Search This Blog

Wednesday, October 26, 2011

KIBADEN AIENDEA YANGA & UBINGWA HIJJA


Team manager wa Wekundu wa Msimbazi, Simba, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, anatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam leo kwenda safari ya hija jijini Makkah, Saudi Arabia.

Kibadeni amewaahidi wapenzi pamoja na mashabiki wa Simba kuwa atamwomba Mungu timu hiyo itwae ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2011/2012 na Afrika.

Akizungumza na tovuti ya Simba, www.simba.co.tz jijini Dar es Salaam jana, Kibadeni alisema anashukuru kwamba anakwenda kuhiji Maka akiwa anatoka katika ajira yake Simba.

“Katika safari yangu ya hija, zaidi ya mambo mengine nitakayoyaombea, nitaomba pia kwamba Mungu aijalie Simba itwae ubingwa wa Tanzania msimu huu na pia ule wa michuano ya CAF kwa vile naamini timu nzuri tunayo,” alisema Kibadeni.

Kibadeni ni muumini wa dini ya Kiislamu na hija ni mojawapo ya nguzo tano au misingi ya dini hiyo.

Meneja huyo, ambaye pia ni miongoni mwa wachezaji bora wa wakati wote wa Wekundu wa Msimbazi, atakuwa Maka kwa takriban wiki tatu.

Anaondoka katika kipindi cha kuelekea pambano la watani wa jadi, linalotarajiwa kupigwa Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa, jijini.

Kuhusu pambano hilo, Kibadeni alisema ana matumaini makubwa kuwa Simba itaibuka kidedea na kujitwalia pointi tatu muhimu na hatimaye kuwa mabingwa msimu huu.

Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kipindi ambacho Kibaden hatakuwa na timu, nafasi yake itashikiliwa na nahodha wa zamani wa Simba, Nicholaus Menrad Nyagawa.

Kamwaga alisema wao hawana hofu na mechi hiyo dhidi ya watani zao Yanga kwa kuwa maandalizi yao yako kamili na wataendeleza kambi katika ufukwe wa Bamba ulioko Kigamboni.

“Imekuwa ikizushwa kuwa Simba inaenda kambi Zanzibar sio kweli sisi tunabaki Bamba tukifanya mabadiliko ya kambi tutasema kwa nini tufiche, tulienda Zanzibar, Arusha tukaseme iweje sasa tufiche,” alisema Kamwaga.

No comments:

Post a Comment