Zachary Baraje |
Mabingwa mara mbili wa Afrika, klabu ya Enyimba ya Nigeria imemsimamisha kazi kocha wake mkuu Zachary Baraje na msaidizi wake Odigie kwa muda usiojulikana.
Maamuzi hayo yamekuja baada ya timu hiyo kupoteza mechi mbili mfufulizo za ligi kuu nchini humo ukiwemo ule wa kufungwa bao 1-0 na wapinzani wao wakubwa Abia Warriors uwanja wa nyumbani.
Baraje ameifundisha timu hiyo kwa miezi minne tu tangu apewe kibarua hicho mwezi Desemba mwaka jana.
Kocha huyo wa zamani wa Dolphins ameiongoza Enyimba katika michezo sabu tu katika michuano ya ligi ya mabingwa na ligi kuu nchini Nigeria ambapo kashinda mechi tatu, kapoteza tatu na kutoa sare moja.
Lakini bado Enyimba hawajatangaza rasmi maamuzi ya kuachana na kocha wake huyo na msaidizi wakati huu wakijiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Warri Wolves.
"Makocha Baraje na Monday Odigie hawatakuwa sehemu ya benchi la ufundi mechi ijayo. Klabu imewasimamisha lakini kutangaza kiofisi bado. Maamuzi hayo yametokana na timu kufanya kushindwa kupata ushindi nyumbani, hata hivyo ilicheza chini ya kiwango. Kiukweli wamefanya vibaya tangu kuanza kwa msimu huu". Wamesema maofisa wa Enyimba walipokuwa wakizungumza na mtandao wa michezo wa Supersport.com
Mtandao wa Supersport.com ulijaribu kuomba kuzungumza na mwenyekiti wa Enyimba, Felix Anyansi Agwu juu ya maendeleo ya klabu hiyo, lakini alikataa kuzungumza chochote.
"Siko tayari kufanya mahojiano kwasasa". Mwenyekiti wa Enyimba alisema.
Enyimba tayari imeshasafiri kuwafuata Warri wakitokea Taraba bila ya Baraje na Odigie ambapo majukumu yote ameachiwa kocha mwingine msaidizi, Imama Amapakabo kuelekea mchezo huo wa kesho jumatano.
Mwezi wa tatu, Enyimba walimsimamisha kocha wao wa makipa, Shuaibu Suleiman, baada ya kupoteza mchezo nyumbani dhidi ya AS Real de Bamako michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Enyimba kwasasa wanashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi kuu nchini Nigeria baada ya kuambulia pointi 4 tu katika mechi nne walizocheza.
No comments:
Post a Comment