Search This Blog

Sunday, September 4, 2011

TAIFA STARS ILICHEZA VIPI DHIDI YA ALGERIA

Taifa Stars imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Algeria katika mchezo wa kutafuta nafasi ya kucheza kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2012 litakalofanyika Gabon na Equatorial Guinea. Wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi walionekana kung’aa sana kuliko wenzao kwenye mchezo huu. Tutazame jinsi wachezaji hawa walivyocheza kila mmoja kwa ubinafsi wake .




1: Juma Kaseja.




Mwanzoni alionekana kuwapanga vizuri mabeki wake kama ilivyo kawaida yake , akiwapigia kelele na kuwapongeza katika nyakati tofauti kadri ilivyostahili . Kazi yake nzuri iliharibiwa na jinsi mabeki wake wa kati Aggrey Morris na Juma Nyosso walivyomuangusha kwa kushindwa kuusoma mchezo na kuruhusu bao la kusawazisha , kwenye kipindi cha kwanza hakuwa mchezoni sana kwa kuwa muda mrefu mchezo ulitawaliwa na Taifa Stars na kwenye kipindi cha pili kwa nyakati tofauti alikuwa akitoka na kuipanga safu yake ya mabeki vyema hasa baada ya kufungwa bao .







2: Shadrack Nsajigwa.




Huu ulikuwa mchezo mgumu sana kwake kwa kuwa alionekana kupambana sana mpaka kufikia kuchoka . Nsajigwa ni mtu ambaye silaha yake kubwa ni nguvu nyingi na juhudi binafsi . Kwa jinsi alivyocheza dhidi ya Algeria alionekana kuchoka sana na hili lilikuwa dhahiri kipindi cha pili kwa kuwa Algeria kama ilivyo kawaida kwa timu za uarabuni huwa wanabadilika na kasi ya mchezo na walitumia sana upande wake kwa kuwa waliona kabisa kuwa umelemewa na mara nyingi kiungo Nizar Khalfan alikuwa anakuja kumpa tafu . Pengine ni ishara kwa kocha kuanza kumtafuta mbadala wa kaka fusso mapema kwani anaonekana kuwa mbali na siku zake za kuisaida timu ya taifa kama mchezaji kamili wa kimataifa , umefikia wakati kwake kuchagua kupunguza uzito wa timu ya taifa na kubaki na klabu yake ya Yanga .







3: Amir Maftah.




Kwa uwezo wa asili Amir ni moja ya wachezaji wenye uwezo mkubwa sana na kipaji halisi . Tatizo kubwa la Amir ni ‘mambo’ yake mengi aliyo nayo anapokuwa uwanjani , mambo ambayo yanamfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake ya msingi kama beki wa pembeni . Kwa kawaida beki wa pembeni hupaswa kuipandisha timu na kurudi kukaba lakini Amir hupanda sana na anajisahau na hili linampunguzia alama kwa watu wanaosoma mchezo wake . kwa mchezo dhidi ya Algeria alicheza vyema lakini tatizo hili lilionekana .




4: Juma Nyoso.




Moja ya mabeki shupavu ambao nchi hii inao kwa sasa. Anajua sana kukaba na pale anapocheza na mtu anayejua jinsi ya kumtuma na kumuelekeza cha kufanya basi Nyoso ni namba 4 mzuri sana . Tatizo lake ambalo linaonekana anapoichezea timu ya taifa ni uwezo wake mdogo wa kuusoma mchezo . Mara nyingi sana huwa anaingiliana na beki mwenzie na pia ana tatizo la kutegea hali ambayo ilisababisha bao la kusawazisha ambapo yeye na beki mwenzie na hasa yeye kwa kuwa alikuwa mkabaji huku mwenzie akisimama kwenye ‘free role’ walishindwa kusoma malengo ya wapinzani wao . Laiti kama Nyoso angeelewa haraka anachokuja kufanya Bouazza angemkaba ‘zero distance’ na pengine bao la kusawazisha lisingetokea .




5: Aggrey Morris.




Ni moja ya mabeki wenye umakini wa hali ya juu sana . Wakati Victor Costa alipoumia na kukaa nje kwa muda mrefu mbadala wake alikuwa mtu huyu . Pengine uzoefu mdogo wa michezo ya kimataifa umemhukumu kwenye mechi dhidi ya Algeria kwani yeye kama ilivyo kwa Nyosso anaingia lawamani kwa kuruhusu goli kupita kwenye njia aliyopaswa kuilinda kama beki . Labda si kwa kuwepo kama ‘man-marker’ lakini kwa kumuelekeza mwenzie ambaye kukaba ndio jukumu lake kufanya hivyo.




6: Henry Joseph.




Alicheza vizuri kwenye eneo lake hasa kwenye kipindi cha kwanza lakini baadae alionekana kulemewa hasa baada ya wimbi la mchezo kugeukia upande wa timu yake pale ambapo Algeria walifanya mabadiliko ambayo yalifanya kasi ya mchezo kubadilika kabisa na hivyo kuonekana amechoka . Bado anaendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye timu hii ya taifa.




7: Nizar Khalfan.




Kama Taifa stars ingeshinda mchezo huu basi Nizar alipaswa kuwa Man Of The Match kuwa kuwa alionyesha ukomavu wake kama ‘proffessional player’. Nizar alikuwa akitimzia majukumu yake ipasavyo na hata kusaidia wenzie ambao walionekana kuelemewa kama ilivyokuwa kwa Nsajigwa.Pasi yake ilisababisha goli lililowekwa wavuni na Mbwana Samatta zaidi ya hapo alionyesha kujituma kwa aina yake na pia hakuwa anapoteza pasi kizembe na hata ilipotokea kafanya hivyo basi alihakikisha anahangaika na kuupata tena . Nizar ni lulu ambayo Taifa Stars inajivunia kuwa nayo .




8: Shabaan Nditi.




Uzoefu wake umeendelea kumlinda kwenye nafasi anayocheza , japo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Athumani Machupa alionekana kucheza vizuri akiituliza timu na kuiendesha ipasavyo , tatizo lake ni kuwa na mtazamo mmoja kwenye mchezo wake na pia kukosa kasi ambayo labda inasababishwa na umri wake kuwa mkubwa lakini bado uzoefu wake ni wa thamani kubwa kwenye timu .




9: Mbwana Samatta.




Ndiye mchezaji bora ambaye Taifa Stars inaweza kujivunia kuwa naye . Mbwana ana sifa nyingi za mchezaji aliyekamilika kwa nafasi yake . Ameendeleza rekodi yake nzuri ya kufunga kwenye kila mechi ‘competitive’ ya Taifa Stars ambayo amecheza . Kiwango chake bado kipo juu sana japo ana mengi ya kujifunza kama vile kuweka akili yake mchezoni muda wote na si pale mpira unapokuwa mguuni kwake tu . Ana uwezo mkubwa sana kwa kuwa ni mfungaji mzuri na ni mtengenzaji mzuri kwa wenzie . Ni mtu ambaye Taifa Stars inamtazama kama mwokozi wa sasa na kwa muda mrefu ujao.




10: Danny Mrwanda .




Kama ilivyokuwa kwa wachezaji wenzie toka nje ya nchi alicheza vizuri huku akijituma sana kutokana na uzoefu alio nao wa kucheza Taifa Stars kwa muda mrefu na pia kucheza nje ya nchi. Danny ni mpambanaji na hilo lilionekana kwenye mchezo dhidi ya Ageria kwani alikuwa hakubali kirahisi pale alipokuwa akikumbana na miili ya kina Hassan Yebda , Karim Ziani na wengine ambao wana miiili iliyomzidi . Hakumaliza dakika 90 lakini kwa zile chache alizocheza alionyesha uwezo mkubwa.




11: Abdi Kassim .




Kwa muda mrefu Abdi amekuwa nje ya timu ya Jan Poulsen lakini alirejea kwenye mchezo dhidi ya Algeria . Alionyesha uwezo wake aliozoeleka nao na pia ukomavu wa kuwa mchezaji wa kimataifa ulionekana, alikuwa akipiga mipira yake ya mbali kama kawaida yake . Kwenye kipindi cha pili alipiga ‘free kick’ moja ambayo almanusra iwe bao la pili kama si umahiri wa mlinda lango wa Algeria . Baadaye alionekana kuchoka na kuwa kwenye kasi tofauti na ile ya mchezo .




Wachezaji Walioingia.




Mrisho Ngassa aliingia kuchukua nafasi ya Danny Mrwanda , kwa dakika chache alizoingia alibadili mpira kidogo japo wachezaji wa Algeria walimsoma na kumdhibiti kirahisi . Aliwahadaa wapinzani kwa chenga zake lakini mawasiliano mabovu baina yake na wenzie yaliinyima Stars magoli na pia uwezo wake mdogo wa kupiga mashuti ya mbali ulikuwa tatizo kwani alikuwa anapata nafasi za kupiga mashuti na aliishia kutoa pasi kwa kuwa hana uwezo wa kupiga .







Athumani Machupa.




Alipata dakika 13 tu za kuonyesha uwezo wake na sio zaidi ya hapo. Hakukugusa mpira mara zaidi ya tano na mara nyingi alikuwa akikimbiza vivuli vya mabeki wa Algeria , pengine swali la kuwauliza TFF kwanini mchezaji anatoka Sweden na kuja kucheza dakika 13 tu?








No comments:

Post a Comment