Search This Blog

Monday, April 16, 2012

REST IN PEACE BADI SALEHE

MCHEZAJI wa zamani wa Yanga ya Dar es Salaam, Badi Salehe amefariki dunia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mtoto mkubwa wa marehemu, Salehe Badi alisema baba yake alikutwa na mauti jana asubuhi Hospitali ya Temeke alikokuwa amelazwa tangu Jumatano akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.


Alisema Salehe ambaye wakati wa uhai wake alikuwa akimudu vyema nafasi mbalimbali, ikiwemo kiungo na wakati mwingine ushambuliaji kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo hadi kufikia kukatwa mguu.


“Hali imekuwa ikibadilika mara kwa mara, wakati mwingine anakuwa vizuri na wakati

mwingine hali inabadilika, lakini Jumatano sukari ilipanda sana, hivyo tukampeleka Hospitali ya Temeke hadi mauti yanamkuta,” alisema Salehe, ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu za Bandari Mtwara na Kariakoo Lindi.

Alisema msiba uko nyumbani kwa marehemu Tandika, Dar es Salaam na kuwa maziko yanatarajiwa kufanyika mchana Msongola, baada ya shughuli ya kumaliza kuuswalia mwili wa marehemu hapohapo Tandika.


Licha ya kuichezea Yanga miaka ya 1960 hadi miaka ya 1970, Salehe pia amewahi kuifundisha timu hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1980 na amewahi kuchezea timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars; kwa nyakati tofauti.


Pia amewahi kuchezea na kuinoa timu ya Sigara ya Dar es Salaam, Bandari Cargo na aliteuliwa

na Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (Tefa) kuwa kocha wa timu ya mkoa huo kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Taifa mwaka jana, lakini alishindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na maradhi.

Kwa mujibu wa Salehe, marehemu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 75, ameacha wajane wawili, watoto nane na wajukuu 14.


 

No comments:

Post a Comment