ilitawala sana mpira kwa maana ya umiliki huku ikimaliza kwa wastani wa asilimia 65 ya umiliki wa mpira huku wakipiga mashuti 21 tofauti na England ambao walipiga mashuti matano pekee. Hata hivyo mashuti mengi ya Ufaransa yalikuwa ya mbali yasiyokuwa na madhara ukiachilia mbali shuti la Nasri ambalo lilizaa bao la kusawazisha, yote kwa yote Ufaransa walihangaika kutengeneza nafasi za wazi.
Vita ya Mfumo
Ilikuwa vita nyepesi. England walikuwa na makundi ya wachezaji wanne wanne kwenye ulinzi na kiungo huku Ashley Young na Welbeck wakicheza mbele - Laureant Blanc alimpa Alou Diarra maelekezo ya kumkaba Ashley Young na kumnyima nafasi ya kufanya kazi kwa uhuru hasa pale ambapo Young alikuwa anarudi chini kusaka mpira. Yohan Cabaye alikuwa akicheza juu karibu na sehemu aliyokuwa Gerard na Malouda alikuwa akijaribu kumvuta Scott Parker kutoka kwenye nafasi yake aliyokuwa. Kiujumla kulikuwa na nafasi finyu sana kwa Ufaransa kufanya mambo yake kwa uhuru kwani England walijaza upande wao na kuwanyima Ufaransa uhuru wa kupiga pasi walizohitaji kupanga mashambulizi. Ufaransa walijaribu mbinu ya kupitisha mipira jambo ambalo liliwafanya  England kutoa mipira mingi iliyoza kona ambazo hazikuzaa matunda .
 
Mashambulizi ya Ufaransa.
Wachezaji wanne wa Ufaransa waliokuwa wanacheza kwenye eneo la mbele akiwemo Malouda walikuwa wakipeana pasi kwa ufanisi. Wakati Riberry akiwa anacheza sana pembeni upande wa kushoto, Samir Nasri yeye alikuwa akisafa uwanja mzima na kucheza kila mahali jambo ambalo lilifungua nafasi kwa Mathieu Debuchy. Kiujumla mbinu na mipango yote ya Ufaransa ilimzunguka Samir Nasri na hata takwimu zilionyesha kuwa alicheza pasi nyingi kuliko wachezaji wote waliokuwa uwanjani jana. Kiujumla Nasri alitengeneza nafasi nane kwenye mchezo wote.
Nasri alikuwa mtu pekee ambaye alikuwa akitumia nafasi akijaribu kujenga mashambulizi, alikuwa akiingia kwenye eneo ambalo lilikuwa wazi na kuwachanganya wachezaji wa England wasijue la kufanya ili kumkabili. Wakati mwingine Lescott alikuwa akitoka nyuma na kujaribu kumfuata kumbugudhi asilete madhara, wakati mwingine Ashley Cole angetoka kwenye eneo lake na kujaribu kumkaba, kiujumla ile hali ya kuwavuruga wachezaji wa England kwenye jinsi ya kumkabili Nasri ndio ilikuwa msingi wa mashambulizi ya Ufaransa. Hata bao alilofunga Nasri lilikuja wakati ambao mabeki wa England walikuwa wamesogea ndani sana na kumuachia Nasri nafasi ambayo ilimfanya achague sehemu ya kupiga mpira na kusawazisha .
Ukiachilia mbali Movement za Nasri, England waliyamudu mashambulizi ya Ufaransa. Kikosi cha Laureant Blanc kilicheza kwa uvumilivu huku wakingoja nafasi ya wazi ambayo ingewapa mwanya wa kuidhuru England na hawakuwa wakiwaachia wachezaji wengi mbele katika hali ambayo pengine ingeweza kuwa na madhara hasa ukizingatia England walivyo wepesi kwenye mashambulizi ya Counter.
 
Mashambulizi ya England.
Mchezo wa England kwa ujumla ulijengwa kwenye kukubali presha ya Ufaransa na kujaribu kuvunja mashambulizi kwa hataka na kushambulia kwa kushtukiza –walifanikiwa katika hili kwenye michezo miwili ya kirafiki kabla ya michuano hii kuanza lakini kwa mchezo dhidi ya Ufaransa walikosa ufanisi kwenye jinsi ya kumalizia nafasi chache zilizotokea ndani ya mchezo. Sababu kubwa ya hili ilikuwa jinsi Ashley Young alivyoshindwa kutumika kwenye mchezo kama ilivyozoeleka. Alimaliza pasi 12 pekee kati ya 20 alizotengeneza .
Hata hivyo sifa kubwa ilimuendea Alou Diarra ambaye alikuwa mjanja sana kwa jinsi alivyojipanga na kumzuia Young wakati England walipokuwa na mpira . Kitakwimu Diarra Diarra alimaliza au alifikisha pasi zote alizopiga na tackles zake zote 5 alizopiga zilikuwa za mafanikio .
Nafasi pekee ya wazi ambayo England walitengeneza wakati mchezo ukiendelea ilikuja wakati James Milner alipomzunguka kipa Hugo Lloris lakini alipiga nje . Alex Oxlade Chamberlain aliingia katikati ya uwanja na Alou Diarra alimfuata jambo ambalo lilimfanya Ashley Young kuwa huru na kumpa Milner pasi, nafasi kama hii haikujitokeza tena. Danny Welbeck alicheza vizuri akikaa na mipira, lakini hakuwa na wakati mzuri kwa kuwa msaada wake mkubwa unatoka kwa Ashley Young ambaye alibanwa kwa kiasi kikubwa .
Young na Welbeck walicheza vizuri sana hasa walipokuwa bila mpira. Hawakukimbiza na kukaba mabeki wa pembeni wa Ufaransa, badala yake walisimama njiani na kuzuia pasi za wafaransa kupita njiani. Philipe Mexes na Adil Rami walikuwa wakipiga mipira ya moja kwa moja na walishindwa kupeleka mipira mbele toka nyuma, matokeo yake mchezo ulikuwa wa taratibu jambo ambalo kwa England lilikuwa zuri.
 
 
Kipindi cha Pili.
Mchezo ulikosa mwendelezo kwenye kipindi cha pili . England waliendelea kukaa mbele ya lango na Ufaransa walishindwa kuongeza idadi ya wachezaji waliokuwa wakishambulia nao. Bado mchezo uliendelea kuwa wa taratibu na timu zote zilionekana kuchoka mapema na kutambua kuwa sare yalikuwa matokeo mazuri.
Labda maendeleo pekee yalikuwa kwenye movement za Karim Benzema ambaye alionekana kukerwa na kukosekana kwa ubunifu na huduma ya pasi zilizoelekea kwake jambo lilomfanya ajaribu kufanya kila kitu mwenyewe . Mwishoni alijaribu kuiga alichokuwa anafanya Samir Nasri na kusogea kwenye maeneo ambayo yalikuwa na nafasi na alifanya hivi na kupiga mashuti ya mbali ambayo Jo Hart aliokoa. Timu zote zilichelewa kufanya mabadiliko, England walimuingiza Jermaine Defoe ambaye aliingia kwenye nafasi ya Alex Oxlade Chamberlain ambapo Ashley Young alienda kushoto na Jordan Henderson aliingia kwneye nafasi ya Scott Parker aliyeonekana kuchoka . Haya yalikuwa mabadiliko ambayo yalilenga kujenga mashambulizi zaidi hasa ukizingatia mabeki wa Ufaransa walionekana wamechoka .
Laureant Blanc alimuingiza Hatem Ben Arfa na Marvin Martin waliochukua nafasi za Malouda na Cabaye lakini mabadiliko haya yalifanywa muda ukiwa umepita na walikosa muda wa kufanya kazi ya kuokoa mchezo.
Mwisho.
Kwenye michezo yote ya raundi ya kwanza kumekuwa na soka la wazi sana ambalo kiujumla limetoa burudani kubwa lakini mchezo wa ufaransa na England ulikuwa wa kasi ya chini kupita yote . Ni kama timu zote zilikuwa zimepanga kutopoteza mchezo huukuliko zilivyopanga kutafuta ushindi na sare ilikuwa kama imepangwa huku Ufaransa wakionekana kupiga zaidi mashuti ya mbali baada ya kuona wameshindwa kuivunja defense ya England .
Shape ya England haikuwa mbaya , hata hivyo mabadiliko ya movement toka wakati ambapo timu haina mpira na pale ilipokuwa na mpira hazikuwa nzuri na hii ilitokana na Ashley Young kufichwa sana . Kwa mfumo wa England Young ni mtu muhimu lakini Ufaransa walifanya kazi kubwa ya kumtia mfukoni . Hodgson anapaswa kufanya kazi kubwa ya kuifanya England kuwa na madhara zaidi inapokuwa na mpira

No comments:

Post a Comment