Search This Blog

Tuesday, June 12, 2012

Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’-EPISODE 6

BAKARI MALIMA MWENYE JEZI YA NJANO.

*Azuiawa kwenda Rwanda, aitwa mahakamani
*Aifungia Yanga bao ugenini, alitoa zawadi
Na Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA tuliishia Malima akiwa ameanza mazoezi na Yanga kujiandaa dhidi ya Rayon. Lakini hofu yake kubwa ilikuwa ni namna ya kuieleza timu yake ya Vaal Professional ya Afrika Kusini kwamba amejiunga Yanga na hatarudi kuichezea. Je atafanyaje? Endelea.
NILIWAZA namna ya kuwaeleza jamaa, mmiliki wa timu alikuwa ni rafiki yangu na tulikuwa tukiwasiliana mara kadhaa kabla sijaenda kule. Hata kile kipindi nilichonyimwa kibali kutoka Fat halafu Nonda akapata kutoka Burundi, bado aliendelea kunikarimu.
Nilijisikia vibaya sana kuona nawaangusha, lakini haikuwa nia yangu kufanya hivyo na sikuwa na ujanja pia. Niliamua kupiga simu na kuwaleza kila kitu, walishangazwa na hali hiyo ingawa walishasikia angalau kidogo kuhusiana na suala hilo.
Walionekana wako upande wangu na kuahidi wangesubiri nimalize suala hilo halafu nirejee kuichezea timu hiyo maana nilikuwa na mkataba wa miaka mitatu na nilikuwa nimecheza nusu msimu tu.
Huku nyumbani, awali sikuelewa vizuri. Yanga ilitakiwa kucheza na Rayon Sports ya Rwanda mechi mbili, nyumbani na ugenini, mshindi anmgevuka na kucheza hatua ya nane bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Hivyo maandalizi hapa Dar es Salaam yaliendelea chini ya Kocha Mkuu, Tito Mwaluvanda na msaidizi, Fred Felix Minziro. Wakati huo tuliweka kambi Chuo cha Posta, Kijitonyama.

Ila mimi niliendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi ya pili ambayo ingechezwa Dar es Salaam, maana mahakama ilizuia paspoti yangu. Sikutakiwa kusafiri nje ya nchi kutokana na kesi yangu ya tuhuma za kuhusishwa na madawa ya kulevya iliyokuwa inaendelea.
Hali hiyo iliniumiza sana, lakini niliamua kukubaliana nayo. Nilichofanya ni kuendelea kujifua kwa nguvu sana, nilijua siku moja suala hilo litaisha tu. Kwa ninavyojijua, nilianza kuwa fiti, niliamini nitacheza vizuri katika mechi yoyote nitakayopangwa.
Siku nne kabla ya Yanga kusafiri kwenda Rwanda, nilitakiwa kwenda mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. Nilikuwa nina hofu sana, nilijua ni wakati mgumu. Lakini nilimuachia Mungu, maana nilijiamini sikuwa nimefanya makosa yoyote.
Tulipofika mahakamani, watu wengi walikuwa pale lakini si sana kwa kuwa kesi haikuripotiwa sana kwenye vyombo vya habari kutokana na kwamba ilikuwa ni ghafla sana baada ya upelelezi kuwa umekamilika.
Niliongozana na wanasheria wangu na mahakama ikafanya kazi yake muda mrefu , nilikuwa pale kimya muda wote. Nilijua kila kitu kitaenda vizuri kwa uwezo wake Mungu. Baada ya muda mrefu wa taratibu za kimahakama, tuliachiwa huru.
Kesi hiyo kwa kumbukumbu zangu ilikwenda kwa mwaka mzima, nakumbuka niliachiwa Mei, 1998. Nilikuwa nina furaha ambayo haina mfano, nilichanganyikiwa. Mashabiki walinifuata na kunikumbatia, baadhi ya ndugu zangu walikuwa pale. Wanayanga na wengi pia wlaikuwa pale na tukafanya sherehe ya muda pale. Baada ya hapo nikaondoka na viongozi kurudi kambini. Sikuamini, niliona kama ninaota.

Pamoja na kufurahi kuachiwa, nilijua ningeweza kusafiri na Yanga kwenda Rwanda, kitu ambacho nilikitaka kwa nguvu sana. Nilitaka kuitumikia Yanga na kuwalipa kutokana na msaada mkubwa walionipa kutoka katika kitu hicho kibaya kabisa maishani mwangu.
Suala hilo la kutuhumiwa kuwa na madawa ya kulevya, lilirudisha nyuma maisha yangu. Niliona ulikuwa ni kama mpango uliosukwa kwa ajili ya kuniharibia maisha yangu. Lakini bado mwisho, niliona acha nimuachie Mungu kwa mara nyingine.
Nilipofika kambini, nilikuwa kama nimepagawa, sikuchelewa. Nilivaa viatu na moja kwa moja nikaenda uwanjani kuanza mazoezi. Baada ya saa moja wenzangu walikuja, tukaungana na kuendelea pamoja tena.
Alhamisi tukaondoka kwenda Kigali, tukiwa tayari kwa vita. Mechi ilichezwa Jumapili na mechi ilipoanza tu, dakika ya tano, mchezaji wetu, Banza Tshikala akalambwa kadi nyekundu. Maana yake tukawa pungufu halafu tuko ugenini.
Lakini mimi nilijituma sana, nilijua kasi haikuwa lahisi. Rayon walipata bao lakini Seki (Chambua) akasawazisha kitaalamu. Baadaye nami nikafunga bao kw akichwa baada ya kuunganisha mpira wa adhabu wa Seki.
Mwishoni kabisa, jamaa wakasawazisha. Matokeo yakawa 2-2, tukarudi nyumbani kusubiri mechi ya marudiano ambayo angalau sare ya bila kufungana au moja moja ingetupeleka mbele. Nilipofika Dar es Salaam, nikalitoa zawadi bao langu kama zawadi kwa Wanayanga.
Kwa pamoja, wachezaji tuliuomba uongozi wa klabu uturuhusu mechi dhidi ya Rayon ichezwe CCM Kirumba, Mwanza. Tulihofia presha ya Dar es Salaam, wangeweza kutuchanganya. Kitu kizuri uongozi ukakubaliana nasi. Maandalizi ya mechi inayofuatia, yakaanza.
MALIMA ameungana na Yanga hadi Rwanda na mchango wake ukawa mkubwa sana. Macho na masikio yameelekezwa katika mechi ya pili iliyopangwa kuchezwa mjini Mwanza. Je, watafanikiwa kuvuka. Kuna kitu kingine Malima atafanya na timu yake ya Afrika Kusini itaendelea kukaa kimya?

1 comment:

  1. shafii huyu aiyevaa jezi ya man u ni nani? au ndio mbwiga. kama sio bac tuwekee picha ya mbwiga mana tunampenda sana.

    ReplyDelete