Mshambuliaji Emmanuel Okwi wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ amekataa heshima ya kutambulishwa kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa maelezo kwamba hastahili hadhi hiyo.
Akizungumza jana, Okwi aliyeng’ara katika michuano hiyo na kufunga mabao yaliyoipa nchi yake taji la 12 la Chalenji, alisema kwamba yeye alifunga mabao manne tu na hivyo waliostahili kuitwa ‘wafungaji bora’ wa michuano hiyo ni Warwanda Olivier Karekezi na Meddie Kagere waliofunga mabao matano kila mmoja.
Awali, ilielezwa baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali ambayo Uganda walishinda kwa penati 3-2 dhidi ya Rwanda kuwa Okwi, Karekezi na Kagere ndio wafungaji bora baada ya kila mmoja kupachika mabao matano.
Okwi alisema kuwa takwimu hizo si sahihi kwani yeye alifunga mabao manne tu; matatu aliyafunga katika mechi moja ya hatua ya makundi dhidi ya Somalia na jingine ‘alimdungua’ kipa anayecheza naye Simba, Juma Kaseja wa wenyeji Kilimanjaro Stars wakati walipokutana katika mechi yao kali ya nusu fainali.
"Kama wamenijumuisha katika orodha ya wafungaji bora watakuwa wamekosea... mimi nilifunga magoli manne tu. Ila wenzangu (Karekezi na Kagere) wana magoli matano kila mmoja na ndio waliostahili tuzo ya ufungaji bora," alisema Okwi.
No comments:
Post a Comment