Search This Blog
Monday, January 30, 2012
YANGA IJIFUNZE KUPITIA MCHEZO DHIDI YA ZAMALEK!
Wakati ilipotoka ratiba iliyoonyesha kuwa Yanga watacheza na Zamalek kwenye hatua za awali za michuano ya Ligi ya mabingwa barani afrika watu wengi kwa haraka waliamiani kuwa mwanzo wa mwisho wa yanga umewadia . Ukitazama historia ya timu za Tanzania dhidi ya timu za kaskazini mwa Afrika unapata sababu ya kwanza ya kuona jinsi Yanga walivyo na kazi kubwa ya kufanya lakini ukiangalia rekodi ya Yanga kama klabu katika michezo yao dhidi ya Klabu za Uarabuni hapo ndio kabisa unaona kiza mbele kwani katika mara chache ambazo klabu za Tanzania zimeonyesha kujitutumua mbele ya timu toka Uarabuni Simba ndio imekuwa ikifanya hivyo na si Yanga.
Hii haimaanishi kuwa Yanga wanapaswa kukata tama moja kwa moja kwani ndio hali halisi ya ushindani wa soka mahali kokote pale hata barani ulaya kwa mtu yoyote anayepangwa kucheza na Barcelona anaona kama UEFA imemuonea kwani asilimia 90 ya matarajio ni kipigo .
Kitu kimoja ambacho klabu za Tanzania zimekuwa zikizembea ni kuchukulia changamoto ya kufanya vibaya kama chachu ya kujipanga na kufanya vizuri siku za mbeleni kwa sababu pale unapofungwa haimaanishi kuwa mchezo wa soka ndio umefikia mwisho , mbele kuna michezo mingine ambayo kama kweli umejifunza kupitia makosa ya nyuma lazima utafanya vizuri .
Zamalek ni moja ya timu tano bora za miaka yote barani Afrika , hivi majuzi tu klabu hii imetimiza miaka mia moja na sehemu walikofika inaendana ama unaweza kusema inaakisi umri waliofikia katika miaka yote hiyo kwani klabu hii imewekeza kwenye soka na ndio maani imefika hapa ilikofika.
Kwa ufupi tu Historia ya Zamalek ilianzia mwaka 1911 ambapo mwanasheria raia wa Ubelgiji aliamua kuanzisha timu ya mpira wa miguu aliyoipa jina la Kasr El-Nile Club . Klabu hii wakati ilipoanzishwa ilikuwa na tofauti na klabu nyingine kwani yenyewe haikuwa na matabaka ambayo yangemzuia mtu kujiunga nayo , kwa kifupi ilikuwa klabu ya kila mtu.
Katika historia yake Zamalek imewahi kutwaa mataji 11 ya ubingwa wa Ligi ya Misri pamoja na mataji 11 ya Kombe la Misri au Egyptian Cup. Kwa upande wa mataji ya kimataifa Zamalek imetwaa ubingwa wa klabu bingwa ya Afrika mara tano pamoja na ubingwa wa kombe la washindi barani afrika mara moja huku wakiwa na mataji matatu ya Caf Super cup.
Hata hivyo hali haijawa nzuri sana kwa Zamalek kwenye miaka ya hivi karibuni kwani hawajatwaa ubingwa wa ligi ya Misri kwa miaka saba sasa huu wa 2012 ukiwa wa nane na mara ya mwisho walionja ladha ya ubingwa huo mwaka 2004. Mwezi uliopita tu bodi ya uongozi wa Zamalek ilisitisha kazi ya Hossam Hassan kama kocha baada ya miaka miwili isiyokuwa na mafanikio na nafasi yake ikachukuliwa na gwiji wa klabu hii pamoja na timu ya taifa ya Misri Hassan Shehata ambaye ndiye amepewa jukumu la kumaliza ukame wa Zamalek kwenye soka la nyumbani na la kimataifa.
Msimu huu ulioisha safari ya Zamalek kwenye klabu bingwa ya Afrika iliishia kwenye hatua za awali kabisa mikononi mwa Club Africain ya Tunisia .
Tangu Shehata aingie kwenye benchi la Zamalek hali inaonekana kubadilika na wachezaji wanacheza kwa furaha tofauti na kipindi cha Hossam ambapo klabu hii ilikuwa inaoenekana kukosa muelekeo . Kwenye ligi Zamalek wana rekodi ya kushinda michezo minne kati ya mitano iliyopita wa mwisho ukiwa Alhamis iliyopita ambapo vijana wa Shehata waliifunga El Dakley 2-1.
Shehata amewarudisha washambuliaji mahiri wa timu ya taifa ya Misri ambao kwa muda waliwahi kucheza Zamalek Amr Zaki pamoja na Ahmed Hossam Mido ambao walikuwa barani ulaya kwa vipindi tofauti .Ukiwaacha hao , Zamalek pia inao wakali kama Razak Omotoyosi ambaye anatoka Benin pamoja na mtu ambaye wengi wanamtazama kama mchezaji bora wa misri katika miaka mitano iliyopita lakini hajawahi kupewa nafasi kwenye timu ya taifa Mahmoud El Razak Shikabala .
Hakuna anayeweza kusema kuwa Yanga watafungwa kirahisi na Zamalek kwani huenda rekodi ya mwaka 2003 ikajirudia na Zamalek ikatolewa na timu toka Tanzania lakini kinachobaki kama ukweli kwa Yanga ni kimoja tu kuichukulia michezo miwili dhidi ya Zamalek kama kozi muhimu ya mafunzo ya jinsi ya kuendesha soka kisasa na kuachana na mambo ya kizamani ambayo yanarudisha soka nyuma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment