BARAZA la wazee la klabu ya Yanga limesikitishwa na kauli za kejeli na zenye kuwadhalilisha alizozitoa mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga juzi, hivyo kuanzia sasa wamemwachia aendelee na timu hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Nchunga kudai kuwa wazee hao walikurupuka na hawezi kukabidhi kwa wahuni, pia sehemu ambapo hana uhakika na usalama, huku akihofu timu hiyo kuhudumiwa na wauza dawa za kulevya.
Wakizungumza na mamapipiro blog leo asubuhi wazee hao wakiongozwa na katibu wao Ibrahim Akilimali walisema kwamba hawakukupupuka kutangaza kuichukua timu bali walikubaliana na Nchunga, lakini wanashangaa baadaye kuwageuka.
“Hatukukurupuka kuongea vile, ilikuwa ni ridhaa ya Nchunga, tulikuwa sahihi kutokana na mapenzi yetu na timu, pamoja na kuwa uongozi ndio una haki tuliikubaliana kuichukua timu kwa lengo la kuhakikisha inaifunga Simba, tunafanya usajili wa uhakika na kurejesha nidhamu,”alisema.
“Ni ajabu kwa Nchunga kututamkia sisi wauza unga, inamaana mama Fatma Karume, Francis Kifukwe, Seif Ahmed, Abdallah Binkleb na Yusuf Manji ni wauza unga?
...hivi Nchunga anajua umuhimu wa hawa watu ndani ya Yanga,tena kwa mshangao mkubwa amediriki hata kutuma watu wamzuie kuingia klabuni mzee Kitundu (Jabir)ambaye alishiriki kuijenga klabu,”alisema Mzee Akilimali.
Naye mjumbe wa baraza hilo, Yussuf Mzimba pamoja kusikitishwa na kauli za Nchunga, alisema Yanga ina wenyewe na kwamba ukifuga kuku wengi lazima utapata aliye kisirani ambao wanajifanya wanajua kumbe si lolote.
“Tunataka serikali iangali watu kama hawa, Nchunga hawezi kutukana watu kama kina mama Karume, inaonekana klabu imemshinda kwani aliingia madarakani kwa bahati tu na matokeo yake kaleta mgawanyiko badala ya umoja”,alisema mzee Bilal Chakupewa.
Aidha Mzee Chakupewa aliongeza kwamba hata kama wakiifunga Simba jumamosi Nchunga ni lazima aondolewe madarakani kutokana na udhaifu aliouonyesha kwenye uongozi wake na kuifikisha Yanga mahala pabaya
No comments:
Post a Comment