Chelsea 3-5 Arsenal:
Vikosi vilivyoanza.
Chelsea walionekana kuwa na mapungufu dhahiri kabla hata ya mchezo kuanza –safu ya ulinzi ya timu hii chini ya AVB imekua ikikabia sehemu ya juu ya uwanja na kwa hili wanakuwa hatarinikukamatwa hasa pale wanapocheza na timu ambayo inatumia mchezo wa kasi kama Arsenal .
AVB alimuanzisha Branislav Ivanovic badala ya David Luiz ambaye amekuwa akiigharimu Chelsea kwa siku za hivi karibuni. John Obi Mikel alicheza katikati mwa uwanja badala ya Raul Meireles na kwenye nafasi nyingine hakukuwa mabadiliko kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya QPR .
Arsene Wenger kwa upande wake aliendelea kumtumia Johan Djourou upande wa kulia na Thomas Vermaelen alikuwa benchi japo alikuwa fit. Huu ulikuwa mchezo ambao ulikuwa na nafasi nyingi sana na kulikuwa na mapungufu mengi kwenye safu za ulinzi za timu zote na mwisho wa siku ilikuwa Arsenal waliowaadhibu wenzao kwa makosa waliyofanya .
Mabadiliko ya kimajukumu .
Jambo la kufurahisha kwenye mchezo huu ilikuwa tofauti ya mifumo ambayo timu hizi iliitumia . Kwa kuutazama kwa jicho la ziada utaona kuwa timu hizi ziliingia taofauti na ambavyo zimekuwa siku za nyuma . Kwa misimu miwili mitatu iliyopita , matokeo ya mchezo huu yamekuwa yakitabirika kirahisi .
Arsenal humiliki sana mpira na Chelsea hukaa na kushambulia kwa kushtukiza na mara nyingi walikuwa wakishinda iwe nyumbani ama ugenini.
Kwenye mchezo huu mambo kidogo yalibadilika. Chelsea walimiliki sana mpira na Arsenal walicheza moja kwa moja kuliko ilivyo kawaida yao . Wenger alikiri hili kwenye mahojiano ya baada ya mchezo akisema Chelsea kiukweli walikuwa wabunifu kwenye mchezo huu kuliko timu yake. Sababu kuu ya hili ilikuwa ‘presence’ ya Juan Mata. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni usingewahi kuona jambo kama hili kwenye Chelsea za kina Mourinho na kina Ancelotti na chini ya AVB Chelsea imeonekana kubadilika sana .
Mstari wa juu wa mabeki.
Jambo ambalo liliuamua mchezo ni jinsi Chelsea walivyokuwa wakijilinda kwa kutumia mstari unaokabia juu au nje badala ya chini au ndani. Dhidi ya timu kama Arsenal hili ni tatizo kubwa hususan unapokuwa na mabeki kama John Terry ambao hawana kasi – Arsenal walitumia tatizo hili kwa faida yao na wakashinda bila tabu kama ubao wa matokeo ulivyoonyesha.
Kwa jinsi mchezo ulivyoenda Arsenal wangeweza kufunga mabao mengine matano juu ya yale waliyoyafunga kwa kupiga tu mipira ya juu ambayo ingewapita kina Terry na kuwapa nafasi mawinga wenye mbio Gervinho na Walcott ya kufunga.
Gervinho alikosa bao la wazi kipindi cha kwanza kwa hivi hivi angekuwa makini zaidi pengine angefunga. Tatizo hili halikuishia hapa na liliendelea kwa muda mrefu . Bao la kwanza lilifungwa baada ya Gervinho kupita akiwa peke yake pasipo kupewa bugudha.
Bao la Walcot lilifungwa wakati alipokuwa na nafasi ya kupita katikati ya msitu wa mabeki. Makosa ya mabeki yalichangia bao la pili , mshambuliaji Daniel Sturidge alizembea kumkaba Andre Santos na kwenye bao la nne muunganiko wa pasi isiyotarajiwa ya Malouda na kuanguka kwa John Terry.
AVB aakichambua mchezo alisema kuwa bao la tano lilifungwa kufuatia timu yake kuwa na mzuka wa kushambulia kujaribu kusawazisha na hivyo kujiacha wazi na katika hali kama hiyo bao hilo lisingeweza kuzuilika.
Lakini huwezi kuzuia ukweli kuwa mabao yote haya yalitokana na jinsi Arsenal walivyoweza kutumia nafasi kubwa iliyokuwepo katikati ya mstari wa mabeki wa Chelsea na Kipa wao na ndio maana mabao mengi ni kama yalikuwa kwenye hali ya 1 vs 1 kati ya mfungaji na kipa.
Mienendo / movement za Chelsea
Huwezi kusahau kuwa Chelsea walitengeneza nafasi za kutosha wao kama wao –na ndio maana wakafunga mabao matatu na wangeweza kufunga zaidi ya hayo kama isingalikuwa bahati mbaya hususan Wakati matokeo yakiwa 0-0. Inaonekana kuwa AVB alikuwa anajua tishio la kasi ya mawinga wa Chelsea lakini bado akaamua kukabia ndani juu na pia hakukuwa na presha yoyote kwa Gervinho na Walcott na ndio maana walitamba sana kwenye mchezo huu.
Moja ya mambo muhimu ambayo yamekuwa yakitokea kwenye michezo mbalimbali ya Arsenal na Chelsea ni performance nzuri ya Ashley Cole hususani jinsi anavyompa tabu mtu anayechezakama Winga na kutoa krosi muhimu . Kulikuwa na ishara za jambo hili kujirudia kwani ilitokea mara mbili ndani ya dakika tano za mwanzo – Djorou alionekana kupotea alipokuwa akicheza beki ya pembeni na ndio maana Cole akapata mwanya lakini baadae Walcott alitambua hili na alirudi na kusaidia kum-neutralise Cole na kumfanya asiwe na madhara yoyote .
Wakati mwingine hali ilipolazimu Jon Obi Mikel alikuwa akirudi nyuma na kuwa kama beki wa kati wa ziada ili kuwaruhusu mabeki wa pembeni wapande kusaidia mashambulizi. Daniel Sturidge alikuwa akiwapa tabu mabeki wa Arsenal na alifanikiwa kwani positioning ya Andre Santos haikuwa nzuri.
Ukabaji mbovu wa Santos ulionekana kwenye bao la Lampard ambapo alikubali kupitwa kirahisi na Juan Matta ambapo mhispania alisogea pembeni na kumpita beki huyu wa kibrazil . Ni vigumu kusema kuwa mabeki wa pembeni wa timu zote waliwapa tabu mawinga wao timu pinzani – mabeki wa pembeni wa Arsenal hawakuwa wakijipanga vizuri na wa Chelsea walikosa kasi na walikuwa wakipitwa kirahisi kwenye mipira ya kufukuza. Katikati ya kiwanja hakukuwa na vita kubwa na kama ilivyosemwa awali kuwa Chelsea walimiliki sana lakini walishindwa mwishoni.
Jinsi mchezo ulivyoendelea.
Hakuna anayeelewa jinsi kibao kilivyogeuka kadri muda ulivyoenda kuanzia 0-0 , 1-0 , 1-1 , 2-1, 2-2, 2-3, 3-3 , halafu 3-4 na mwisho wa siku ukaisha kuwa 3-5. Mojawapo ya sababu kuuilikuwa jinsi mchezo ulivyokuwa wazi na kasi ambayo ulikuwa ukichezwa – mchezo muda wote ulikuwa wa kasi na mara pekee ambapo kasi ilipungua na ilikuwa kwa mara chache na nadra sana pale ambapo Aron Ramsay na mikael Arteta walipopata mpira wakajaribu tena bila mafanikio kutuliza mchezo. Zaidi ya hapo mchezo ulikuwa wa kasi kubwa na timu zote zilionekana kuwa na njaa ya mabao .
Hali ilibadilika baada ya matokeo kuwa 2-3 , japo hakuna muda wowote ambapo mchezo ulikuwa umetuama kwenye matokeo husika . AVB alifanya mabadiliko matatu ya msingi sana kwa timu yake na baada ya hapo Chelsea walionekana kupitisha mpira kirahisi kidogo na kwa kasi. Mabadiliko hayo yalisaidia kuwapa Chelsea moyo wa kurudi kwenye mchezo kwani hadi kufikia dakika ya 80 matokeo yalikuwa sare na karibu kila mtu aliamini kuwa yangeisha hivyo. Jambo la msingi ni kwamba kadri Chelsea walivyopata moyo wa kurudi mchezoni ndio walivyojiacha wazi nyuma na iliwagharimu mwishoni .
Wakati huo huo upande wa Chelsea hawakutengeneza nafasi nyingi kabla ya bao la Mata ambalo ukiacha ukweli kuwa lilikuwa bao la shuti la mbali halikuwa na ufundi wowote unaoweza kusema limetengenezwa. Arsenal walifunga walipata bao la nne kupitia makosa ya Terry na Malouda na wakati walipomtoa Walcott kumuingiza Rosicky ilionekana kuwa kuna aiana ya mchezo wa kumiliki mpira pasipo kushambulia waliokuwa wanataka kuuleta lakini haikuwa hivyo.
Mwisho
Matatizo ya ulinzi ya Arsenal bado yako dhahiri na ndio maana walifungwa mabao matatu na hili bado ni tatizo ambalo wanapaswa kulitatua . Mwisho wa siku walishinda na walishinda kwa akili. Walitumia kasi ambayo ilikuwa udhaifu wa Chelsea na pia walicheza soka la moja kwa moja ambalo walistahili kupata ushindi kwa kutambua mbinu ya kutumia kupata ushindi .
Huu ni ushindi mzuri na muhimu kwa Arsenal na kubwa katika hili ni jinsi ushindi wenyewe na mabao yalivyokuwa yakifungwa. Hadi kufikia hatua hii Arsenal hawajapata ushindi wowote unaoonyesha maendeleo kwa timu yao hususan maendeleo ambapo wameonyesha kubadili mtindo wao kucheza lakini dhidi ya Chelsea walifanya hivyo na hapa mabadiliko ya kuondoka kwa kina Nasri na Fabregas yanaoenekana kwani ushindi dhidi ya Chelsea ulipatikana kwa kuwatumia vilivyo kina Walcott na Gervinho.
Hata hivyo mchezo walioonyesha dhidi ya Chelsea unaonekana kuwa na matokeo positive kuliko mitindo mingine, kwani hili ndio hasa soka la Uingereza na mara nyingi Arsenal huwa wanaonekana kufanya majaribio ya kuwa Barcelona nyingine lakini huu ni mfumo ambao umeonekana kushindwa England.
Endapo Arsenal waterejea kwenye soka lao zamani kwenye mchezo unaofuata usishangae kuona wakipata matokeo mabaya kwani ni aina ya soka ambalo linaonyesha kuwa limezoeleka toka kwao na pia Arsenal haijakamilika kwa kuutumia mfumo huu kama ilivyo kwa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania .
AVB atajitetea juu ya timu yake kutumia mstari wa mabeki wanaokabia juu sana. Kwa jinsi mchezo ulivyoenda huu sio mtindo unaoweza kufanya kazi kwenye mazingira ya soka laEngland.Inaonekana kuwa anapenda kuiona Chelsea ikicheza soka la aina hii kwa muda mrefu lakini wachezaji alionao kwenye safu yake ya ushambuliaji hawawezi kufanya vizuri kwa falsafa yake anayopenda kuitumia na kama Chelsea wataendelea hivi watapatatabu sana msimu huu.
No comments:
Post a Comment