Mtashangilia hivi hivi hapo kesho uwanja wa Taifa dhidi ya wana TamTam Kagera Sugar?
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
MZUNGUKO wa 24 wa ligi kuu soka Tanzania bara kuwania ubingwa unatarajia kuendelea kesho kwa mechi mbili
kupigwa katika miji ya Dar Es salaam na Pwani.
Mabingwa watetezi Dar Young Africans chini ya kocha
mkuu, Mholanzi Hans Van Der Pluijm watatupa
karata yao muhimu dhidi ya wakata miwa wa Kagera Sugar katika dimba la Taifa
jijini Dar Es Salaam.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam fc chini ya bosi,
Mcameroon, Joseph Marius Omog watakuwa na kibarua kizito katika dimba la
Mabatini Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya wenyeji wao, Ruvu Shooting wanaonolewa
na Mkenya Tom Alex Olaba.
Timu za Yanga na Azam fc zipo katika kinyan`anyiro
cha ubingwa na mechi za kesho ni muhimu zaidi kwa timu zote.
Azam fc wanahitaji ushindi kwa nguvu zote ili kuendelea
kujiwekea mazingira mazuri ya kuweka rekodi yao ya kutwaa taji la ligi kuu kwa
mara ya kwanza tangu wapande msimu wa 2008/2009.
Mpaka sasa matajiri hao wa Bongo wapo kileleni kwa
pointi 53 baada ya kushuka dimbani mara 23.
Yanga wanatakiwa kushinda mechi tatu zilizosalia ili
angalau kuwa na matumaini ya kulibakisha kombe la maeneo ya makutano ya Twiga
na Jangwani.
Mpaka sasa kikosi hicho cha Pluijm kimecheza mechi
23 na kujikusanyia pointi 49 kibindoni.
Ushindi kwa Yanga SC katika mchezo wa kesho ni
muhimu mithiri ya dhahabu kwasababu kutawafanya waongeze pointi tatu, huku
wakisikilizia matokeo ya Mabatini.
Kagera Sugar wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa
hawana malengo ya kutwaa ubingwa wala
kushika nafasi ya pili katika msimamo.
Mpaka sasa wamepiga kambin nafasi ya tano wakiwa na
pointi zao 34 baada ya kucheza mechi 23.
Wazee wa kuamua matokeo msimu huu kwa Azam fc, je, kesho watafua `dafu` kwa Ruvu Shooting Mabatini?
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange aliueleza
mtandao huu kuwa malengo yao ni kushinda mechi zote zilizosalia ili kuipata
nafasi ya nne.
Kama kweli watashinda mechi zote tatu watafikisha
pointi 43 ambazo Mbeya City wameshapita
wakiwa nafasi ya tatu.
Kwa maana hiyo Kagera Sugar kwasasa wanaitaka nafasi
ya nne ambayo imekaliwa na Simba SC yenye pointi 37.
Endapo Mnyama Simba sc atashinda mechi mbili zijazo
dhidi ya Ashanti United na Yanga sc atavuna pointi sita na kufikisha pointi 43
kutoka 37 alizonazo sasa.
Msimu wa mwaka jana, Simba sc walishika nafasi ya
tatu, na nafasi ya pili walikuwepo Azam fc, na ubingwa ulichukuliwa na Yanga
sc.
Kagera Sugar wakiwa chini ya kocha mkongwe, Abdallak
Kibadeni `King Mputa` walishika nafasi ya nne baada ya ushindani wa muda mrefu baina
yake na aliyekuwa kocha wa Simba sc kwa wakati ule, Mfaransa Patrick Liewig.
Kama Kagera na Simba sc zitashinda mechi zao zote
zilizosalia, zitafungana pointi na itabidi utofauti wa mabao ya kufunga na
kufungwa utazamwe.
Safari hii timu hizi zimeshuka chini. Sasa zinagombeana
nafasi ya nne kwasababu nafasi ya tatu ipo mikononi mwa Mbeya City ambao pia
wanaweza kushika nafasi ya pili kutegemeana na matokeo ya timu za Yanga na Azam
fc.
Kikosi Kagera Sugar kilichotoa sare ya 1-1 na Simba Kaitaba mechi iliyopita
Mchezo wa Kagera Sugar hapo kesho dhidi ya Yanga
utakuwa na changamoto kubwa kwa timu zote kwasababu kila klabu ina malengo
tofauti.
Yanga wanahitaji ubingwa na Kagera Sugar wanahitaji
nafasi ya nne msimu huu.
Yanga wamekuwa wakiutumia vyema uwanja wake wa
nyumbani, hivyo mpira mzuri unategemewa kuonekana uwanjani.
Hata hivyo itakuwa mechi ngumu kwao kwasababu Kagera
Sugar wana watu wanaoweza kuamua matokeo kwa wakati wowote akiwemo mshambuliaji wao namba moja, Them Felix
`Mnyama`.
Huyu ni mtu wa kuchungwa sana hapo kesho, kwasababu
ukiachiwa nafasi moja anaweza kuwafanya Yanga wawe watumwa.
Hatutegemei mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Yanga kwenye mchezo
huo.
Bila shaka Pluijm atamuanzisha mlinda mlango wake chaguo
la kwanza Deo Munish `Dida`.
Nafasi ya beki wa kulia itategemeana na mipango ya
Mholanzi huyo. Kama Kelvin Yondani ataanzishwa beki ya kati, basi beki wa kulia
anaweza kuanza Mbuyu Twite.
Endapo Yondani hatacheza kesho, basi beki wa kulia
anaweza kuanza tena, Juma Abdul.
Nadir Haroub `Canavaro` kama kawaida lazima ataanza
beki namba nne, huku kitasa akimaliza Mbuyu Twite.
Frank Domayo `Chumvi` atakalia nafasi ya kiungo wa
ulinzi, huku winga wa kulia akianza Saimon Msuva.
Kiungo namba nane anaweza kuanzishwa kinda Hassan
Dilunga.
Mshambuliaji wa kati anaweza kuanza Didier Kavumbagu,
na namba kumi ikiwa mikononi mwa mzee wa `Hat Trick`, Mrisho Khalfan Ngasa.
Winga wa kushoto, Mganda, Hamisi Kiiza `Diego` anaweza
kuanza katika mechi hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa Pluijm.
Hata hivyo Jerryson Tegete, Hussein Javu, Hamis
Thabit ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuanzishwa hapo kesho kutegemeana na
mipango ya kesho.
Lakini kama Haruna Niyonzima atakuwa fiti, basi tutegemee
mabadiliko kwenye kikosi hasa sehemu ya kiungo.
Kwa mechi ya Mabatini, Azam fc watakuwa kwenye
wakati mgumu wa kuwafunga Ruvu Shooting ambao wametamba kuweka rekodi ya kuwa
timu ya kwanza kuwafunga Azam fc msimu huu.
Ruvu Shooting wapo nafasi ya 6 wakiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi
23.
Wao hawana haja ya kutafuta ubingwa wala nafasi tatu
za juu, bali ni kujiwekea heshima kubw aya kukifunga kikosi bora cha Mcameroon
Omog.
Azam fc mpaka sasa hawajafungwa mechi yoyote, na wanahitaji
kushinda mechi mbili tu kati ya tatu walizosaliwa nazo ili kujitangazia ubingwa
msimu huu.
Kama watashinda mechi ya kesho, watahitaji kupiga
hesabu katika michezo miwili ijayo dhidi ya Mbeya City na JKT Ruvu.
Mechi ya Mbeya City sokoine jijini Mbeya itakuwa
ngumu kwa Azam fc kutokana na mazingira ya uwanja huo na rekodi ya wenyeji wao.
City ni washindani wa nafasi ya pili msimu huu,
hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanawafunga Azam fc.
Endapo Azam watawafunga katika mchezo huo, watavunja
rekodi ya Mbeya City ya kutofungwa uwanjani wa Sokoine.
Matokeo kwa Azam ni muhimu kuanzia hapo kesho,
kwasababu hawana uhakika wa kule Mbeya.
Lakini wakirudi Chamazi Aprili 19 dhidi ya JKT Ruvu
wanaweza kuwa na faida ya kushinda kwani huo ndio uwanja wao na wamekuwa na
rekodi nzuri hapo.
Tutegemee ushindani mkubwa hapo kesho kutokana na
ubora wa Ruvu Shooting.
Matokeo yatakayokuwa yanapatikana kadri muda
utakavyokuwa unakwenda katika viwanja hivi viwili, Taifa na Mabatini, ndivyo
ugumu wa mechi utakavyokuwa unaongezeka kwa Yanga na Kagera Sugar.
Kila la heri timu zote katika michezo ya kesho na
waamuzi watakaopangwa kuchezesha wazingatie sheria 17 ili kuepuka tafrani
uwanjani.
Hizo ni mechi muhimu sana kwa klabu zote. Ugumu wake
hautokana na majina ya timu pinzani kwa Yanga na Azam fc, bali ni namna matokeo
yalivyo muhimu kwao.
No comments:
Post a Comment