Search This Blog

Tuesday, December 13, 2011

RAGE: WAVIVU NA WATOVU NIDHAMU KUTOVUMILIWA SIMBA


WACHEZAJI wavivu na watovu wa nidhamu hawatakuwa na nafasi katika kikosi cha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirvociv, raia wa Serbia, ambaye amewasilisha rasmi ratiba yake ya kazi kwa uongozi juzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema katika programu ya kocha huyo aliyowasilisha kwa Kamati ya Ufundi ameweka wazi kuwa hatawavumilia wachezaji wavivu na watovu wa nidhamu.

Alisema kuwa kocha huyo amebainisha kuwa atakuwa na mazoezi magumu ili kuwandaa vijana wake kwa ngwe ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

“Tumeipokea ratiba ya CAF na pia tunafurahi kwamba kocha wetu, Milovan, ameshatupatia proramu yake huku akisema hatawavumilia wachezaji wavivu na watovu wa nidhamu bali atawatimua kwa kuwa anataka kuiimarisha Simba, na sisi tutamkubalia kwa hilo,” alisema Rage.

Alisema Simba inapigania kuwavua Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na pia inataka kufanya vizuri kwenye michuano ya Shirikisho, hivyo itamuunga mkono kocha huyo.

Kwenye michezo ya Shirikisho Simba imepangwa kuanza kampeni yake kwa kucheza na Kiyovu ya Rwanda, mchezo utakaopigwa mjini Kigali, Rwanda kati ya Februari 17 na 19 mwakani na mchezo wa marudiano utapigwa jijini Dar es Salaam kati ya Machi 2 na 4, 2012.

No comments:

Post a Comment