Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC leo jioni wanacheza mechi yao ya 22 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya wagosi wa Kaya, Coastal Union ya jijini Tanga.
Wakiwa tayari wameshashuka dimbani mara 21 na kujikusanyia pointi 36 katika nafasi ya nne, Simba chini ya kocha mkuu, Mcroatia, Dravko Logarusic wapo katika mazingira magumu zaidi ya kupata matokeo ya ushindi.
Simba SC kama vile wameshajitoa katika mbio za ubingwa na kuwaachia Yanga, Azam na Mbeya city, leo hii watataka kuonesha kuwa ni wakongwe wa soka la Tanzania.
Loga amekuwa na wakati mgumu tangu aanze kukinoa kikosi cha Simba mwanzoni mwa mzunguko wa pili akirithi mikoba ya Abdallah Kibadeni.
Kocha huyo anayesifika kudhibiti nidhamu kwa wachezaji, amekifanya kikosi cha Simba kuwa cha `tia maji tia maji` kwasababu leo kinaweza kupata ushindi na kesho kupoteza mechi.
Wakati Simba wakiwa na malengo ya kuzoa pointi tatu kutoka kwa Coastal Union leo ili angalau kusogea juu kwa kufikisha pointi 39, wagosi wa kaya nao wanahitaji ushindi na kupunguza maumivu ya mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC mechi iliyopita.
Coastal mpaka sasa wapo nafasi ya 7 wakiwa na pointi 26, huku wakisifika kuwa na wachezaji wazuri msimu huu.
Kocha Yusuf Chipo atahitaji kuwapunguzia machungu wapenzi wa klabu hiyo yenye makazi yake jinni Tanga.
Kutokana na umuhimu wa mechi ya leo kwa Simba na Coastal Union, mpira unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa .
Mechi ya mzunguko wa kwanza kule CCM Mkwakwani jijini Tanga, timu hizi zilishindwa kufungana.
Mechi nyingine yenye mvuto leo hii ni baina ya vinara, Azam fc dhidi ya JKT Oljoro.
Oljoro wapo nafasi ya 13 wakijikusanyia pointi 15 tu na wapo katika hatari ya kushuka daraja.
Wataingia kwa lengo la kusaka pointi tatu muhimu, lakini Azam fc ambao hawajafungwa katika mechi 20 walizocheza, wanahitaji pointi tatu ili kuwasomesha namba Yanga wanaowafuatia kwa tofauti ya pointi moja baada ya ushindi wa jana wa mabao 3-0 dhidi ya Rhino Mjini Tabora.
Endapo Azam fc watashinda leo, watafikisha pointi 47 kileleni na kuwaacha Yanga kwa pointi 4,wakati huo huo Yanga watakuwa wanasubiri mchezo wa machi 26 (jumatano) dhidi ya Tanzania Prisons, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kama Yanga watashinda mechi ijayo na Azam fc kufungwa leo au kutoka sare basi, Azam fc atakuwa amepinduliwa kileleni.
Lakini kama Azam fc atashinda leo na Yanga atashinda jumatano, bado wanajangwani wataendelea kuisoma namba kwa Azam fc.
Mechi nyingine za leo ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment