Search This Blog

Wednesday, October 26, 2011

RAZACK KHALFAN NA WENGINE WANNE KUFUATA NYAYO ZA NGASSA SEATTLE SOUNDERS


Klabu ya soka ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam inatarajia kuwapeleka wachezaji wake watano katika klabu ya Seattle Sounders ya Marekani kufanya majaribio kucheza soka la kulipwa.

Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa timu hiyo, Rahim Kangezi aliwataja wachezaji hao kuwa ni Jarufu Kizombi (U-18), Hamis Thabit (U-20), Abdul Seif (U-23), Razack Khalfan na Mganda Hood Mayanja.

"Hamis Thabit yeye ataondoka kesho kwa majaribio ya wiki mbili katika Taasisi ya kulea na kukuza vipaji ya Seattle Sounders, wengine wataondoka mapema mwezi ujao," alisema Kangezi.Alisema endapo atafaulu mtihani huo, chipukizi huyo aliyewahi kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa nia ya kupata uzoefu ataingia mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo.

Hata hivyo, alisema mchezaji Jarufu Kizombi (U-18) mshindi wa Tamasha Serengeti soka Bonanza lililofanyika jijini Mwanza mapema Juni amepata fursa adimu kujiunga chuo cha Louisiana kujiendeleza kielimu muda wa miaka mitatu.
Kizombi ambaye ni yatima ameushukuru uongozi wa timu hiyo kumpatia nafasi ya kujiendeleza kimasomo katika chuo cha Louisiana Marekani.

"Naushukuru uongozi wa Lyon kunipatia nafasi hii adimu, naahidi kuiwakilisha vyema nchi yangu na familia yangu," alisema Kizombi.Naye Thabit alisema atahakikisha anajituma pamoja nidhamu ili kuhakikisha anafuzu majaribio hayo.

No comments:

Post a Comment