Timu ya taifa ya Tanzania imecheeza dhidi ya Algeria mchezo ambao umeisha kwa sare ya bao moja kwa moja .
Mwanzoni mchezo ulionekana kama umetawaliwa na watanzania kwa kiasi kikubwa hasa ukizingatia kuwa uwanjani walikuwepo wachezaji wasiopungua watano ambao wanaocheza soka la kimataifa kwa upande wa Tanzania , kingine ambacho kilionekana labda kuwachagiza wachezaji wa Tanzania kucheza vizuri ilikuwa umuhimu wa mechi yenyewe ambapo Tanzania ilikuwa na pointi 4 ikihitaji ushindi na kutazama matokeo ya mechi kati ya Moroco na Jamhuri ya Afrika ya kati ili kufufua matumaini ya kufuzu kwa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika .
Wachezaji wa Stars walionekna kuonana vizuri kipindi cha kwanza huku wachezaji wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakionekana kung’aa sana hasa Nizar Khalfan na Mbwana Sammata ambao walishirikiana kuipa Stars bao la kuongoza huku Mbwanna Sammata akifunga bao lake la nne katika mchezo wake wanne akiwa na timu ya taifa ya wakubwa .
Kulikuwa na maelewano mazuri sana baina ya mabeki wawili wa kati kwenye kipindi cha kwanza na hili lilichangiwa na Walgeria kutumia kipindi hicho kuwasoma wapinzani wao na kutumia kipindi cha pili kama wakati wao wa kutawala mchezo , na pia Mlinda lango Juma Kaseja alikuwa salama na maelekezo yake kwa mabeki wake kwenye jinsi ya kujipanga na kukaba yalionekana kueleweka sana .
Wakati kipindi cha kwanza kilipoisha mchezaji wa Algeria anayecheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Milwall Hamer Bouzza aliamka kwenye benchi na kwenda kupasha misuli moto uwanjani huku wenzie wakienda kwenye chumba cha kubadili nguo , mwalimu msaidizi wa Algeria alionekana akimpa maelekezo ya peke yake wakati huo huku akiwa karibu nae akionekana kumuonyesha vitu Fulani kutoka kwenye ubao mdogo aliokuwa ameushikilia mkononi.
Hii ilitoa ishara ya kuwa Hamer Bouazza hajakaa benchi kama mchezaji baki wa ziada la hasha bali alikaa benchi kama silaha muhimu ya siri kwa Algeria na Watanzania walitambua hilo dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza kwani huyu jamaa alifunga bao jepesi akitumia uwezo mkubwa wa kusoma mgongano wa mawasiliano baina ya mabeki wawili wa kati Aggrey Morris na Juma Nyosso mgongano wa mawazo uliotokea sambamba na uwezo mdogo wa vijana hawa wa kuusoma mchezo kwenye nafasi yao. Bouazza hakufanya ajizi , aliukwamisha mpira wavuni na kusawazisha kwa upande wa timu yake huku akiwaacha watanzania 11 uwanjani na wengine takribani 30,000 kwenye majukwaa wakiwa hawana la kufanya huku wengine wakimtupia lawama mwamuzi kwa kudhani labda mfungaji aliotea lakini hakuwa ameotea na lilikuwa bao safi.
Mwalimu wa Taifa Stars Jan Poulsen alifanya mabadiliko kwa kumtoa Danny mrwanda na kumuingiza Mrisho Ngassa . Mabadiliko haya yalikuwa na walakini ndani yake kwa sababu kuu mbili . Kwanza Mrwanda hakuwa amechoka na alikuwa akielewana vyema tu na wenzie huku tatizo pekee lililokuwa likimkabili likiwa kimo kidogo huku akipambana na wapinzani wenye vimo vikubwa hali iliyokuwa inamlazimu kutumia nguvu nyingi ambazo zilikuwa zikitumiwa na Walgeria kujiangusha na kupata faulo nyingi. Pili kama mwalimu alifanya mabadiliko kwa kuzingatia tatizo hili basi hakulisuluhisha kwa kumuingiza Ngassa ambaye kama ilivyo kwa Mrwanda hana kimo zaidi tu ya kuinyima timu mtu ambaye ana uwezo wa kupiga mashuti na kumuingiza mtu ambaye hakuwa na uwezo wa kupiga mashuti na hivyo kuinyima timu mabao ambayo pengine yangewezwa kwa mtindo huu.
Kulikuwa na mabadiliko mengine ambapo Shaban Nditi alitolewa na akaingia Athumani Machupa, labda ingeeleweka kama kwenye nafasi ya Mrwanda angeingia machupa na si Ngassa . Kwa mtazamo wa kiufundi ingekuwa na faida kama labda angepumzishwa Abdi Kassim Babi na si Mrwanda .
Kwa upande wa wapinzani mabadiliko yaliyofanywa yalikuwa makini na yaliyozingatia utaalamu mkubwa wa kuusoma mchezo na nini kilihitajika kutoka kwenye mchezo huo . Aliingia Bouazza ambaye ni mfungaji na alifanya kazi yake kwa kufunga goli na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga lakini aliingia mchezaji mwingine aliyekuwa ameletwa ili kusaidia umiliki wa mpira ambao Algeria walikuwa nyuma kipindi cha kwanza na hilo kweli lilitokea kwani Algeria walimiliki mpira kipindi cha pili .
Wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza nje ya nchi walikuwa kivutio kikubwa kwa jinsi walivyoonyesha mabadiliko makubwa yanayoleta matumaini kwa upande wa Tiafa Stars . Wote kwa pamoja wlaionekana kuleta kitu tofauti kwenye timu huku wakijaribu kutumia uzoefu wanaoupata kutoka huko wanakocheza.
Upande wa mtu aliyeonekana kulemewa kidogo na mechi ilikuwa kwa nahodha na kaka mkuu wa timu Shadrack Nsajigwa Fusso ambaye kidogo alionekana kuwa na kasi tofauti na ile ya mchezo kwa ujumala , ya wenzie kwenye timu nay a wapinzani. Labda ni uchovu unaotokana na kucheza mechi nyingi kwenye kipindi kifupi pasipo kupumzika lakini pengine saa imeanza kusoma tofauti kidogo yaani pengine umefikia wakati wa kupumzika kwa majukumu ya kuichezea timu ya taifa kwa mkongwe huyu.
Kwa jinsi timu ilivyocheza kwanza faida kubwa ya kucheza nje ya nchi imeonekana nap engine hii ni changamoto kwa viongozi wa timu kuwa wepesi wa kuwatafutia wachezaji wao wanaocheza hapa nyumbani timu za kucheza nje ya nchi lakini tatizo kubwa limeendelea kuwa kukosa umakini mchezoni na hili ni tatizo litakaloendelea kuihukumu timu ya tiafa ya Tanzania . Kipindi cha pili kuna nafsi kama tatu za uhakika za kufunga zilizotengenezwa lakini kwanini wavu haukucheka ni wachezaji wa Taifa stars tu ndio wanaojua lakini kama umakini ungekuwepo ubao wa matokeo ungesoma tofauti kidogo.
No comments:
Post a Comment